Habari za Punde

Wajumbe wa BLW Wapatiwa Semina Kufahamu Kazi za ZURA.

Mwashungi Tahir   Maelezo   13/2/2021.

WAZIRI wa Maji na Nishati  Mhe.Suleiman Masoud Makame amewataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kujua uwepo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati  Zanzibar ZURA pamoja na kujua utendaji wake wa kazi.

Akizungumza na wajumbe hao huko katika Ukumbi wa ZURA uliopo Maisara wakati alipokuwa akifungua semina maalum kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar  na kuwataka kujua kazi zinazofanywa ya Mamlaka hiyo.

Amesema kuelewa kazi za Mamlaka ya udhibiti wa Huduma za  Nishati  na Maji kutaweza kuwaelimisha kwa kujua majukumu yote yanayofanywa pamoja na kujenga ushirikiano katika utendaji wao wa kazi kwa wote.

Hivyo amesema Lengo la mafunzo hayo ni kuwa  pamoja  kuwepo  na ukaribu mashirikiano kwa kufahamu kazi zote zinazofanywa na mamlaka hiyo ambayo ndio mdomo mkuu kwa wananchi katika shughuli zote ikiwemo huduma za mafuta na  gesi, nishati ya umeme pamoja na maji safi na salama.

“Lengo la mafunzo hayo ni kuzitambua kuzielewa na kuzijuwa kazi zote zinazofanywa ili kuwepo na ukaribu Mamlaka hiyo”, alisema Waziri huyo.

Akiwasilisha mada ya hali halisi ya udhibiti ya mamlaka hiyo ZURA  Mkurugenzi Mkuu Bi Hindi Nassor Khatib amesema mamlaka imeanzishwa chini ya kifungu namba 3 cha Sheria no 7/2013 ya kuanzisha mamlaka ya udhibiti wa huduma za Maji na Nishati Zanzibar.

Amesema pamoja na kifungu hicho shughuli kuu za mamlaka hiyo ni pamoja na kudhuibiti sekta za Maji na Nishati kiufundi na kiuchumi ambapo mwaka huo Baraza la wawakilishi lilipitisha sheria ya kuanzisha chombo chenye jukumu la kudhibiti na kusimamia watoa huduma katika sekta za maji,umeme,mafuta na gesi.

Wakitoa michango yao wajumbe hao wamelalamikia ZURA kwa ukosefu wa kupatikana huduma ya maji safi na salama pamoja na umeme wa uhakika na kuwataka wawe na utaratibu wa kuvisafisha visima ili huduma hiyo uipatikane kwa kuridhisha jamii.

Pia wameiomba mamlaka hiyo kuweka bei za gesi kuwa pamoja kwani kila mfanyabiasara anaweka bei yake na kukuta wananchi wengine wanashindwa kutumia huduma hiyo.

Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Zubeir Ali Maulid akifunga mafunzo hayo amesema wameweza kujifunza kazi za mamlaka hiyo na kuwahakikishia ZURA watashirikiana katika kutatua changamoto zilizojitokeza ili wananchi wafaidike na huduma hizo.

Mada zilizowasilishwa ni mbili ikiwemo Hali halisi ya udhibiti wa ZURA na Dhana za misingi na udhibiti ambapo mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati Zanzibar ZURA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.