Habari za Punde

Siku ya Takwimu Afrika kuadhimishwa tarehe 18/11/20 ili kuelewa umuhimu wa takwimu kijamii na kiuchumi

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mayasa Mahfoudh akizungumza na waandishi wa habari juu ya suala zima la takwimu,  ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra kuelekea siku ya takwimu Afrika huko Ofisini kwake Mazizizni Zanzibar.


 Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mayasa Mahfoudh akizungumza na waandishi wa habari juu ya suala zima la takwimu,  ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra kuelekea siku ya takwimu Afrika huko Ofisini kwake Mazizizni Zanzibar .


PICHA NA FAUZIA MUSSA /MAELEZO

Issa Mzee,Maelezo      16/11/2020

Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar inatarajia kuadhimisha siku ya takwimu barani Afrika ifikapo tarehe 18 mwezi huu kwa lengo la kuhamasisha jamii katika umuhimu wa takwimu kwa maendeleo ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari  Mazizini Zanzibar  Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mayasa Mahfoudh amesema Tanzania ikiwemo Zanzibar ni miongoni mwa nchi za Afrika ambayo imeridhia kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuongeza uelewa kwa jamii juu ya umuhimu wa takwimu kijamii na kiuchumi nchini na  Afrika  kwa ujumla.

“Tunapoadhimisha siku ya takwimu Afrika tunakusudia kuihamasisha jamii kuhusu umuhimu na jukumu la kila mmoja wetu katika ukusanyaji ,uchambuzi , na uwasilishaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya nchi zetu za Afrika”. Alisema Mtakwimu Mkuu

Alisema kuwa miongoni mwa malengo makuu ya siku ya takwimu Afrika ni pamoja na kuongeza uelewa juu ya uratibu na uaptikanaji wa takwimu rasmi,kufanya majadiliano  kati ya wazalishaji na  watumiaji wa takwimu rasmi na kuishirikisha jamii na sekta binafsi katika uzalishaji ,usambazaji na kutumia takwimu zilizo rasmi.

Aidha alisema maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mageuzi makubwa katika tasnia ya takwimu katika nyanja zote za utoaji na utumiaji wa takwimu kuanzia ukusanyaji ,uchambuzi,uwasilishaji na hata ubadilishanaji wa taarifa za kitakwimu.

“Ukusanyaji wa taarifa umekuwa ukifanywa kwa ufanisi zaidi hivi sasa ikilinganishwa na hapo zamani hii ni kutokana na matumizi ya vifaa  ikiwemo simu janja ,vishikwambi ambavyo  vinawezesha taarifa kukusanywa kutoka sehemu mbalimbali na kuwasilishwa ofisini kwa muda huo huo kwa njia ya mtandao” alisema mtakwimu

Alifafanua kuwa teknolojia inatumika katika tafiti zote zinazofanywa na Mtakwimu Mkuu Wa Serikali  zimewezesha kupungua kwa gharama za ukusanyaji taarifa,kupungua kwa muda wa ukusanyaji na uchakataji taarifa na kuongezeka kwa ubora wa taarifa zinazokusanywa.

Aidha alisema Ofisi ya Mtakwimu Mkuu itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa takwimu,jamii na nchi mbalimbali za Afrika ili kutimiza jukumu la dhamana ya kuwa na mamlaka ya utoaji wa takwimu bora na sahihi.

Vilevile Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali inaomba wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla kutoa mashirikiano ya dhati katika suala zima la utoaji taarifa sahihi ili kuwa na takwimu bora na sahihi kwa maendeleo ya nchi.

Siku ya takwimu barani Afrika huadhimishwa kila ifikapo tarehe 18 Novemba ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema “uimarishaji wa mifumo ya kitaifa ya takwimu kwa ajili ya utoaji wa taarifa na takwimu, ili kuwepo kwa amani na maendeleo endelevu barani afrika”

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.