Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi amuapisha Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar

 

                                  

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemuapisha Othman Masoud Othman Sharif kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kufuatia uteuzi alioufanya hapo jana Machi 01, 2021.

Uteuzi wa Othman Masoud Othman unafuatia kifo cha aliekuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, aliefariki dunia Februari 17, mwaka huu.

Hafla hiyo ya kiapo imefanyika Ikulu Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab na  Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid.

Wengine ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa,Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Juma Abdalla Sadalla, Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zubeir Zito Kabwe, Mawaziri, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa vyama vya Siasa, Viongozi wa madhehebu mbali mbali ya Dini  pamoja na wanafamilia.

Rais Dk. Mwinyi amemuapisha kiongozi huyo kushika wadhifa huo  kutokana na matakwa ya Kikatiba chini ya kifungu cha 9(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kilichobainisha kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimteua kiongozi huyo kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu namba 39(3) cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 baada ya kushauriana na Chama cha ACT Wazalendo.

Kabla ya uteuzi huo Othman Masoud Othman aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali za juu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikiwemo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Katika hatua nyengine, akizungumza na vyombo vya habari, Makamo wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman alisema atatumia uzoefu mkubwa alionao kumsaidia Rais wa Zanzibar kujenga na kuendeleza misingi ya maridhiano ya umoja wa kitaifa kwa maslahi mapana ya Wazanzibar.

Alisema atasaidia kuimarisha misingi ya sera katika nyanja mbali mbali ikiwemo kutengeneza sera bora ili kuleta maendeleo ya kiuchumi pamoja na kusimamia ustawi mwema wa wananchi.

Aidha, alisema atasaidia kujenga Serikali itakayoweza kusimamia maridhiano ya nchi ili kuendeleza amani na umoja uliopo, akibainisha kuwa yeye ni muumini wa kushajiisha umoja miongoni mwa Wazanzibari.

Vile vile alisema atatumia uzoefu mkubwa alionao Kimataifa katika kusimamia misingi ya rasilimali za Serikali, uwekezaji pamoja na uwajibikaji katika taasisi za umma. 

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.