Kila sifa njema ni
zake Mwenyezi Mungu. Tunamshukuru Yeye kwa kutuwezesha kufika siku hii ya leo ambapo
tunauaga mwaka 2020na baada ya masaa machache tutaukaribisha mwaka mpya 2021.
Tuliuanza mwaka 2020 tukiwa pamoja na wenzetu ambao leo hii hatunao tena, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, wameshatangulia mbele ya haki. Tumuombe Mola wetu awape malazi mema peponi na sisi tulio hai atujaalie kila la kheri katika maisha yetu hapa duniani na atupe hatma njema. Amin!
Ndugu Wananchi,
Kipindi cha mwaka
mmoja ni kirefu katika maisha ya mwanadamu.Ndani ya kila mwaka hutokea mambo
mengi makubwa ambayo, baadhi yao, huacha alama na kumbukumbu za historia katika ngazi ya
kimataifa, kitaifa na hadi ngazi ya
familia na mtu mmoja mmoja. Bila ya
shaka, mambo yote hayayametokea katika mwaka 2020 ambao leo tunauaga.
Kwa ngazi ya Kimataifa, moja kati ya mambo makubwa yaliyotokea katika mwaka 2020 ni kuenea na kusambaa kwa maradhi ya Virusi vya Korona (COVID - 19) ambayo yalijulikana na kutangazwa rasmi mwezi wa Disemba, 2019.
Athari za maradhi ya COVID – 19kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni kubwa. Yamezusha hofu na taharukiisiyomithilika;bado athari zake zimegubika nyanja zote za maendeleo ya karne hii ya 21. Mataifa mengi duniani, hasa Ulaya na Amerika, yamekuwa yakiweka na kuondoa karantini, ambazo zinaathari kubwa kwa mwenendo wa watu bidhaa na huduma hali ambayo inaendelea kuathiri uchumi wa dunia.Wiki mbili zilizopita taharuki imeongezeka baada ya kuzuka kwa aina mpya yaVirusi vya Korona nchini Uingereza. Hadi tarehe 30 Disemba 2020 idadi ya watu walioambukizwa duniani imeshafikia milioni 81 na idadi ya vifo ni milioni 1.8. Nchi yetu inafuatilia kwa karibu habari hizi ili iwe inachukua hatua zinazofaa.
Athari za maradhi COVID - 19 kwa nchi za visiwa ni kubwa zaidi kutokana na utegemezi wa sekta za huduma, hasa utalii, kwa maendeleo ya kiuchumi; hali hiyo kama tunavyoendelea kushuhudia imejitokeza hapa Zanzibar.
Kwa hivyo tunauaga mwaka huu ikiwa kasi ya ukuaji wa uchumi wetu imeathirika sana kutokana na maradhi hayo. Ni vyema tukachukua changamoto zilizojitokeza kutokana na maradhi ya COVID -19 tukazifanyia kazi ili zisiendelee kuathiri kasi yetu ya utendaji na uwajibikaji. Kamwe, isiwe kwamba kuendelea kuwepo kwa maradhi ya COVID 19 katika mataifa mengine kuwa kisingizio au kikwazo kwa kila kitu tulichopanga kufanya kwa maendeleo yetu.
Ndugu Wananchi,
Kwa ngazi ya
Kitaifa, tutaukumbuka mwaka huu 2020 kwa
tukio la kuondokewa na Kiongozi wetu Mpendwa, Rais Mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Benjamin Mkapa ambae alifariki tarehe
24 Julai, 2020 na kuzikwa tarehe 29, Julai,2020 kijijini kwao Lupaso Mkoani
Mtwara. Tunamuomba Mwenyezi Mungu ampe malazi mema.
Vile vile, matukio mengine makubwa ya kukumbukwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni zoezi la Uchaguzi Mkuu ambalo limefanyika kwa hali ya amani na utulivu na hatimae kumuwezesha Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuendelea kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha Pili cha Serikali ya Awamu ya Tano anayoiongoza.
Watanzania tunaendelea kuukumbuka mwaka 2020 kwa maendeleo makubwa ya kiuchumi tuliyoyapata ndani ya mwaka huu chini ya Uongozi wa Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli.Benki ya Dunia ilitangaza rasmi kwamba Tanzania imeingia katika uchumi wa kipato cha kati ngazi ya chini kuanzia Julai mosi, 2020 tarehe ya kwanza ya mwaka mpya wa fedha. Mafanikio hayo, yameiwezesha nchi yetu kujiunga namataifa saba ya Afrika yaliyoKusini mwa Jangwa la Sahara yenye hadhi hiyo.Tujipongeze kwa kupiga hatua hiyoukizingatiwa kwamba kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Tanzaniaya 2025, ilitarajiwa kwamba tutafikia kiwango hicho ifikapo mwaka 2025. Bila ya shaka, hili ni jambo kubwa la kukumbukwa kwa mwaka huu 2020 tunaouaga.
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa Zanzibar, yako matukio mengi ya kihistoria
ambayo yatatufanya tuukumbuke mwaka huu 2020.Tutaukumbuka kwa tukio
lililotokea katika Mji Mkongwe wiki iliyopita, tarehe 25 Disemba, 2020 siku ya
Krismas la kuanguka sehemu kubwa ya
Jengo la ‘Beit El Ajaib’ na kusababisha vifo vya ndugu zetu wawili baada ya kufukiwa na kifusi na wengine kadhaa
kujeruhiwa. Vifo hivi vimeleta mshtuko
kwa wananchi wa Zanzibar.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu azilaze mahala pema peponi roho za marehemu wote. Kwa mara nyengine, tunatoa mkono wa pole kwa familia za marehemu. vile vile, tunamuomba Mwenyezi Mungu awape uzima na nguvu za kuendelea na maisha ya kawaida wale wote walioumia kutokana na ajali hiyo.
