Na. Paschal Dotto-MAELEZO
“Kama maendeleo ya kweli yatachukua nafasi ni lazima watu washiriki katika kujenga maendeleo hayo”. Ni kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuhimiza wananchi kushiriki katika ujenzi wa Taifa kwani nchi haijengwi na mtu mmoja, na waswahili husema ‘kidole kimoja hakivunji chawa’.
Hayati, Dkt. John Pombe Magufuli alipenda kutumia msemo usemao ‘kawia ufike, tumeamua tufike ni kauli ambayo alikuwa akiitumia Katika kuchukua dira ya kujenga uchumi wa kati kwa wananchi wake, Hayati Dkt. Magufuli alichukua dhamira ya kweli ya kuleta mapinduzi ya uchumi katika ngazi zote nchini, na hasa alitaka kuona Tanzania ikiwa na umeme wa kutosha utakaoweza kuendesha miradi mikubwa kama ule wa Reli ya Kisasa (SGR) mradi unaojengwa kutoka lango la uchumi Mashariki wa Tanzania hadi lango la uchumi Kanda ya ziwa.
“Duniani tuna nukuu
(quotes) za watu maarufu kama Martn Luther King, Jr. Abraham Lincoln na wengine
wengi. Kwa hapa kwetu tuna nukuu za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Sasa ni
wakati mwafaka kuweka nukuu zake kwenye uzi huu, usihofu iwe mbaya masikioni
mwako au iwe nzuri wewe weka tu maana lolote analo litamka Mkuu wa nchi
linapaswa kutunzwa”, Ni kauli ambazo zilitoka
kwa uzalendo mkubwa kutoka kwa Rais wa Awamu
ya Tano, Tanzania Hayati, Dkt.John Pombe Magufuli.
Maana hata Biblia katika kitabu cha Mithali sura ya
13:10, inasema “kiburi huleta mashindano tu, bali hekima hukaa nao
wanaoshauriana,” hii ni kauli ambayo inatoa mwelekeo mmoja kwa watu wote kusikilizana na kujua njia sahihi ya kuelekea kwa hiyo Watanzania hatuna budi
kujenga utamaduni wa kufanya kazi na kutekeleza majukumu kwa kufuata ushauri wa
viongozi.
Katika hotuba
mbalimbali, Hayati, Dkt. Magufuli alikuwa akisisitiza nia ya kuendeleza ndoto
za Mwasisi wa Taifa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiwemo ndoto ya kuhamia Dodoma makao
makuu ya nchi na ujenzi wa bwawa kubwa la umeme, Nyerere Hydro Power Project
(NHPP) katika mto Rufuji litakalogharimu shilingi trilioni 6.5.
Katika ukuaji wa
nishati nchini ilikuwa ni dhamira ambayo inaendana na Sera ya Serikali ya Awamu
ya Tano “Tanzania ya viwanda”. Moja ya ndoto kubwa ya Baba wa Taifa ilikuwa ni
ujenzi wa bwawa hilo litakalo zalisha Megawati
2,115 ili kuiwezesha Sera hiyo kufikiwa kwa uhakika zaidi na hapo mawazo yake
yalikuwa sahihi kama Hayati, Dkt. Magufuli alivyona akajenga mradi mkubwa wa
Reli ya kisasa (SGR) kilomita 1,200 inayogharimu shilingi trilioni 7.
“Kama tumeamua
kujenga nchi kwa ajili ya viwanda ni lazima tufanye uwekezaji wa kutosha katika
sekta ya nishati hasa kwenye umeme wa maji (Hydroelectric Power) na hii itakuwa
njia sahihi kwa ukuaji wa viwanda vyetu, lakini pia itatusaidia kwenye
uwekezaji wa miundombinu kama ya reli zinazotumia umeme”, Hayati, Dkt. Magufuli.
“Ukitaka kuruka agana
na nyonga,” hii ni kauli ambayo inasisitiza maandalizi ya kufanya kitu hususani
katika kufanya mapinduzi ya uchumi, katika Miradi hii mikubwa lazima wananchi
wote wanapaswa kujiandaa ili kuwa na mwelekeo mmoja katika kutimiza azma hiyo
ya kutengeneza nchi kwa vizazi na vizazi.
“Ninafahamu kuwa
umeme huu wa Steiglers Gorge (JNHPP) utapata mapingamizi mengi, lakini nawaomba
Watanzania tusimame imara katika kuhakikisha mradi huu unafanikiwa, kwa sababu
ndiyo yalikuwa mawazo ya Baba wa Taifa aliona mbali katika maendeleo ya nchi
yetu,” alisisitiza Hayati, Dkt. Magufuli.
Nchi nyingi za Afrika
sasa zimedhamiria kujenga na kuimarisha sekta ya nishati kupitia vyanzo vya
maji, Ethiopia ambao walitusaidia katika
ushauri wa mradi huu mkubwa wenyewe wana
nishati ya kutosha katika masuala ya nishati kwa hiyo ujenzi wa mradi huu
utainua sekta ya nishati na kukuza uchumi kwa wananchi kwani bei ya umeme
itashuka kwa hiyo Watanzania wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa mradi huo wa JNHPP
kwani ndio mradi mkubwa wa nishati na utakuwa
na umeme wa uhakika
Mathalani katika
hotuba yake, Hayati, Dkt. Magufuli na
wataalamu wa nishati kutoka Ethiopia alisema kuwa taifa hilo lina wataalamu
wengi na kuna mabwawa mengi ya Gibe 2 na 3 na lingine kubwa ambalo linajengwa
linalotarajia kuzalisha megawati 6,000, hivyo Tanzania haina budi kujenga bwawa
la JNHPP lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.
