Msimamizi wa Mradi upande wa Mkandarasi (Dimetoclasa Real Hope Limited) Mhandisi John Bhoke akieleza kuhusu hali ya maendeleo ya ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Carolyne Nombo. Ujenzi unaoendelea katika Kampasi hiyo ni pamoja na kumbi za mihadhara, Hosteli za wanafunzi, Kituo cha Afya, Nyumba za wtumishi na Bwalo la Chakula.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo ametembelea eneo la ujenzi wa
Kampasi mpya ya Chuo iliyopo Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, mnamo tarehe 2 Julai
2025 na kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo. Ziara hiyo imelenga kufuatilia
maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kampasi hiyo ikiwa ni ufadhili
wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Prof. Nombo alipata fursa ya
kukagua hatua mbalimbali za ujenzi wa majengo yanayojengwa katika eneo hilo, na
kujionea kasi pamoja na viwango vya ubora vinavyotumika. Akiwa kwenye ukaguzi
huo, Prof. Nombo alitoa pongezi kwa namna kazi inavyoendelea na akasisitiza
kuwa Menejimenti ya Chuo inapaswa kuhakikisha usimamizi wa karibu ili kazi
zikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Aidha, Prof. Nombo
alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa kozi za amali katika kampasi hiyo, ambazo
zitamjengea mwanafunzi uwezo wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli
za kiuchumi. Pia alieleza kuwa uwepo wa baadhi ya wajumbe wa Menejimenti katika
ukaguzi huo ni jambo jema litakalosaidia usimamizi madhubuti na kuharakisha
utekelezaji wa mradi kwa ufanisi zaidi.
Prof. Nombo amemtaka
Mkandarasi kuzingatia ubora katika kila hatua ya ujenzi na kuhakikisha kuwa
mradi unakamilika kwa wakati ili wanafunzi waanze kudahiliwa ifikapo mwaka wa
masomo ujao. Vilevile, Prof. Nombo alihimiza matumizi ya vijana waliomaliza
mafunzo ya ufundi kupitia vyuo vya VETA, hasa wale wanaotoka mkoa wa Tanga, ili
kuwapa fursa ya kuchangia katika ujenzi wa kampasi hiyo na kunufaika kiuchumi.
Pia alisisitiza umuhimu wa ukusanyaji wa takwimu kuhusu namna jamii ya Kata ya
Gombero imenufaika na uwepo wa mradi huu, hususani kwa upande wa ajira, huduma,
na fursa nyingine za kiuchumi.
Prof. Nombo amesisitiza kuwa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaendelea kufuatilia kwa karibu
utekelezaji wa miradi yote ya elimu ya juu nchini, kuhakikisha inatekelezwa kwa
ubora, kwa wakati, na kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma.
Awali, Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, aliwasilisha taarifa ya maendeleo ya ujenzi
ambapo alieleza kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia
57.5. Alifafanua kuwa hosteli za wanafunzi zimekamilika kwa asilimia 58, nyumba
za watumishi kwa asilimia 68, jengo la taaluma kwa asilimia 57, bwalo la
chakula kwa asilimia 56 na kituo cha afya kwa asilimia 58.
Alieleza kuwa licha ya
changamoto za hapa na pale, mradi unaendelea kwa kasi nzuri kutokana na
ushirikiano wa karibu kati ya Chuo, Mkandarasi na wadau wengine wanaohusika
katika utekelezaji na usimamizi wa mradi huo
Katika ziara hiyo, Prof. Nombo aliambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Chuo pamoja na timu ya Mkandarasi wa Ujenzi kutoka kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Ltd.
No comments:
Post a Comment