Habari za Punde

Tume ya Uchaguzi Zanzibar yatoa utaratibu uendeshaji kampeni uchaguzi mdogo jimbo la Pandani na Wadi ya Kinuni

 

TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR

 

TAARIFA YA TUME YA UCHAGUZI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UTARATIBU WA UENDESHAJI WA KAMPENI ZA UCHAGUZI MDOGO WA JIMBO LA PANDANI NA WADI YA KINUNI KATIKA KIPINDI CHA MAOMBOLEZO YA KIFO CHA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 


Ndugu Waandishi wa Habari, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC inaendelea na maandalizi ya  Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Pandani na Wadi ya Kinuni unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Machi 2021, kutokana na aliyekuwa Mwakilishi Mteule wa Jimbo la Pandani na Diwani Mteule wa Wadi ya Kinuni Kufariki Dunia mwezi wa Novemba, 2020. Wakati Tume ikiendelea na maandalizi hayo Usiku wa jana tarehe 17/03/2021  tumepokea taarifa ya kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala pema peponi. (Amiin).

Kutokana na msiba huu, Serikali imetangaza siku 14 za maombolezo ya kitaifa. Kwakuwa kampeni za vyama vya Siasa kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo huo zinaendelea katika maeneo mbali mbali ya Jimbo la Pandani na Wadi ya Kinuni,  Tume ya Uchaguzi kwa Mamlaka iliyonayo inatangaza utaratibu mpya wa kuendesha kampeni katika kipindi hicho cha Maombolezo kama ifuatavyo:-

       i.        Viongozi wa vyama vya siasa na Wagombea ambao wanaendelea na Kampeni zao waache kupiga Muziki, kuimba nyimbo za Kisiasa na wasitishe shamrashamra za sherehe wakati wote wa kipindi cha Maombolezo.

     ii.         Viongozi wa vyama vya siasa na Wagombea wawatake wafuasi wao kabla ya kuanza mikutano ya hadhara kutenga muda angalau wa dakika moja kusimama na kukaa kimya na kumuombea dua Marehemu.

    iii.         Viongozi wa vyama vya siasa na Wagombea wanatakiwa kuacha kufanya kampeni siku ya mazishi.

    iv.         Viongozi wa vyama vya siasa na Wagombea wanasisitizwa kutumia matumizi ya maneno mazuri na lugha inayoendana na wakati huu wa maombolezi.

Ndugu Waandishi wa Habari, Tume ya Uchaguzi inasisitiza kuwa, tarehe ya Uchaguzi Mdogo iko kama ilivyopangwa na inawataka Wagombea wa Uchaguzi Mdogo  kuendelea na kampeni zao huku ikisisistiza kuelewa kua  Taifa lipo katika Kipindi cha maombolezo juu ya Msiba wa Kiongozi Mkuu wa Taifa la Tanzania.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatumia nafasi hii kumuombea Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli apumzike kwa amani na kuwaombea Watanzania  kuwa na subira wakati wote wa Msiba.

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR

MUNGU IBARIKI TANZANIA

Ahsante Sana

 

JAJI MKUU (Mst) HAMID MAHMOUD HAMID

MWENYEKITI

TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR

ZANZIBAR

18 MACHI,2021

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.