Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Afanya Ziara Bandari ya Zanzibar Malindi Leo.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa  Shirika la Bandari Zanzibar alipotembelea Bandari ya Malindi Jijini Zanzibar kujionea  uendeshaji wa Bandari hiyo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametembelea Bandari ya Malindi Jijini Zanzibar pamoja na eneo la Maruhubi kwa ajili ya kutafuta muwarubaini wa ucheleweleshwaji wa kutolewa kwa mizigo bandarini hapo.

Ziara hiyo ya Dk. Husein Mwinyi ni ya kwanza kuifanya  mara tu baada ya kushika wadhifa wa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambapo alifika bandarini hapo kujua sababu zinazopelekea kuchelewa kushushwa kwa mizigo , mlundikano wa makontena  pamoja na meli kukaa kwa muda mrefu nje ya Bandari hiyo.

Katika maelezo yake Dk. Hussein Mwinyi alisisitiza kufanyika  jitihada za  makusudi za kutafuta ufumbuzi wa kuondoa makontena bandarini hapo kwa lengo la   kuondosha usumbufu na mlundikano wa makontena katika eneo hilo.

Rais Mwinyi alisema kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea sana bandari na pale pasipokuwepo ufanisi katika utendaji wa shughuli zake ni dhahiri kwamba uchumi hauwezi kuimarika.

Aliongeza kwamba katika hali ya sasa  kuna meli zinateremsha mizigo katika bandari za Mombasa na Dar es Salaam na hivyo kuleta usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara kiasi ambacho huwasababishia kupata hasara.

Alisema kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara walioamua kutokuleta mizigo yao Zanzibar kutokana na mizigo yao kukaa kwa muda mrefu, hivyo alisisitiza haja ya kutafutiwa ufumbuzi wa changamoto hiyo.

Rais Dk. Husein aliutaka uongozi huo wa bandari kuongeza kasi ya ushushaji wa mizingo ili kupunguza muda wa kukaa meli muda mrefu nje ya bandari.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa kumekuwepo changamoto ya kupanda bei kwa bidhaa kiholela kutokana na utendaji wa bandari.

Alisisitiza haja ya kuwepo kwa eneo la kuweka makontena (bandari kavu) ili kuondosha mlundikano wa makontena katika eneo hilo la bandari ya Malindi.

Hivyo, Rais Dk. Hussein aliusisitiza uongozi huo haja ya kuwajibika kwa kufahamu kuwa bandari ni kitovu cha uchumi wa nchi huku akizuia utumiaji wa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya upembuzi yakinifu katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kuweka makontena (bandari kavu) huko Maruhubi.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliutaka uongozi huo kutumia fedha walizonazo ili kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma za bandari.

Akitoa maelezo Mkurugenzi Mwendeshaji Juma Sururu Juma alisema kuwa miongoni mwa sababu za zinazosababisha kuwepo mlundikano wa makontena bandarini hapo ni kuchelewa kwa baadhi ya wafanyabiashara kutoa mizigo yao pamoja na masuala mengine ya kiofisi.

Aidha,  Mkurugenzi huyo alieleza shughuli za bandari hiyo ya Malindi huku akieleza kuwa mizigo ambayo haichelewi kutolewa bandarini hapo ni pamoja na ile ya  vyakula, saruji na mafuta hizo ni bidhaa zinazoletwa na wafanyabishara maalum.

Akieleza kuhusu ukaaji wa meli Bandarini hapo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa meli haikai zaidi ya siku tano na tayari inakuwa imeshaondoka hasa ikizingatiwa kwamba shughuli hizo zinafanywa usiku na mchana.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Ali Haji Haji alieleza kuwa katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo lilipatikana eneo la Maruhubi kwa ajili ya eneo la makontena (bandari kavu) na ndilo wanalokusudia kulifanyia shughuli hizo.

Viongozi hao katika maelezo yao walieleza kuwa msongamano wa makontena ndio sababu inayopelekea ufinyu wa nafasi katika eneo hilo la bandari ya Malindi.

Kaimu huyo Mkurugenzi alimueleza Rais Dk. Hussein kuwa pindipo itapatikana nafasi wataweza kutumia zamu tatu za kufanya kazi kwa siku na hivyo, kuondokana na tatizo la meli kukaa nje ya bandarini muda mrefu.

Pamoja na hayo, viongozi hao walieleza kuwa njia moja wapo ya kutatua tatizo hilo na kupata muwarubaini wake ni kuanzisha eneo la kuwekea makontena (bandari kavu) ambalo katika mitizamo yao waligundua eneo hiklo la Maruhubi.

Rais Dk. Hussein alitembelea eneo hilo la Maruhubi lililotengwa na Shirika hilo la Bandari kwa ajili ya kuweka makontena (bandari kavu) huku Kaimu Mkurugenzi huyo akieleza kuwa ni vyema bandari hiyo ikawa  karibu na badari kuu ili kupunguza gharama na kubainisha kuwa kazi zote za kupeleka na kuondoa makontena matupu zitafanyika wakati wa usiku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.