Habari za Punde

Maandalizi ya Kumwapisha JPM Yakamilika

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maandalizi ya uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo Novemba 4, 2020, ambao utatumika kwa ajili ya uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakaofanyika, kesho Novemba 5, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maandalizi ya uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo Novemba 4, 2020, ambao utatumika kwa ajili ya uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakaofanyika, kesho Novemba 5, 2020.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa leo amekagua maandalizi ya hafla ya kumwapisha Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli itakayofanyika Novemba 5, 2020 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akiongeoa na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma mara baada ya viongozi kukagua uwanja Jamhuri Dodoma utakaotumika kwa hafla ya kitaifa ya kumwapisha Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na. Eleuteri Mangi na Jonas Kamaleki- MAELEZO, Dodoma

Maandalizi ya hafla ya kumwapisha Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli itakayofanyika Novemba 5, 2020 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma  yamekamilika.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi mara baada ya viongozi kukagua uwanja huo utakaotumika kwa hafla ya kitaifa ya kumwapisha Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa mara ya kwanza kiapo cha Rais kinafanyika hapa Dodoma, ni jambo la kihistoria ambalo wananchi wanapaswa kulifahamu. Uwanja wa Jamhuri Dodoma upo tayari kwa ajili ya shughuli ya kesho maandalizi yote yamekamilika”, amesema Dkt. Abbasi.

Katika kufanikisha shughuli hiyo, Dkt Abbasi amesema kuwa nchi yetu itapokea ugeni mkubwa ambao utashiriki kwenye kiapo cha Mhe. Rais Mteule, Dkt. Magufuli ambapo watakuwepo viongozi wakuu wa nchi au wawakilishi wa wakuu hao wapatao 20 ambao wamethibitisha kushiriki.

Marais ambao wamethibitisha kuwepo kwenye hafla hiyo ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Comoro Azali Assoumani na Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.

Viongozi wengine ambao wamethibitisha kushiriki ni  ni pamoja na Mawaziri Wakuu, Makamu wa Rais wa nchi mbalimbali za Afrika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ambaye atamwakilisha Mfalme wa huko.

Aidha, Rais Mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo na Nabii TB Joshua watashiriki pamoja na   mabalozi 83 wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini

Katika hafla hiyo watashiriki pia viongozi waandamizi wa Serikali wakiwemo Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, viongozi wa taasisi za umma na binafsi, viongozi wa siasa, viongozi wa dini pamoja na Mawaziri na Manaibu Mawaziri wanaomaliza muda wao.

Fauka ya hayo, Dkt. Abbasi amesema kuwa viongozi wote walioalikwa ambao wana kadi za mwaliko, magari yao yatapaki Bustani ya Chinangali karibu na uwanja wa ndege wa Dodoma ambapo watapanda mabasi kuwapeleka eneo la tukio.

Hafla hiyo itakuwa na sehemu mbili ambapo kutakuwa na gwaride la kiapo litaongozwa na majeshi ya ulinzi na usalama na sehemu ya burudani ambayo itawashirikisha wasanii mbalimbali nchini ikizingatiwa Tanzania ni nchi ya amani na ni siku ya furaha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.