Habari za Punde

Waumini wa Kiislam Wajumuika na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Katika Sala ya Ijumaa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akitoa salamu kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kukamilika ka Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Amani.

Mwanachuoni Maarufu Ustadhi Rajab Mohamed Shaal akiongoza dua mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Amani Mjini Zanzibar.

Imamu wa Msikiti wa Ijumaa wa Aman Sheikh Ismail Mohamed katu kati akimtakia safari njema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman wa kwanza kushoto baada ya kukamilika kwa Ibara ya Sala ya Ijumaa.

Wa kwanza kulia ni Mtoa Hutba ya Ijumaa Mwachuoni Ustadh Rajab Mohaed Shaali.

Picha na – OMPR – ZNZ.

 Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema mshikamano wa pamoja kati ya Viongozi, Waumini wa Dini pamoja na Wananchi mahali popote walipo ndio njia ya msingi itakayorahisisha kulijenga Taifa imara.

Akitoa salamu mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ijumaa pembezoni mwa Uwanja wa Michezo wa Aman Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwakumbusha Waumini hao kwamba kila Mwananchi ana nafasi yake katika kujenga Nchi si lazima ame Mtumishi wa Umma.

Mheshimiwa Hemed alisema hatua hiyo ya mshikamano wa pamoja ambayo Serikali Kuu tayari imeshaonyesha muelekeo wa mfano katika ngazi ya Uongozi itawezekana na kufanikiwa ipasavyo endapo jamii nzima itaendelea kuhamasishana katika usimamizi wa masuala ya Amani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba yapo Mataifa Duniani baadhi ya Waumini wake wenye Imani ya Uislamu wameshindwa kutekeleza Ibada ya sala ya Ijumaa kutokana na machafuko yaliyosababishwa na Itikadi za Kisiasa au Kidini.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alihimiza umuhimu wa Waumini na Wananchi kuendelea kuzingatia Uadilifu katika matendo yao kama ulivyosisitizwa katika Hotuba ya Ijumaa ili kuleta utulivu wa moyo ndani ya vifua vya Watu katika maeneo yao.

Alieleza kwamba changamoto za Kijamii kwa asilimia kubwa zinaweza kuondoka au kupungua kabisa kama ulafi wa baadhi ya Watu hasa katika masuala ya Fedha utadhibitiwa jambo ambalo hivi sasa Serikali Kuu imekuwa ikiendelea kuchukuwa hatua za kukabiliana nalo.

Aliwahimiza Wananchi pamoja na Waumini wa Dini kuvumilia kipindi hichi ambacho Uongozi wa Serikali umekuwa ukichukuwa hatua hizo zinazoonyesha mwanga kwa baadhi ya Washirika wa Maendeleo ndani na Nje ya Nchi kwa kutaka kuungwa mkono jitihada hizo za Serikali.

Mapema akitoa Hotuba ya sala ya Ijumaa Mwanachuoni Maarufu Ustaadh Rajab Mohamed Shaali aliwakumbusha Waumini wa Dini ya Kiislamu kuhakikisha kwamba suala la uadilifu linapewa nafasi yake ili Jamii Mitaani iendelee kuishi kwa upendo.

Ustaadhi Rajab alisema Utamaduni wa baadhi ya Watu kupenda kujilimbikizia Mali za dhulma sio malengo ya uwepo  wao Duniani katika kufanya ibada bali unazidisha chuki na uhasama miongoni mwa Jamii  katika ngazi ya ufukara, umasikini na utajiri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.