Habari za Punde

Makatibu Wakuu Watakiwa Kusimamia Fedha za Serikali na Kupambana na Uzembe na Ufisadi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati akizungumza na Makatibu Wakuu na Manaibu baada ya kuwaapisha katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo.25/1/2021.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyiamewata Makatibu Wakuu wapya kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuzisimamia fedha za serikali na kupambana na uzembe na ufisadi.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar mara baada ya kuwaapisha viongozi mbali mbali aliowateua hivi karibuni wakiwemo Makatibu Wakuu.

Amesema kuwa ameamua kupunguza idadi ya Manaibu Makatibu Wakuu kwa lengo la kupunguza ukumbwa wa Serikali pamoja na kupunguza matumizi ya Serikali.

Alisema kuwa Makatibu Wakuu ndio Maafisa Masuuli ambao ndio wasimamizi wa fedha za Serikali ambapo aliwataka fedha za mahuduli za Serikali zinapatikana kwani bado kuna taasisizinakusanya kwa njia ya risiti za mkono na kutaka fedha kukusanywa kwa mtandao.

Aliwataka kuondoa matumizi yasiyokuwa na tija kama vile semina na makongamano pamoja na kuwataka kuondoa aina zote za ubadhilifu, matumizi nje ya bajeti kwani mifumo ya bajeti ya fedha za serikali zimekuwa zikichezewa sana.

Alisema kuwa hali hiyo imepelekea wahasibu kadhaa kuuchezea mfumo huo na kuchukua fedha nyingi na kusema kuwa tayari ameshatoa agizo kwa wahasibu wote waliotuhumiwa kufanya mchezo huo kusimamishwa kazi kati ya wahasibu zaidi ya  80 ambao bado walikuwa Serikalini.

Aliutaka uongozi wa Wizara ya Fedha kurekebisha mfumo huo mara moja huku akiwataka Makatibu Wakuu hao kuyafanyia kazi mambo hayo.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi aliwatakaMakatibu Wakuu hao  kuondoa uzembe, uvivu, utoro na kuwataka kuchukua hatua kwa wale wasiowajibika mara moja kwani wao ndio wenye dhamana.

Alisema kuwa Makatibu Wakuu hao ndio wenye Mamlaka na dhamana ya wafanyakazi hivyo aliwataka kuhakikisha wafanyakazi wanaokwamisha kazi kutokana na urasimu wao wanafanyiwa kazi.

Rais Dk. Mwinyi aliwataka Makatibu Wakuu hao kuhakikisha nidhamu inajengwa katika maeneo yao ya kazi  huku akiwataka kuhakikisha suala la haki za wafanyakazi linapewa kipaumbele zikiwemo posho zao, muda wa ziada wa kazi pamoja na fedha za likizo.

Aliwataka kuhakikisha safari za kikazi zinakuwa zenye tija na zisiwe na upendeleo kwani taasisi nyingi zipo ambazo wanakwenda wao kwa wao sambamba na nafasi za masomo ambazo wamekuwa wakienda hao kwa hao na kuwataka kutofanya hivyo kwani hali hiyo inaondoa utendaji na morari ya kazi.

Alieleza kuwa ipo haja ya kusimamia vizuri kamati za manunuzi na kuwataka kila kinachonunuliwa kiwe na thamani ya fedha zinatolewa huku  akitolea mfano wa pampu zilizonunuliwa na Mamlaka ya ZAWA ambazo zimefanya kazi kwa muda wa kati ya miaka miwili na mwaka mmoja wakati zipo ambazo zinakaa zaidi ya miaka kumi.

Aliwataka kuchukua hatua na kutomsubiri yeye na kusema kwamba iwapo watashindwa wao kuchukua hatua yeye atachukua lakini akiwamaliza atawachukulia hatua na wale viongozi wa Mawizarani.

