Habari za Punde

Mapinduzi Cup kutimua vumbi, Yanga na Simba kushiriki


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Omar Hassan King akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu Michuano ya Mapinduzi Cup hafla iliyofanyika Ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale.

Na  Rahima Mohamed / Mariam Kidiko  - Maelezo   

Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo  Omar Hassan King  amewataka wananchi kushiriki katika  michuano ya Mapinduzi Cup kwa lengo la kuleta umoja na kuimarisha sekta ya michezo nchini.

Hayo ameyasema  katika ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni Mjini Unguja wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema mashindano hayo yanatarajiwa kuwa na makundi manne makubwa ambayo yataandaliwa kitaifa.  

Alisema makundi hayo ni kama vile Mapinduzi Cup ya wakubwa, mashindano yatakayoshirikisha Wizara na taasisi za Serikali ya Zanzibar  na Tanzania zilizopo Zanzibar , ZBC Mapinduzi Cup watoto pamoja na  Mapinduzi Cup ya timu za wanawake.

Alifafanua kuwa  Mapinduzi Cup wakubwa yatashirikisha timu za Zanzibar na Tanzania Bara ambapo timu tisa zitashiriki katika mashindano ikiwemo timu ya Simba, Yanga, Mlandege, Mtibwa Sugar, Malindi, Jamuhuri, Chipukizi, Namungo na timu ya Azam.

Alisema  kwa  upande wa  mashindano yanayoshirikisha Wizara,Taasisi na mashirika ya Serikali ya Zanzibar  na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ofisi zake zipo Zanzibar.

Vilevile alisema mashindano ya ZBC Mapinduzi Cup watoto  yatashirikisha vijana wenye umri  mdogo  kutoka Wilaya  kumi na moja za Zanzibar kwa lengo la kuibua  vipaji .

Hata hivyo alisema kwa mwaka huu wanategemea kuwa na mashindano ya Mapinduzi Cup ambayo yatashirikisha timu za wanawake na  yaataandaliwa na  Shirikisho la soka Zanzibar .

Michuano hiyo yanatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao  kwa kutegemea  ratiba ya ligi za Tanzania  Bara  sambamba  na kuunda kamati maalum kwa ajili ya kuratibu mashindano hayo.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.