Habari za Punde

WAZIRI WA NCHI (OR) KATIBA SHERIA UTUMISHI NA UTAWALA BORA AAHIDI JENGO JIPYA OFISI YA MUFTI

 Waziri wa Nchi (OR)  Katiba Sheria  Utumishi na Utawala bora Haroun Ali Suleiman akizungumza na watendaji mbalimbali wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana huko Mazizini Zanzibar.
Na Sabiha Khamis    Maelezo    27/11/2020                                                   

Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora Haroun Ali Suleiman ameahidi kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga afisi mpya ya Mufti Zanzibar ili kuweka mazingira bora na kuleta ufanisi wa kazi.

Akizungumza na watendaji wa ofisi hiyo huko Mazizini katika muendelezo wa ziara ya kutembelea Idara zote zilizopo chini ya Wizara yake alisema ipo haja ya kuwepo jengo litakalo kidhi mahitaji ya watendaji ili kuweza kufanya kazi katika kiwango kinachotakiwa.

Alisema kupatiwa jengo jipya la ofisi kutasaidia katika kufanyakazi na kutekeleza majukumu kwa ufanisi mkubwa, utulivu na kuwawezesha watendaji wote wa ofisi hiyo kuwa na ofisi zao kwani bado wapo baadhi ya watendaji ambao hawana ofisi za kutosha.    

“Jitihada zinazofanywa na ofisi hii ni kubwa na zina umuhimu mkubwa kwa jamii katika utoaji wa fat-wa, utatuzi wa migogoro na usimamizi wa masuala ya Kiislamu ninawaomba watendaji kulinda na kuendeleza maadili mema yaliojengeka kwa utamaduni wa Kiislamu, hivyo ipo haja ya kupatiwa jengo la kutosha kwa maendeleo ya nchi yetu” Alisema Waziri.

 Aidha amesema ameridhishwa na jitihada zinazochukuliwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo za kutoa taaluma kwa wananchi ambazo zimeleta amani na utulivu katika Nchi.

Aliwataka wafanyakazi wa Ofisi ya Mufti kuendelea kufanyakazi kwa ushirikiano ili kuongeza ari, nguvu uzalendo katika utendaji wa kazi.

Kwa upande wake Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi amemshukuru Waziri huyo kwa kuonyesha ushirikiano na kuahidi kutoa ushirikano wa dhati kwa Wizara ili kuijenga jamii iliyo bora na yenye maadili mema.

Aidha katika ziara hiyo Waziri Haroun alitembelea Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Mazizini na kufanikiwa kuzungumza na watendaji wa Ofisi hiyo ambao walitoa changamoto zao ikiwemo maslahi ya wafanya kazi.

Akitoa changamoto hizo Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Abdulla Talib Abdulla alisema uhaba wa wafanyakazi na fedha unasababisha kuzorota kwa utendaji wa kazi katika kamisheni hiyo.

Kwa upande Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi na Utawala Bora Yakuti Hassan Yakuti amesema suala la maslahi ya wafanyakazi liliwahi kufanyiwa kazi lakini hali ya kifedha haikuwa nzuri lakini bado suala hili linaendelea kufatiliwa na kuwataka wafanyakazi hao kuwa wastahamilivu kwani uongozi uliopo utatatua matatizo hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.