Habari za Punde

Ili nchi iweze kupata maendeleo, kila mwananchi anastahiki kulipa kodi- Wito

 Na Mwashungi Tahir       Maelezo            08/03/2021.

Waziri wa Ardhi  na Maendeleo  ya Makaazi Riziki Pembe  Juma amesema dhamira ya Serikali katika awamu ya nane ni kila mwananchi anastahiki kulipa kodi ili nchi iweze kupata maendeleo na kuweza kukuza uchumi.

Akizungumza na wakaazi wa Saateni katika Mkutano kuhusu ustawi wa nyumba za Saateni Mjini Unguja wakati alipokuwa akisikiliza changamoto za wakaazi hao na kuahidi kuzifanyia kazi ili kuepukana  nazo.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawajali wananchi wake kwa kuwaona wanaishi  kwa amani na utulivu katika mazingira yaliyo bora na kuwataka walipie kodi ya nyumba hizo ili kuepusha usumbufu ikiwa ni amri ya Rais kuweka kipaumbele kulipa kodi.

Aidha amewataka wafanyakazi wa shirika la nyumba kuwa na lugha nzuri ya kuwajibu  wakati wananchi wanapokuja kutoa malalamiko yao na kuweza kuwapatia ufumbuzi  ili kero zao ziweze kumalizika.

"Nawaomba wafanyakazi kuwa na lugha nzuri kwa wakaazi wanaoishi katika nyumba   wanapokuja kuipa kodi ili wapate hamasa zaidi kwani mteja ni mfalme", alisema Waziri huyo.

Pia amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote zinazowastahiki ikiwemo Hospital, makaazi yaliyo bora, maji safi na salama ,  skuli zilizo na ubora  na mambo mengine yote yanayohitajika kwa jamii bila ya pingamizi yeyote.

Waziri Riziki amewaomba wakaazi hao kwa kila aliyelimbikiza madeni afike kwenye shirika pamoja na risiti zake na kuelekezwa jinsi ya kupunguza madeni hayo ili waweze kulipa kwa awamu.

Hivyo amesema Serikali kwa sasa haina mpango wa kupunguza kodi  kwani kutolipa kodi ni moja ya kuhujumu uchumi na maendeleo hayatoweza kupatikana .

Nao wakaazi hao wameiomba Serikali iwapunguzie kodi ambayo iko juu ili waweze kulipa kwani wakaazi wengi wanaoishi katika nyumba hizo  hali zao ni duni na wanajikuta wanashindwa kulipa kwa wakati na madeni yanajilimbikiza.

Vile vile wameiomba Serikali kuwafanyia marekebisho nyumba hizo kama ilivyokuwa zamani  sehemu za mapaa ambayo mabati yaliyoezekewa ni ya zamani na yanaleta athari kwa afya zao, kuwapatia huduma ya maji safi na salama .

Kwa  upande wake sheha wa shehiya hiyo ya Saateni Hussein Hamza Nyange amesema wananchi wake wamefurahishwa sana kuja Waziri huyo kusikiliza kero zao na kuwaahidi watazitafanyiwa kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.