Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amempongeza Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kutoa salamu wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango katika viwanja vya Ikulu Chamwino Dodoma leo 31-3-2021.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameshuhudia kuapishwa kwa Dk. Philip Isdor Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hafla iliyofanyika leo Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma alimuapisha Dk. Philip Isdor Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kiapo ambacho kilisimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Bashiru Ali Kakurwa.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa, Serikali, viongozi wa dini, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wastaafu walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, Mama Mariam Mwinyi pamoja na Mama Mpango.

Mara baada ya kiapo hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano alipata fursa ya kuzungumza na Watanzania ambapo katika mazungumzo yake alisema kuwa hakuona mtu mwingine aliyempata mwenye sifa kama za Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na ndio sababu za kumteua kushika wadhifa huo.

Rais Samia alimpongeza Dk. Mpango kwa kushika wadhifa huo na kukipongeza chama chake cha CCM kwa kuridhia jina la Dk. Mpango huku akilipongeza Bunge kwa kumkubali Makamu huyo wa Rais.

Alisema kwamba Dk. Mpango ni mcha Mungu, muadilifu, hodari, mchapa kazi na ana matumaini nae makubwa kwamba atakwenda kumsaidia katika kuimarisha uchumi sambamba na matumizi ya fedha za Serikali.

Rais Samia alieleza kwamba kwa upande wa kutatua changamoto za Muungano tayari kazi kubwa imefanyika na kumpa kazi Dk. Mpango iliyobaki ya kuhakikisha shughuli za kifedha zinakaa sawa kwani wakati akiwa Waziri wa Fedha na Mipango shuguli hizo hazikufanyika vyema.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alitoa pongezi za dhati kwa Dk. Mpango kwa kupata wadhifa huo huku akieleza jinsi anavyomfahamu kiongozi huyo kuwa hodari, mweledi, mchapa kazi na muwadilifu.

Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba nafasi aliyoipata anastahili huku akieleza haja katika kufanikisha changamoto za Muungano ambapo tayari nyingi zimeshapata ufumbuzi.

Nae Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango alimuhakikishia Rais Samia wkamba atakuwa msaidizi muadilifu,mtiifu na mzalendo wa kweli kwa nchi yake.

Dk. Mpango alimuahidi Rais Samia kwamba  hatokuwa kama Yuda akimaanisha kwamba hatomsaliti na badala yake atatekeleza kazi zake kwa bidii na kusisitiza kuwa yuko tayari kuchapa kazi ikiwa ni pamoja na kutekeleza Ilani ya CCM, maono ya Rais pamoja na ustawi wa wananchi.

Aidha, Waziri Mpango aliahidi kushirikiana na viongozi wenzake wote wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na mihimili yote ya Dola.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri pamoja na kufanya uteuzi wa wabunge watatu

Akitangaza mabadiliko ya baraza hilo leo Jumatano Machi 31, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, katika hafla ya kumuapisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Rais Samia amesema wabunge aliowateua ni Bashiru Ali Kakurwa, Balozi Liberata Mulamula na Balozi Mbarouk Nasoro Mbarouk

“Kuondoka kwa Dk Mpango kumeacha nafasi ndani ya Wizara ya Fedha na tupo kwenye Bunge la Bajeti ambalo Waziri wa Fedha ni muhimu sana, sasa nikasema nisifanye kazi kidogo kidogo, hii imenifanya nilitazame baraza lote la mawaziri hivyo nimefanya mabadiliko madogo, wanasema zege hailali ni hapa hapa,”

Katika uteuzi wake Rais Samia amemteua Ummy Mwalimu kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI huku Manaibu Waziri wakibaki kuwa walewale, Festo Lugange na David Silinde.

Ofisi ya Utumishi na Utawala Bora, Waziri aliyeteuliwa ni Mohamed Mchengerwa, Naibu Waziri, Deogratias Ndejembi na Mwita Waitara., George Mkuchika anakuwa Waziri ndani ya Ofisi ya Rais Kazi Maalum.

Ofisi ya Makamu wa Rais, Waziri anakuwa Suleiman Jafo, Naibu waziri ni Hamad Chande, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji ambayo imeondolewa kwenye Ofisi ya Rais na kupelekwa chini ya Waziri Mkuu, Waziri akiwa ni Geofrey Mwambe huku Naibu Waziri akiwa ni William Ole Nasha, ambapo Rais ameagiza Wizara hiyo kuundwa haraka ndani ya miezi mitatu iwe imeanza kazi.

Wizara ya Fedha na Mipango, Waziri ni Mwigilu Nchemba na Naibu Waziri ni Hamadi Masauni, Wizara ya Katiba na Sheria, Waziri ni Palamagamba Kabudi na Naibu Waziri ni Jose Mizengo Pinda.

Wizara ya Mambo ya Nje, Waziri ni Balozi Leberata Mulamula na Naibu Waziri ni Mbarouk Nasoro Mbarouk, Wizara ya Biashara na Viawanda, Waziri ni Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Waziri ni Exaudi Kigae.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri aliyepangwa ni Innocent Bashungwa huku Naibu Waziri akiwa ni Pauline Gekul.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri anabaki kuwa Dorothy Gwajima, Naibu Waziri ni Godwin Molel ambapo Mwanaidi Hamis amepelekwa Wizara hiyo kushughulikia masuala ya maendeleo ya jamii na wanawake.

Kwa upande wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Waziri anabaki kuwa Mashimba Ndaki na Naibu Waziri ni Abdalah Ulega, Rais Samia ameeleza kuwa wizara nyingine zinabaki kama zilivyokuwa huku Ofisi ya Makamu wa Rais, Waziri anakuwa Suleiman Jafo, Naibu waziri ni Hamad Chande.

Dk. Mpango aliyezaliwa Jumaapili tarehe 14 Julai 1957, alikuwa ni Mbunge wa Buhigwe Mkoa wa Kigoma ambapo mpaka anapata wadhifa huo alikuwa ni Waziri wa Fedha na Mipango ambapo aliingia Bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2015 baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kisha akateuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango nafasi aliyoitumia mpaka jana Jumaane ya Machi 31.2021.

Katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020 Dk. Mpango alirejea nyumbani kwao Buhigwe na kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo  ambapo alishinda kwa kishindo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.