Habari za Punde

Maandalizi ya Tamasha la Saba la Biashara Zanzibar Katika Viwanja vya Maisara.

Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya viwanda Mudrik Ramadhan Suraga akikagua maeneo mbalimbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya tamasha la saba la biashara  linalotarajiwa kuanza januari 04,2021 huko Viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar.
Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya viwanda Mudrik Ramadhan Suraga akikagua maeneo mbalimbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya tamasha la saba la biashara  linalotarajiwa kuanza januari 04,2021 huko Viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Idara ya Biashara na Masoko Khamis Ahmada Shauri akimpatia maelekezo  Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya viwanda Mudrik Ramadhan Suraga kuhusu maandalizi ya Tamasha la saba la biashara linatarajiwa kuanza januari 04,2021 huko Viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar.
 

Na Ramadhani Ali – Maelezo            31.12.2020

Tamasha la saba la Biashara la Zanzibar linatarajiwa kuanza tarehe 4 na kumalizika tarehe 15 Januari 2021 katika Viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar.


Akizungumza na Waandishi wa Habari katika viwanja vya Maisra baada ya  kukagua maandalizi ya Maonyesho hayo, Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Mudrik Ramadhani Soraga amesema kuwa zaidi ya wafanyabiashara na wajasiriamali 340 wa ndani na nje ya nchi wamethibitisha kushiriki Tamasha hilo.


Alisema madhumuni makubwa ya Tamasha la Biashara la Zanzibar ni kutoa nafasi kwa wajasiriamali na Wafanyabiashara kutangaza bidhaa na huduma zao ndani na nje ya nchi ili kupata masoko ya uhakika ya bidhaa zao.


Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda alibainisha kuwa Tamasha ni njia moja ya kukutana na wanunuzi wa bidhaa ama huduma wanazotoa ana kwa ana, kwani ukuaji wa sekta ya biashara ndio chanzo cha kuongeza ajira na kunyanyua pato la wananchi  na Taifa kwa jumla.


Alieleza kuwa Tamasha la Biashara litaweka jukwaa kwa ajili ya kutangaza Uchumi wa Bluu pamoja na kuwa na siku ya maalum ya ubunifu yenye lengo la kuibua vipaji vya wajasiriamali.

Akitaja mafanikio ya yaliyopatikana katika Tamasha la sita, Kaimu Waziri alisema jumla ya wafanyabiashara na wajasiriamali 398 kutoka ndani na je ya Zanzibar walishiriki na inakisiwa kulikuwa na mauzo ya zaidi ya shilingi milioni 954.7 yalifanyika katika kipindi hicho


Waziri Soraga alisema Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan atalifungua rasmi Tamasha la saba la Biashara la Zanzibar tarehe 6 Januari 2021katika viwanja vya Maisara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.