Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Askofu Mkuu wa Kinisa la Tanzania Assemblies of God Ikulu leo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Dr.Barnanas Welston Atokambali alipowasili katika ukumbi wa Ikulu kwa ajili ya mazungumzo yaliofanyika leo, 11/12/2020akiwa na Askofu wa Jimbo la Zanzibar Askofu  Dikson Kaganga,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Dr.Barnanas WelstonMtokambali wakati wa mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar akiwa na Askofu wa Jimbo la Zanzibar Askofu  Dikson Kaganga,
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza uongozi wa Kanisa la ‘Tanzania Assemblies of God’ (TAG) kwa kuendelea kuhubiri amani na kuliombea Taifa wakati wa uchaguzi, kabla na baada uchaguzi.

Rais Dk. Hussein aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kanisa hilo la ‘Tanzania Assemblies of God’ (TAG) ukiongozwa na Askofu Mkuu wa Tanzania Barnanas Weston Mtokambali akiwa amefuatana na Askofu wa Jimbo la Zanzibar Dikson Kaganga, uliofika Ikulu kwa ajili ya kumpongeza baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka huu 2020.

Katika maelezo yake, Rais Dk.  Hussein alitoa shukurani kwa uongozi huo kwa ujio wao sambamba na pongezi na maneno ya hekima waliyayatoa kwa Rais.

Rais Dk. Hussein alitoa pongezi kwa uongozi huo wa Kanisa la TAG kwa ushirikiano uliotoa Kanisa hilo katika kipindi chote cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2020 katika kuliombea amani Taifa.

Alisema kuwa katika kipindi cha Kampeni aliweza kukutana na waumini wa dini ya Kikristo wa madhehebu mbali mbali na kuzungumza nao ambapo pia na wao walieleza changamoto walizonazo ambapo aliahidi kuzifanyia kazi.

Aidha, Rais Dk. Hussein Mwinyi alitoa shukurani kwa Kanisa hilo kwa kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusema kwamba Serikali anayoiongoza itashirikiana na Kanisa hilo kwa kuthamini huduma inazozitoa kwani mbali ya huduma za kiroho pia, limekuwa likichangia katika sekta ya afya, elimu na maji na nyenginezo.

Alisema kuwa maombi yote ya wananchi yameweza kukubaliwa na Mwenyezi Mungu na hivi sasa tayari kuna maridhiano ambapo lengo lake ni kuondoa kasoro katika kada za kisiasa hivyo, aliwanasihi waumini wote kuendelea kuliombea Taifa.

Rais Dk. Hussein alimpongeza Askofu Dk. Barnanas Weston Mtokambali, kwa nafasi yake ya uongozi aliokuwa nayo kwa Tanzania na pia kuwa kiongozi mkuu wa Makanisa yote 48 ya TAG barani Afrika, Mjumbe wa Halmashauri ya Kanisa hilo katika makanisa 150 dunianina kueleza kuwa yeye akiwa Rais yuko tayari kushirikiana nae na milango yake iko wazi.

Mapema Askofu Dk. Barnanas Weston Mtokambali alimpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa niaba ya Maaskofu wote, waumini na viongozi wengine wa Kanisa hilo kwa ushindi wa kishindo alioupata katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka huu 2020.

Katika maelezo yake alimueleza historia ya Kanisa hilo ambalo lina Majimbo 71 hapa nchini likiwemo Jimbo la Zanzibar na kueleza kuwa Kanisa hilo lilianza rasmi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1927 na kuingia Zanzibar mwaka 1929 na mwaka 1939 lilipata usajili rasmi ambapo tayari limeshatimiza miaka 81.

Askofu Dk. Mtokambali alimpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kuonesha ukaribu mkubwa kwa madhehebu mbali mbali ya dini ya Kikristo wakati wa Kampeni na kuzipongeza hotuba zake alizokuwa akizitoa ambazo zimewapa mwanga mkubwa waumini hao na kusisitiza kuwa licha ya uchache wao lakini wamekuwa wakiishi salama hapa Zanzibar.

Kiongozi huyo pia, alipongeza uteuzi alioufanya Rais Dk. Mwinyi wa Mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi alietoka katika dini ya Kikristo Anna Athanas Paul ambaye alisema anatoka katika kanisa la TAG.

Aidha, alisema kuwa Kanisa lao hilo lina Sera tatu ambapo ya kwanza ni ya kiroho, ya pili ni kuendeleza utume wa kikristo na ya tatu ni kushiriki katika shughuli mbali mbali za maendeleo ambapo kwa upande wa Zanzibar wameweza kushirikiana vyema na Serikali zilizopita na kuahidi kushirikiana na Serikali hii ya Awamu ya Nane.

Amesema kuwa Kanisa hilo limekuwa likitoa msaada wa kuchimba visima, huduma za elimu na za afya Tanzania Bara na Zanzibar ambapo tayari kwa Zanzibar wana skuli tatu za kiengereza na wanatarajia kujenga moja huko kisiwani Pemba.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa Kanisa la TAG waliahidi kuendelea kushirikiana na Rais Dk. Hussein Mwinyi pamoja na kuendelea kumuombea ili aendelee kuwa kiongozi mwema na kuweza kuiongoza Zanzibar na watu wake pamoja na kuiletea maendeleo endelevu.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.