Katika harakati hizi
nzuri kwa Taifa la Tanzania wazo hili ni muhimu kutekelezwa ili kuleta maendeleo
katika maeneo mengi pamoja na kumuenzi Baba waTaifa kwa kuanzisha wazo hili.
“Tumeona twende na mawazo
mazuri yaliyowekwa na Hayati Baba wa Taifa
Julius Kambarage Nyerere tokea miaka ya
1972 na 1975 alipoamua kuunda sheria ya kuanzisha RUBADA kwa lengo la
kuhakikisha kuwa Steiglers Gorge (JNHPP), inajengwa kwa manufaa mapana ya nchi
yetu”, alifafanua Hayati, Dkt. Magufuli.
Mradi huo mkubwa
utagharimu shilingi za Kitanzania trilioni 6.5, ambazo zitatolewa na Serikali
ya Tanzania na lengo la Serikali ni kufikia megawati 5,000 ili kuwezesha
wananchi kuwa na nishati ya kutosha kutoka vyanzo mbalimbali, pia Serikali
inalenga kufikia megawati 10,000 ifikapo
mwaka 2025 kama Sera ya nishati ya mwaka 2015 inavyoeleza kuelekea uchumi wa
viwanda.
Katika tafiti
zilizopo nchini zinaonesha kuwa, Tanzania inaweza kuzalisha megawati 4,700 kutoka
katika vyanzo vyake vya maji, mradi huo mkubwa utawezesha wananchi katika eneo
husika kupata mahitaji mengine kama alivyoelezea Hayati, Dkt. Magufuli.
“Tukijenga mradi huu
tutategemea kuwa na eneo la ziwa la maji mengi ambalo litatumika kwa uvuvi,
wanyama wetu kunywa maji, litakuwa eneo zuri kwa utalii, kilimo cha
umwagiliaji, maji ya kunywa kwa wananchi pamoja na umeme megawati 2,115 utakaotolewa na bwawa hilo kwa hiyo ni mradi
mzuri wenye fursa nzuri za kiuchumi kwa Wananchi,”
alisisitiza Hayati, Dkt. Magufuli.
Kwa nchi kama
Tanzania yenye vyanzo vingi vya nishati, Serikali inawashauri wananchi kutoa
ushirikiano wa kutosha ili kuweza kuingia katika mapinduzi hayo akieleza kuhusu
vyanzo hivyo Hayati, Dkt. Magufuli
alisema kuwa..
“Kuna maeneo mengi na
vyanzo vingi sana vya nishati Uranium
ipo tu, Makaa ya mawe tani 1.9 milioni, gesi ujazo wa trilioni 57.25 pamoja na upepo kwa maeneo ya Singida
kwa hiyo tumeanzia kwanza kwenye ndoto ya Baba wa Taifa ya ujenzi wa wa Bwawa
la Julius Nyerere (JNHPP), kwa hizo megawati 2,115 na tutaendelea kujenga vituo
vingine kwa sababu wataalam wapo.”
Sekta ya nishati ni
muhimu kwa maisha ya wananchi wote kwa hiyo inatakiwa kuungwa mkono kwa
asilimia 100 na kusiwepo na lugha ya kutofautiana maana ndiyo sekta
itakayotufikisha kwenye ndoto yetu ya uchumi wa viwanda kwa sababu kwenye kuwekeza miradi mikubwa inafaa zaidi
kwa manufaa ya milele.
Hivi karibuni, Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alitembelea na
kujionea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambapo aliwaeleza Watanzania kutokuwa
na hofu juu ya mradi huo ambao Serikali imewekeza ili kulete uhuru wa kiuchumi
kwa Taifa na Serikali kwa ujumla.
“Wataalam Wetu
wametuambia kwa kasi ya mradi tuna matumaini kuwa ifikapo Juni mwaka 2022 mradi
utakuwa umekamilika, kwa sababu maeneo makubwa na nyeti ya mradi huu yamefikiwa
kwa asilimia 47, na Serikali itaendelea kutoa fedha kukamilisha mradi huu.
Bwawa hili litatoa Megawati 2,115 ambazo zikijumlishwa na Megawati 1,500
zinazozalishwa na vyanzo mbalimbali hivi sasa zitaifanya Tanzania kuwa na umeme
toshelevu”, Mhe. Kassim Majaliwa.
Alibainisha kuwa lengo kuanzisha mradi huo ni
moja ya juhudi za Serikali za kupunguza gharama za umeme kwa wananchi kwa
sababu uzalishaji wake ni wa gharama nafuu, uniti moja ya umeme unaozalishwa
kwa kutumia maji unagharimu shilingi 36 hadi shilingi 50.
Aidha, Majaliwa
alieleza gharama za umeme unaozalishwa kutoka katika kila chanzo cha uzalishaji
umeme ikiwemo upepo shilingi 103.5, jua shilingi 103.5, makaa ya mawe shilingi
114, jotoardhini shilingi 118, nyuklia shilingi 65 na gesi shilingi 147 huku
umeme wa maji gharama yake ikiwa ni ndogo kuliko zote yaani shilingi 36, hivyo
amewaomba wananchi waondoe hofu juu ya utekelezaji mradi huo kwani utakamilika
kwa wakati.
Kwa upande wake, Waziri
wa Nishati Dkt. Medard Kalemani Jumatatau ya Tarehe 12, 2021 alilieleza Bunge
kuwa Novemba mwaka huu Bwawa la kuzalisha umeme (JNHPP), litaanza kujazwa maji
rasmi na hapo ndiyo ndoto ya Hayati, Dkt. John Magufuli itaanza kutimia
kuelekea uhuru wa uchumi alioutaka kwa Watanzania.
No comments:
Post a Comment