Habari za Punde

Fainali ya Mashindano ya Kuhufadhi Qur-an Kufanyika Zanzibar Uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar 24 April 2021.

Na.Sabiha Khamis - Maelezo Zanzibar. 05/04/2021

Ofisi ya Mufti Zanzibar ikishirikiana na Jumuiya ya Almanahilul Irfan pamoja na Jumuiya ya Kuhufadhisha Qur-an imewataka waislamu wote na wasiokuwa waislam kushiriki katika fainali ya mashindano ya kuhifadhi Qur-an Tukufu ya Afrika Mashariki yatakayofanyika tarehe 24/04/2021 katika uwanja wa Amani Zanzibar.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya Mufti wa Zanzibar Sheikh wa Mkoa wa Dar-es-salam Alhad Mussa Salum amesema anawakaribisha waislamu wote kwenda kusikiliza na kuona vipaji vya watoto waliohifadhi Qur-an Tukufu.

Amesema waislamu watakabiliwa na mwezi Mtukufu wa Ramadhani hivyo matarajio yake kuona wakimiminika katika viwanja hivyo ili kuwaona vijana  waliohifadhi Qur-ani tukufu wakionyesha vipaji kwa kuisoma Qur-an tukufu.

“Tunatarajia kuona waislamu wa Zanzibar wakijitokeza kwa wingi katika viwanja vya Amani ili kushuhudia vijana wetu wa Afrika Mashariki wakishindana katika kusoma Qur-an Tukufu” alisema Sheikh wa Mkoa wa Dar-es-salam.

Aidha ameeleza kwa upande wa Tanzania Bara wamemaliza mchujo kwa washiriki wa Juzuu tatu, saba na 20, na kubakisha Juzuu 30 ambao wanaendelea na mchujo wa mwisho wa nusu fainali utakaofanyika tarehe 09/04/2021 katika Masjid Azizi Mtoni kwa Azizi Ally Temeke.

Pia amesema mashindano hayo yatawashirikisha washiriki kutoka nchi jirani kama Uganda, Burundi, Rwanda, Somalia, Comoro, Msumbiji, Djibouti na Ethiopia.

Na kwa upande wake Mkuu wa Fatwa na Utafiti Ofisi ya Mufti Zanzibar Sheikh Thabit Nouman Jonga amewataka waislamu kuhudhuria kwa wingi pamoja na kuwashajihisha watoto wao kushiriki katika mashindano ya kuhifadhi Qur-an Tukufu ili kuipata shifaa ya Allah (S.W).

Katika mashindano hayo Mgeni Rasmin anatarajiwa kuwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.