Habari za Punde

Dkt.Abbasi kuwa Mlezi wa THT

Msimamizi wa Kituo cha Tanzania House of Talents (THT) Kemmy Mutahaba ambaye akimshukuru Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi (hayupo pichani) kwa kutembelea kituo hicho

Baadhi ya Vijana wenye vipaji katika Sanaa ya Muziki wanaolelewa na kituo cha Tanzania House of Talents (THT) na viongozi wa kituo hicho wakiwa katika picha ya pamoja na  na  Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi aliyeketi (watatu kushoto) leo Desemba 04, 2020 Jijini Dar es Salaam, alipotembelea kituo hicho kwa lengo la kuona namna kinafanya kazi na kuahidi kuwa mlezi wao.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi ameielekeza Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo kuanza kushirikiana na Tanzania House of  Talents (THT) katika  mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa Muziki.

Dkt. Abbasi ametoa kauli hiyo leo Desemba 04, 2020 alipotembelea kituo hicho kilichopo Jijini Dar es Salaam, kuangalia maendeleo ya vijana wanaolelewa na kituo hicho kilichokuwa kimeanzishwa na marehemu Ruge Mutahaba kwa lengo la kukuza vipaji vya sanaa ya muziki kwa vijana na  kuwajengea uwezo wa kujiendeleza .

Akizungumza katika ziara hiyo Dkt.Abbasi alisema wizara inatambua mchango wa THT katika kukuza tasnia ya muziki na inaheshimu vipaji vya vijana wanaolelewa na taasisi hiyo, pia inafahamu maono ya mwanzilishi wake kuhusu kuendeleza kituo hicho na ipo tayari kuwapa ushirikiano.

“Nitaunganisha wadau wote wenye nia na mapenzi mema ya kukuza  Sanaa na kuendeleza kituo hichi, nikiwemo mimi mwenyewe ili tuwe walezi wa THT kwa kipindi chote,” alisema Dkt.Abbasi.

Pamoja na hayo nae Msimamizi wa Kituo hicho kwa sasa Kemmy Mutahaba alieleza kuwa THT imekuwa ikifanya kazi kwa takribani miaka 15 sasa, na kazi yake kubwa ni kuibua na kukuza vipaji vya vijana  katika tasnia ya Muziki ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“THT imekuwa ikilea vijana katika misingi ya uzalendo kwa kusimamia  msemo huu wa marehemu Ruge  kuwa Watu wenye njaa ya mafanikio hawatazami ukubwa wa changamoto, wanatazama ukubwa wa ndoto,” alisema Kemmy.

Halikadhalika nae mama Mzazi wa Marehemu Ruge Christina Mutahaba ambaye ndiyo mwanzilishi wa kituo hicho alitoa ombi kwa serikali kuendelea kutoa ushirikiano wa kuendeleza kituo hicho cha THT ili kuendelea kuishi ndoto za mwazilishi wake..

Akihitimisha ziara hiyo Dkt. Abbasi alisema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na kituo hicho , pia alitembelea  studio ya kituo hicho na kuahidi kutafuta wadau watakaosaidia upatikanaji wa vifaa ambavyo ni vibovu, pia aliwasihi kushiriki katika Tamasha la Serengeti Music and Arts Festival linaloandaliwa na serikali na litafanyika Desemba 26,2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.