Kamishna Idara ya Michezo Zanzibar Ameir Mohamed Makame amekabidhi Hati ya Ujenzi wa Viwanja vya Michezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya AE&Q consultant ltd huko katika eneo la Skuli ya Unguja Ukuu Wilaya ya Kati.
Zaidi ya Sh. Bilioni 5 zinatarajiwa kutumika katika Mradi wa Ujenzi wa Viwanja vya Michezo vya Unguja Ukuu Mkoa wa Kusini Unguja.
Kamishna Idara ya Michezo Zanzibar Ameir Mohamed Makame ameyasema hayo wakati wa makàbidhiano ya Hati ya Ujenzi wa Viwanja katika eneo la Skuli ya Unguja Ukuu Wilaya ya Kati.
Amesema Ujenzi wa Viwanja hivyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi baada ya maombi ya Wananchi kujengewa viwanja vya michezo katika eneo hilo.
Amesema Ujenzi wa Viwanja hivyo, vitasaidia kutoa fursa kwa jamii kutumia, ikiwemo Wanafunzi, Walimu na Wakaazi wa eneo na maeneo ya jirani kuepuka kufuata viwanja vya michezo maeneo ya mbali.
Aidha amesema Viwanja hivyo vitatumika kwa mashindano mbali mbali kama vile ya elimu bila malipo, Ndondo Cup na Mikutano ya kitaifa ambapo yataweza kuibua vipaji mbalimbali vya vijana.
Hata hivyo amewataka Wakandarasi wa Ujenzi wa Mradi huo, kufanyakazi kwa bidii ili kuhakikisha wanamaliza kwa mujibu wa makubaliano yaliofikiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Wananchi wa Unguja ukuu, Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli hiyo, Mussa Maulid Khamis ametoa shukrani kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Husein Ali Mwinyi kwa kuwakubalia ombi la kuwajenga viwanja hivyo.
Sambamba na hayo wasema Viwanja hivyo, vitakuwa chachu ya maendeleo kwa kuzalisha vipaji vya Vijana na kuweza kuleta tija kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla na kuweza kufikia malengo yaliokusudiwa.
Nae Naibu Waziri wa Michezo katika Skuli ya Unguja ukuu Fabian Masimbuko Kitundo amesema kukamilika kwa ujenzi huo, kutawasaidia kuibua vipaji vya Wanafunzi sambama na kuepuka kujishirikisha na vitendo viovu, ikiwemo utumiaji wa Dawa za kulevya na Bangi.
Kwa upande Mshauri elekezi kutoka Kampuni ya AE&Q consultant ltd, Feisal Fadhil Soud amesema Ujenzi wa Viwanja hivyo, utajumiisha viwanja vya michezo mbalimbali kama vile kiwanja cha Mpira wa miguu na vyengine vidogovidogo kama vile Mpira wa mikono, Wavu, Meza, Pete.
Mara baada ya makabidhiano hayo, Kamishna wa Idara ya Michezo Zanzibar Ameir Muhammed Makame ametembelea viwanja vya Michezo Kitogani na Mwehe Makunduchi ambapo amewapongeza Wakandarasi wa Ujenzi wa Viwanja hivyo kwa hatua nzuri ya Ujenzi waliofikia.
Imetolewa na Kitengo cha Habari,
WHVUM.
No comments:
Post a Comment