Habari za Punde

MWENYEKITI BARAZA LA VIJANA ZANZIBAR AZUNGUMZA NA VIJANA

Kijana Mzalendo Aisha Khatibu Juma (katikati) anamuomba Rais wa  Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk.Hussein Ali Mwinyi kuliboresha Soko la Mombasa ili kukuza hadhi ya Biashara kwa vijana huko  Soko  la Wajasiriamali Mombasa Zanzibar. (kushoto)  Mwenyekiti wa Baraza la  Vijana Zanzibar  Khamis Rashid Kheir (makoti).
Mwenyekiti wa Baraza la  Vijana Zanzibar  Khamis Rashid Kheir (makoti) ampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kushinda ushindi wa kishindo na  kuanza kutekeleza majukumu yake,  wakati alipotembelea Soko la mboga mboga Mombasa kuwapongeza vijana kwa kumchagua Dk. Mwinyi.
Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 04/11/2020.

Baraza la Vijana Zanzibar limempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Husein Ali Mwinyi kwa kupata ushindi mkubwa na kuahidi kumuunga mkono ili kuweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir ameyasema hayo wakati alipofanya ziara katika Soko la Mombasa  ili kuwapongeza vijana kwa kumpigia kura Dk. Mwinyi na   kubaini changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa Soko hilo.

Alisema Vijana wanamatumaini ya  kupata mwendo kasi wa kimaendeleo kutoka kwa Dkt. Hussein Mwinyi kutokana na ahadi alizozitoa wakati wa Kampeni.

Aidha alisema Vijana wameahidi kushirikiana nae katika kutekeleza majukumu yake na kutoa ushauri kwa viongozi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao  ipasavyo.

‘’Sisi Vijana tunahitaji Viongozi wanaotekeleza majukumu vizuri na kuleta mabadiliko,hatuhitaji Viongozi wazembe wanaoleta mbwembwe na kiburi na kushindwa kujali majukumu waliokabidhiwa’’alisema Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo amewataka viongozi na watendaji kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuhakikisha wanaleta maendeleo kwa Wananchi.

Nae Mwenyekiti wa Vijana Magharibi “B” Hassan Ali Nasour amewataka vijana kujishirikisha katika kufanya kazi za ujasiriamali  wasikae vijiweni ambako kutawasababisha kujiingiza katika vitendo viovu

Alieleza tutegemee  maendeleo kwa vijana kwani katika ahadi za Rais wa Zanzibar ni pamoja na  kuawawezesha wavuvi kufika bahari kuu, na kuvua samaki wenye viwango kwa wingi na kuwapatia maslahi makubwa.

Akizungumzia kuhusu wafanyabiashara wa soko hilo aliwataka kutegemea mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kiutendaji kwa kutatuliwa matatizo yanayowakabili ambayo hurudisha nyuma ufanisi wa kufanyabiashara zao.

Nao wafanyabiashara hao waliomba kupatiwa Soko la kudumu kwani wamekuwa wakihamishwa kila sehemu na kusababisha kupoteza wateja wao wa awali. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.