Kwa upande mwengine, tumehuzunika kutokana na kuharibika kwa jengo la Beit El Ajaib, ambalo ni mithili ya uso wa Mji wetu Mkongwe ambao tunaupenda na unapendwa duniani kote kutokana na Historia yake na uzuri wake.
Kwa hivyo, kwa pamoja, azimio letu la mwaka mpya 2021, liwe ni kuungana katika kutafuta njia bora na endelevu za kuulinda na kuuhifadhi Mji Mkongwe, ikiwa ni pamoja na kuyatekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa katika mkutano tulioufanya juzi tarehe 28 Disemba, 2020 baina ya Viongozi wa Serikali na Wadau mbali mbali wa Mji Mkongwe kwa lengo la kutafuta njia bora za kuuhifadhi na kuuendeleza. Tunamuomba Mwenyezi Mkungu atupe wepesi katika kutekeleza mambo hayo mema tuliyoyadhamiria.
Vile vile, tutaukumbuka mwaka 2020 kwa kufanya Uchaguzi Mkuu na kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa salama na amani.Katika mwaka huu tumeshuhudia kumalizika muda wa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba iliyokuwa ikiongozwa na Rais Mstaafu Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein na kuanza kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane ninayoiongoza mimi. Tumeshuhudia tena historia na sifa ya nchi yetu ya kubadilishana madaraka na nafasiza uongozi kwa hali ya amani na utilivu.
Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba tumeshuhudia maendeleo makubwa ya kiuchumi yakiwemo kukamilika kwa miradi mingi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu, skuli za ghorofa, majengo ya Ofisi, makaazi na maduka ya kisasa pamoja na miradi ya usambazaji wa maji safi na salama.
Kati ya miradi hiyo,imo miradi ya jengo la Abiria la Terminal IIIkatika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, wa Abeid Amani Karume, Maduka ya Michenzani (Michenzani Shopping Mall) na barabara mbali mbali za Unguja na Pemba zilizojengwa kwa kiwango cha lami.
Mwaka 2020, vile vile, utakumbukwa kwa kuwa ni mwaka ambao Zanzibar imekamilisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020 na kufikia lengo la kiwango cha nchi zenye kipato cha kati(Low Middle Income Status) kwa kuzingatia vigezo vya kiuchumi vilivyowekwa na Jumuiya za Kimataifa.
Ndugu Wananchi,
Tunaukamilisha mwaka 2020 ikiwa tumeshatumia miezi miwili
ya mwanzo ya Uongozi wa Serikali, katika
kipindi hiki tumeunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984 inavyoelekeza na viongozi wa kushika nyadhifa mbali mbali
wameshateuliwa. Moja kati ya malengo ya kuwekwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa ni kuimarisha umoja na mshikamano
miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Nasaha zangu hivi sasa ni kwamba sote tuuanze mwaka mpya 2021 kufanyakazi kwa ari mpya na kuiunga mkono Serikali kwa yale mambo yaliyopangwa kutekelezwa. Mapinduzi makubwa ya kiuchumi tuliyodhamiria kuyafanya katika uchumi wa buluu, ujenzi wa miundombinu, uwekezaji, utalii, biashara, ujenzi wa viwanda, kilimo, uvuvi, ufugaji, elimu, afya, usambazaji wa maji safi na salama na uwezeshaji wa wananchi tutayafikia ikiwa kila mmoja atafanya kazi kwa bidii na kutekeleza wajibu wake.
Tuunge mkono juhudi za Serikali katika kupambana na rushwa, wizi, ubadhirufu wa mali ya umma na uzembe katika sehemu zetu za kazi. Tuiunge mkono Serikali katika utekelezaji wa mipango ya kukomesha udhalilishaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia.
Mwaka 2021 uwe ni mwaka wa kuwa na mipango imara ya usafi wa miji yetu na uhifadhi wa mazingira. Kwa pamoja, tuhimizane matumizi bora ya ardhi na tushirikiane katika kuitatua migogoro ya ardhi iliyopo na itakayojitokeza.
Ndugu Wananchi,
Ikiwa ni sehemu ya Shamra shamra za Sherehe za
maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya
Zanzibar, kesho tarehe 01 Januari, 2021 tutafanya Bonanza la Mazoezi ya viungo.
Tutaanza na matembezi yatakayoishia katika Viwanja vya Amani kwa
hapa mjini Unguja. Nawaalika wananchi
mushiriki katika matembezi hayo, na wale watakaokosa nafasi ya kushiriki
wafanye mazoezi katika Mikoa na Wilaya
zao. Sote tushiriki katika shamra shamra za Sherehe za Mapinduzi kwa namna mbali mbali ili kuzienzi
na kuziendeleza fikra na mawazo ya
waasisi wa Mapinduzi na Viongozi mbali mbali walioiongoza nchi yetu katika
kipindi hiki cha miaka 57.
Ndugu Wananchi,
Nafahamu kwamba usiku wa kumkia mwaka mpya huwa ni usiku
wa furaha. Nawasihi wananchi tufurahie kuingia
kwa mwaka mpya tukizingatia Sheria na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa
amani.
Namalizia risala yangu kwa kutoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa Tanzania. Kadhalika, natoa salamu kwa viongozi wa nchi marafiki, Taasisi za kimataifa na washirika wetu mbali mbali wa maendeleo. Tunamuomba Mola wetu aujaalie kheri na baraka nyingi mwaka mpya wa 2021. Tunamuomba atuzidishie neema na baraka na adumishe umoja na mshikamano uliopo.
Mungu Ibariki Tanzania
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment