Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi Ameongoza Mamia wa Wananchi wa Zanzibar Katika Kisomo cha Hitma Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad Viwanja vya Maisara Suleiman Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi ameongoza Wananchi wa Zanzibar katika kisomo cha Hitma na Dua ya kumuombea aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, kilichofanyika leo 20-2-2021 katika viwanja vya Maisara Suleiman Wilaya ya Mjini Unguja na (kulia kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi na (kushoto kwa Rais) Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali. 
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyileo amewaongozawananchi katikakisomo cha dua ya Hitma ya kumuombea Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Hitma hiyo ilifanyika katika viwanja vya Maisara Jijini Zanzibar ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa,dini na serikali,  pamoja na mamia ya wananchi ambapo pia, viongozi wanawake wa kitaifa nao walihudhuria wakiongozwa na Mama Mariam Mwinyi.

Kisomo hicho kiliongozwa na Sheikh Abubakar Al-Khashim na baada ya hapo mawaidha yalitolewa pamoja na Qaswida zinazohusiana na tukio hilo, salamu za shukurani pamoja na dua iliyosomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih.

Akitoa mawaidha katika kisomo hicho Sheikh Suwed Ali Suwed ambaye pia, ni Mjumbe wa Baraza la Ulamaa, alisema kuwa kila mwanaadamu ataonja umauti na duniani ni mahala pa kupita na yule ambaye atanusurika na adhabu ya moto huyo ndie aliyefanikiwa.

Sheikh Suwed alisema kuwa msiba kwa waumini wa dini ya Kiislamu unatakiwa uwe kwa siku tatu na baada ya hapo kuna haja ya kurejesha sunna za kawaida na hakuna haja ya vilio zaidi ya siku tatu huku akisisitiza haja ya kumtakia msamaha Marehemu.

Aliongeza kwamba kwa hadithi ya Mtume Muhammad (S.A.W) hakuna Muislamu yeyote atakaye muombea dua mwenziwe aliyetangulia mbele ya haki bali dua hiyo inakubalika, ambapo alitumia fursa hiyo kumuomba Mwenyezi Mungu (S.W) kuikubali dua hiyo na kumsamehe Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad makosa yake.

Akitoa salamu za shukurani kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe.Haroun Ali Suleiman alitoa shukurani kwa wale wote waliofanikisha shughuli hiyo ya kisomo cha Hitma huku akisisitiza kwamba zawadi nzuri aliyoiacha Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ni kuendeleza umoja na mshikamano uliopo.

Kazi iliyopo ni kuuendeleza na kuimarisha umoja, amani na mshikamano uliopo sambamba na kumuombea dua Rais na viongozi wote wa Serikali, vyama vya siasa pamoja na wananchi kwa kushirikiana kikamilifu katika shughuli hizo.

Waziri Haroun aliomba mashirikiano hayo yaliyooneshwa katika kipindi hichi cha msiba yaimarike zaidi kwa lengo la kuendeleza mashirikiano, amani na umoja uliopo kwa azma ya kuiletea nchi maendeleo.

Nae Mwakilishi wa Chama cha ACT Wazalendo Mhe. Juma Duni Haji akitoa neno la shukurani kwa niaba ya chama hicho alitoa shukurani kwa Serikali na uongozi wa Maulamaa kwa hitma hiyo pamoja na ile iliyofanyika kisiwani Pemba ambazo zimefanyika kwa mashirikiano makubwa.

Alisema kuwa katika kipindi chote hicho cha msiba watu wote walikuwa ni wamoja bila kujali itikadi zao za kisiasa kwani huo ni wema kwa Marehemu na kumuomba Mwenyezi Mungu kwamba dua zote hizo zilizosomwa zimfike huku akitoa shukurani kwa wale wote waliofanikisha shughuli hizo.

Mhe.Juma Duni kwa niaba ya chama chake hicho cha ACT Wazalendo alisisitiza kuwa chama chao kinaomba mashirikiano hayo yaendelelee kwa msiba na mambo mengine yote.

Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad alifariki dunia mnamo Februari 17, 2021 huko katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar-es-Salaam na kuzikwa kijijini kwao Mtambwe Nyali, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba siku ya Alkhamis ya Februari 18, 2021.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.