Alitoa mfano wa taa zilizowekwa na mradi wa ZUWSP awamu ya kwanza barabarani, mradi wa MRI katika Hospitali ya Mnazi Mmmoja , vifaa vya kupimia mizigo uwanja wa ndege kati ya 12, tisa mbovu, 

Alisema kuwa hatua zinapochukuliwa hazichukuliwi kwa sababu anachukiwa mtu kwa sababu anaonewa mtu kwa sababu wakati serikali inajenga na kutoa fedha wengine wanabomoa hivyo ni vyema wakati kunajengwa wengine wasiwepo.

Rais Dk. Mwinyi alitolea mifano miradi michache ikiwemo ile ya maji ambayo haikufanywa vizuri na badala yake jukumu linawaangukia Wabunge na Wawakilishi hivyo, alitaka hayo yasifichwe yasemwe na wale waliotuhumiwa wasimamishwe kazi na hawafukuzwi kwani baada ya uchunguzi ikithibitika hawajahusika watarejeshwa kazini na iwapo wakithibitika hatua zitachukuliwa.

Alisema kuwa manunuzi ni eneo ambalo ni lazima lifanyiwe kazi na kuwataka Makatibu hao Wakuu kuchukua hatua za haraka na kufuata taratibu za tenda.

Sambamba na hayo, aliwataka kila Mamlaka iliyokuwa chini ya Wizara yake ni jukumu lao kuzifanyia kazi na kuchukua hatua na kuhakikisha kuna utendaji mzuri katika Mamlaka zao na hakuna rushwa, hakuna wizi wa fedha za umma hususan katika manunuzi.

Alisema kuwa mikataba yote ni lazima iwe na maslahi kwa umma na kuwataka mikataba yote ipite kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwemo ile inayohusu mikopo ambapo ni lazima ipate  kibali cha Waziri wa Fedha na kuwataka kusimamia hali hiyo.

Rais Dk. Mwinyi aliwataka kusimamia miradi yote ya uchafu ukiwemo mradi wa ZUSP ambao mradi huo haukusaidia na mpaka leo mji bado haujawa msafi.

Akieleza kuhusu taarifa za Mkaguzi wa ndani na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliwataka Makatibu Wakuu kufanya kazi na Wakaguzi wa ndani na kutafuta wakaguzi watakao wasaidia hukuwakihakikisha kasoro zote zinafanyiwa kazi.

Pamoja na hayo, alisema kuwa kumekuwa na mtindo wa kuchukuliwa fedha za fidia ambazo zimekuwa zikichukuliwa na wahusika wa kulipwa fidia wamekuwa hawazipati wakiwemo wale wanaobomolewa nyumba zao kupitisha miradi ya barabara.

Aliwataka Makatibu Wakuu hao kufanya uhakiki wa fedha za Pencheni za wazee, fedha za TASAF, fedha za ruzuku za kilimo, fedha za uwezeshaji wananchi kiuchumi na nyenginezo na kuwataka kuhakikisha hayo ni majukumu yao na wanayafuatilia vyema.

Sambamba na hayo, aliwataka kutokuwa vikwazo kwa miradi ya uwekezaji huku akiitaka ZIPA kuwa ni kituo kinachukusanya wahusika wakuu wote wa uwekezaji na kutowabughudhi wawekezaji.

Alisisitiza haja kwa kila Wizara kuandaa miradi ya maendeleo na iwepo bajeti yake hivyo wote wawe tayari kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maendeleo huku akiwaahidi kwamba atazitembelea Wizara zote.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwataka kila Katibu Mkuu kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na kufuatilia ahadi zote zilizotolewa kwa wananchi.

Kwa upande wa Katibu Mkuu Kiongozi, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kumekuwa na utamaduni wa kuzorota kwa kazi zile zinazopangwa kwa Wizara zaidi ya moja kwa kawaida kazi zinakuwa haziendi hivyo alimtaka Katibu Mkuu Kiongozi kutekeleza majukumu hayo ipasavyo.

Nao Makatibu Wakuu hao walioapishwa hivi leo waliahidi kwenda mwendo kasi wa Rais Dk. Mwinyi na kueleza kuwa wako tayari kutekeleza majukumu yao na kubwa wanaloliomba ni mashirikiano kati yao na watendaji wengine katika sehemu zao za kazi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.