Habari za Punde

Waziri Ndugulile Atembelea Vituo vya Tehama kisiwani Pemba

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Faustine Ndugulile (mwenye suti ya kijivu) alipowasili uwanja wa ndege wa Pemba kwa ajili ya kuanza ziara ya kutembelea vituo vya TEHAMA vilivyojengwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kisiwani hapo. Kushoto kwake ni Waziri Kindamba Mtendaji Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Faustine Ndugulile (mwenye suti ya kijivu) akisalimiana na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo pamoja na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kabla ya kuanza ziara ya kutembelea vituo vya TEHAMA kisiwani Pemba. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt.Zainab Chaula 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Faustine Ndugulile (mwenye suti ya kijivu) akizungumza  na watendaji wa Wizara hiyo pamoja na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kabla ya kuanza ziara ya kutembelea vituo vya TEHAMA kisiwani Pemba. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt.Zainab Chaula 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (katikati) akipokea maelezo kutoka kwa mdhamini wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi kisiwani Pemba Ibrahim Juma (kushoto) katika kituo cha TEHAMA cha Micheweni TEHAMA kisiwani Pemba. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt.Zainab Chaula 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Faustine Ndugulile (kwa tatu kushoto) akizungumza katika kituo cha TEHAMA cha Wete kisiwani Pemba. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Bakari, akifuatiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo Dkt. Mzee Mndewa na Kulia ni Waziri Kindamba Mtendaji Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania


 Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Faustine Ndugulile (Katikati) akitoka kukitembelea kituo cha TEHAMA cha Micheweni kisiwani Pemba akiambatana na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo pamoja na na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Na Faraja Mpina- WMTH, Zanzibar

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amefanya ziara ya kutembelea vituo vya TEHAMA Kisiwani Pemba vilivyopo Wete, machomane, Micheweni na Chonza ambavyo ni miongoni mwa vituo kumi vilivyojengwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa gharama ya shilingi 1,138,000,000 visiwani Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma za TEHAMA kwa wananchi.

 

Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika Wizara yake kuna maeneo ambayo ni ya kimuungano hivyo, ziara yake ni kwa ajili ya kutembelea na kufahamu shughuli mbalimbali zinazoendelea kufanyika ambazo ni za muungano na mojawapo ni vituo hivyo vilivyojengwa na UCSAF, vinne kisiwani pemba na sita kisiwani Unguja ambapo jumla ni vituo kumi.

 

“Tumeviona vituo vya TEHAMA, vina kompyuta lakini havifanyi kazi, niziombe taasisi zangu ziwe zinazungumza katika juhudi zetu tunazozifanya kwasababu tuna uwezo wa kushirikiana kufanya kwa pamoja katika baadhi ya maeneo, sio mfano UCSAF anajenga jengo na kuweka vifaa halafu halina intaneti wakati Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lipo lingeweza kuhakikisha intaneti inapatikana”, Dkt. Ndugulile

 

Aidha, amezisisitiza  taasisi za mawasiliano kuangalia huduma zinazoweza kuwekwa katika vituo hivyo ili viweze kutoa huduma ya pamoja na kusaidia uendeshaji wa vituo hivyo kuliko kuiachia mzigo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuviendesha kwa kulipia gharama mbalimbali za uendeshaji.

 

“Tukiweza kufanya vizuri katika vituo vya TEHAMA vilivyopo, vitatupa nguvu zaidi ya kupanua wigo wa vituo kama hivi katika maeneo mengine, ili huduma za TEHAMA ambayo ni haki ya msingi ya kila mwananchi ipatikane kwa wigo mpana zaidi visiwani hapa”, Dkt Ndugulile

 

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Bakari amesema kuwa kutakuwa na mpango wa dharura wa kuhakikisha vituo hivyo vinaanza kufanya kazi ndani ya muda wa wiki moja na baadae kutakuwa na mpango endelevu kwa kuhakikisha vituo hivyo vinaendelea kutumika.

 

Aliongeza kuwa wamefanya mazungumzo na TTCL ikiwa ni pamoja na taratibu za kufanya malipo ili kuhakikisha Shirika hilo linafikisha  huduma ya intaneti katika vituo hivyo ili wananchi waanze kuvitumia.

 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa Wizara hiyo ni ya muungano na wamekuja katika vikao wa mashirikiano baina ya Wizara hizo mbili ili kuangalia mafanikio na changamoto ili kuweza kuzitatua kwa pamoja.

 

“Katika ziara hii nimekuja na watendaji wa Wizara na wa taasisi zetu zote za mawasiliano ili kutembea pamoja kwa kila mmoja kujifunza kwa mwenzake na kutoka na mpango mkakati wa kuhakikisha tunatatua changamoto zilizopo na kuzidi kuuimarisha muungano wetu”, Dkt. Chaula

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba amesema kuwa amefarijika kuona Waziri huyo wa Serikali ya Muungano ametembelea vituo hivyo na kudhihirisha Tanzania Bara na Visiwani ni wamoja na yanayofanyika ambayo yanahusiana na sekta za muungano yanatekelezeka katika pande zote mbili.

 

“Ziara hii inadhihirisha tuna muungano imara na upo vizuri kufuatilia yale ambayo ni ya pamoja ili kuweza kuhakikisha mapungufu yanafanyiwa kazi kwa kushirikiana na kuyaweka vizuri, ndio maana ujio huu umetaja mpaka muda ambao vituo hivi vitaanza kufanya kazi”, alisema

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.