Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais, Mhe Hemed ateta na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mazingira Mh. Ummy Ali Mwalimu

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdullah, Kulia akielezea umuhimu wa kuzingatia suala ya Tabia Nchi ili kulinda mazingira alipozungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mazingira Mh. Ummy Ali Mwalimu aliyefika kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mazingira Mh. Ummy Ali Mwalimu aliyekaa kati kati akimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed kutekeleza jukumu lake kwa umakini mkubwa.
Mheshimiwa Hemed Suleiman akimpa matumaini ya Waziri Mwalimu jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakavyoendelea kutoa ushirikiano wa kina ili Sekta ya mazingira ifanyiwe kazi kwa umakini mzuri.

 Waziri Ummy Mwalim akielezea faraja yake kutokana na Viongozi na Watendaji wa Taasisi za Umma pande zote mbili za Muungano kuanza vikao vya majadiliano na kuchukuwa hatua za kutatua kero zilizobakia za Muungano.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman alisema katika suala zima la kuendelea kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchini ipo haja kwa Wataalamu wa Sekta za Mazingira Nchini kuangalia kwa kina uvamizi wa Maji ya Bahari yanayoendelea kukiathiri Kijiji cha Sipwese kiliopo Mkoa Kusini Pemba.

Alisema Wananchi wa Kijiji hicho  hivi sasa wanaendelea kupata usumbufu mkubwa kutokana na sehemu wanayovukia kwenda upande wa Vijiji Jirani kuvamiwa na mmong’onyoko kukubwa wa ardhi unaosababishwa na kasi ya Maji ya bahari na kuhatarisha pia maisha ya Watoto wanaokwenda Skuli.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia masuala ya Muungano na Mazingira wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Ummy Ali Mwalimu aliyefika kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti kutoa Ushirikiano ya kina katika kuona kero hilo la Sipwese linapatiwa ufumbuzi kama ilivyoshughulikiwa changamoto ya athari ya Tabia Nchi iliyokikumba Kisiwa Panza chini ya usimamizi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano kwa Ujenzi Daraja na upandaji miti mambo yaliyoleta afueni kwa Wananchi wa Kisiwa Panza.

Mheshimiwa Hemed alieleza kwamba yapo matumaini makubwa ya kuendelea kuimarika Zaidi kwa Muungano wa Tanzania kutokana na Marais wote wawili Zanzibar na Tanzania kwa kuwateuwa Mawaziri madhubuti wenye nguvu ya kusimamia masuala ya Muungano.

Alisema hana shaka ya Mawaziri hao Wawili waliokwishaonyesha muelekeo wenye matumaini mema kwa kuanza kusimamia Vikao vya Wataalamu na Viongozi wa pande hizo mbili kuyaangalia maeneo ambayo yana dalili za changamoto za Muungano kwa pande zote mbili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Waziri Ummy Ali Mwalimu kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo ambayo pamoja na mambo mengine inahusika moja kwa moja na masuala ya Muungano ambae ana sifa zote hasa kutokana na umakini wake wa kuitendea Haki Tanzania wakati wa Taifa lilipopata maambukizi ya Virusi vya Corona wakati akiwa Waziri aliyesimamia masuala ya Afya.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira Mheshimiwa Ummy Ali Mwalimu alisema Wizara yake imepewa kazi nzito ya kuratibu masuala ya Muungano sambamba na Mazingira kwa pande zote mbili.

Hata hivyo Waziri Ummry alisema bado pia wanapaswa kuimarisha masuala ambayo yako nje ya Muungano lakini yanajumuisha Moja kwa Moja Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa upande wa Zanzibar ambayo inapata dhamana ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mh. Ummy alielezea faraja yake kutokana na Wataalamu na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya  Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuanza Majadiliano  ya kidugu katika utekelezaji wa changamoto zilizopo kwenye Sekta ya Mazingira.

Alisema hatua za haraka za kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchini zimeanza kuchukuliwa hasa ikizingatiwa kwamba mazingira ya Visiwa vya Zanzibar yanalingana kwa karibu na yale yaliyopo katika mwambao wa Ukanda wa Mashariki Mwa Tanzania Bara.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mzingira Mh. Ummry Ali Mwalimu alikutana kwa mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi Dr. Khalid Salum Mohamed.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Vuga Mjini Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed alisema pande hizo mbili zinapaswa kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika Taasisi za Kiutendaji badala ya kusubiri kutatua Kero za Muungano.

Wakichangia katika Mkutano huo baadhi ya Viongozi Waandamizi wamehimiza kuwepo kwa mawasiliano ya karibu yatakayorahisisha Utendaji na Utekelezaji wa Miradi inayoanzishwa ikigusa pande zote mbili za Muungano.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mzingira Mh. Ummry Ali Mwalimu alifanya ziara maalum Visiwani Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha Rasmi kwa Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.