Habari za Punde

Buriani Dkt.Mohammed Seif Khatib

Mwanasiasa nguli wa siku nyingi Dk. Muhammed Seif Khatib amefariki Dunia, leo asubuhi katika Hospitali ya Ar Rahma Unguja mjini Zanzibar. Emmanuel Mohamed mtoto wa Khatib, amethibitisha.

Amesema, msiba upo nyumbani kwa marehemu eneo la Magomeni Zanzibar na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho saa nne asubuhi na kuzikwa kijiji kwao Umbuji Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.


Wakati wa uhai wake Khatibu aliyezaliwa Januari 10, 1951,  amewahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali katika Chama Cha Mapinduzi na Serikalini, ikiwemo kuwa  Mbunge wa Jimbo la Uzini  Zanzibar kwa tiketi ya CCM mwaka 1995 na pia amewahi kuwa Waziri katika wizara mbalimbali.


Khatibu atakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa waasisi wa kwanza wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambapo  kati ya mwaka 1978 hadi 1983 alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM  na kati ya mwaka  1978 na 2002 Khatibu alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Pia amewahi kuwa Katibu wa NEC, Oganaizesheni Makao Makuu ya CCM.


Kabla ya kuwa mjumbe wa NEC alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu  anayeshughulikia masuala ya Habari, na baadaye January 4, 2006  aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo   na  February 12, 2008 akateuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.