Habari za Punde

Tatizo la Maji Kongwa kuwa Historia

 

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kutoka kushoto) na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Kongwa katika ziara ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji Wilayani Kongwa. 

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akizungumza na wananchi katika ziara ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji katika Kiijiji cha Ndurugumi ,Wilayani Kongwa. Kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Ndugai.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Ndugai akizungumza na wananchi katika ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto ) ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji Wilayani Kongwa.
Mkazi wa Kiijiji cha Ndurugumi, Bi. Leah Assenga akitoa maoni yake kuhusu upatikanaji wa maji katika ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani) ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji Wilayani Kongwa.
Mkazi wa Kiijiji cha Suguta, Bi. Anna Makoleko akitoa maoni yake kuhusu upatikanaji wa maji katika ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani) ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji Wilayani Kongwa.
Baadhi ya wakazi wa Kiijiji cha Ndurugumi wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji Wilayani Kongwa.


Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameahidi kushughulikia tatizo la upatikanai wa maji  lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2020/21 mpaka 2021/22.

Mhandisi Sanga ametoa ahadi hiyo alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero za upatikanaji wa maji  katika  Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa , jijini Dodoma.

"Tumetoa ahadi ambazo zinatekelezeka na kimsingi kazi za ujenzi wa mradi wa maji  katika kijiji cha Sugutu zitaanza jumatatu hii na nimeelekeza mradi huu ujengwe ndani ya miezi miwili na katika kijiji cha Ndurugumi kutajengwa mradi wa shilingi milioni 910 ndani ya miezi hii mitatu na kazi itaanza ndani ya siku 14 ", amezungumza Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu Mhandisi Sanga amezungumza kuwa miradi hiyo itakapomalizika itanufaisha na vijiji vingine vilivyo karibu na maeneo hayo.

 Aidha, Katibu Mkuu amewataka wananchi watakaopitiwa na miradi hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mitaro.

Awali, katika ziara hiyo baadhi ya wananchi wa vijiji vya Suguta na Ndurugumi walitoa malalamiko yao  juu ya changamoto za upatikanaji wa maji zinazowakabili.

Naye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Ndugai amewataka wananchi kutunza miundombinu ya maji ili miradi hiyo iwe endelevu.

"Lazima wawepo vijana wetu wa kukagua usalama wa hiyo miradi ili iwe endelevu kwa sababu tuna tabia tofauti, kwa mfano mwingine anatoboa usiku ili maji yaende nyumbani kwake, mwingine anatoboa ili maji yamwagike kwenye bustani yake, wengine wanapeleka mifugo na tabia nyinginezo kama hizo ", amefafanua Mhe. Ndugai.

Ziara ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Wilayani Kongwa ni mwendelezo wa ziara zake za kikazi katika kusikiliza kero za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji  na kuzipatia ufumbuzi. Ziara hiyo pia iliijumuisha kutembelea mradi wa uchimbaji wa visima katika kijiji cha Ibwaga na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Vihingo.

Kitengo cha Mawasiliano

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.