Habari za Punde

Wizara ya Elimu kutoa mwongozo matumizi ya vazi la Joho kwa maskuli

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said katikati, akiwa na Mwalimu Mkuu wa Skuli ya FEZA Mr Ali Nunghu, wakicheza mziki na Wanafunzi wa Skuli hiyo wakati wa Sherehe za Mahafali ya Skuli hiyo.
Wanafunzi wa Skuli ya Feza wakiwa katika mahafali ya  skuli yao
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said akisalimiana na Wanafunzi wa Skuli hiyo wakati alipofika katika sherehe zamahafali ya Skuli ya FEZA.


 Wanafunzi wa Skuli ya FEZA wakionesha vipaji vyao vya Sanaa na sayansi katika sherehe ya mahafali yao iliyofanyika katika ukumbi wa Skuli hiyo, kisauni mjini Unguja.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Skuli ya Feza alipojiunga nao kwenye Mahafali ya skuli hiyo


Picha na Maulid Yussuf, Wema


Na maulid Yussuf, WEMA

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema Wizara yake itatoa muongozo maalum juu ya matumizi ya Vazi la joho katika skuli wakati wa mahafali, ili kuliwekea heshima na hadhi yake kama lilivyo awali.
Amesema vazi hilo limekuwa likivaliwa bila ya utaratibu hali inayoweza kupelekea kumfanya mtoto kutokuwa na ari ya kuendelea kusoma.
Akizungumza katika mahafali ya Skuli ya FEZA huko Kisauni Mjini Unguja amesema utaratibu wa kuvaa joho unajuilikana kuvaliwa mpaka Mwanafunzi afike Chuo kikuu na sio kumaliza Mandalizi, Msingi au Sekondari.
Aidha Mhe Simai amewataka wazazi na walezi kushirikiana na Walimu katika kuwalea watoto wao pamoja na kuwafuatilia kwa karibu zaidi mienendo yao ili waweze kuwa watoto wema na viongozi wazuri wa baadae.
Amesema kutokana na kuwa elimu ni muhimu katika maisha ya mwanaadamu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuilipia elimu kwa kutoa huduma hiyo kwa wote kuanzia ngazi ya Maandalizi Msingi hadi Sekondari ya lazima ili kila mtoto aweze kupata haki hiyo ya msingi bure.
Amesema pia Serikali imetoa fursa katika Skuli binafsi, ambapo amesema Wizara itaendelea kuziunga mkono Skuli hizo na kuziwekea miongozo na utaratibu mzuri kwa lengo la kutoa Elimu bora kwa watoto.
Aidha Mhe Simai amefahamisha kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ina lengo la kuanzisha mashindano ya midahalo katika Skuli kwa kutoa mada mbalimbali kwa lengo la kuongeza uelewa kwa Wanafunzi katika masuala mbalimbali pamoja na kuweka ushindani wa kimasomo kati ya Skuli moja na Skuli nyengine.
Mhe Simai amewashauri Walimu kuwafanyia wanafunzi ziara za kimasomo hasa katika sehemu mbalimbali za kihistoria ili waweze kujifunza zaidi kwa vitendo badala ya kuishia darasani pekee.
Hata hivyo Mhe Simai ameutaka uongozi wa Skuli ya FEZA kufikiria juu ya suala la kusomesha lugha ya kituruki kwa wanafunzi wao na umuhimu wake kwani hio ni kuwaongezea mzigo wa masomo watoto.
Katika hatua nyengine, mhe Simai ametoa angalizo kwa wazazi juu ya kutowapa vyombo vya moto watoto wao wanapokwenda Skuli hasa vya maringi mawili kwani vinahatarisha Usalama wao wanapoingia barabarani.
Katika mahafali hiyo, Mhe Simai amewapongeza Wanafunzi waliomaliza masomo yao na kuwataka kuendelea kuzidisha bidii zaidi katika masomo yao katika ngazi zinazofuata ili waweze kufanikiwa katika maisha yao.
Nae Mwalimu mkuu wa Skuli ya FEZA Zanzibar Mr Ali Nunghu Amesema ushirikiano kati ya Skuli hiyo na Wizara ya Elimu Zanzibar, ulianza tokea mwaka 2005, ambao umeweza kuwapa mafanikio mazuri na kufanikiwa kuwa miongoni mwa Skuli bora Tanzania katika kufaulisha Wanafunzi.
Pia amewashukuru wazazi kwa kufuata muogozo wa Skuli yao na kufanikiwa kufikia malengo waliyoyakusudia.
Aidha Mr Nunghu amewapongeza Wanafunzi waliohitimu masomo yao hasa wa Elimu ya msingi, na kuwataka kuogeza bidii zaidi ya masomo ili waweze kufaulu vizuri hapo baadae.
Akisoma risala kwa niaba ya Wahitimu Mwanafuzi Ulfat Said amewashukuru Walimu wao wote kwa juhudi walizozichukua kuwasomesha na kuweza kumaliza Elimu yao ya awali ambapo amewanasihi wanafunzi wenzao kuendelea kujisomea kwa bidii pamoja na kudumisha nidhamu ili waweze kufanikiwa katika masomo yao.
Jumla ya Wanafunzi 114 wamehitimu masomo yao kati ya hao Wanafunzi 69 ni wa kidatu cha NNE na Wanafunzi 45 ni wa darasa la sita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.