Habari za Punde

“TUSITAFUTE HURUMA KAZINI” VIONGOZI WANAHABARI WANAWAKE

Na: Lillian Shirima – Habari MAELEZO

Manyanyaso na ubaguzi kazini dhidi ya wanawake licha ya kuwa tatizo kubwa kitaifa na kimataifa lakini pia ni tatizo  linaloathiri utu wa mwanamke, haki  za binaadamu na  afya za wengi  bila kujali kiwango cha elimu, maeneo wanayofanyia kazi na majukumu makubwa ya kujenga familia.

Akiongea na Habari MAELEZO,  Pili Mtambalike  ambaye ni miongoni mwa wanawake wanahabari  24 waliotunukiwa tuzo  maalum ya heshima  kutokana na mchango wao kwa wanahabari wachanga na jamii kwa ujumla kupitia tasnia ya habari amesema unyanyasaji wa wanawake kazini ni athari za mfumo dume ndani ya jamii.

“Kwa fikra zangu unyanyasaji wa wanawake sehemu za kazi ikiwa ni pamoja na vyumba vya habari ni muendelezo tu wa mifumo iliyojengeka katika jamii ambayo inatukuza na kumpa hadhi zaidi mwanaume kuliko mwanawake”.

Aidha, amesema tafiti kadhaa zilizofanyika ndani na nje ya nchi zinaonesha unyanyasaji dhidi ya wanawake ni matokeo ya silka ya mfumo dume ulioshika mizizi kwenye jamii zetu na kwamba nguvu zinazotumika kupoka haki za wanawake kwa kuwanyanyasa na kuwafanyia ubaguzi kupata vyeo zinaonekana pia katika tasnia ya habari

 

“Katika vyumba vya habari fursa za uongozi wanapata zaidi wanaume kuliko wanawake kwa visingizio kuwa sio viongozi wazuri, kwa sababu wana mihemuko ya hisia, wana majukumu ya kifamilia ambayo yanaingilia utendaji kazi wao jambo ambalo ni udhaifu wa fikra”.

 

Ingawa ni ukweli usiopingika kuwa wanawake wana majukumu mengi, lakini ili kuwapatia fursa za uongozi ni lazima kuwepo na utashi na dhamira ya kujenga mazingira ambayo yatasaidia utendaji kazi wa wao kuwa  mzuri,  kujenga mazingira wezeshi kwa wanawake na wasichana kupata fursa za uongozi.

 

Jambo hili litafanyika kwa kuweka sera za jinsia ambazo kila mfanyakazi atatakiwa kuzifahamu. Sera zitakazosaidia kujenga na kuimarisha  mifumo ya kusikiliza na kutatua malalamiko ya unyanyasaji wa kijinsia yanayotokea kwenye vyumba vya habari pamoja na adhabu zitakazostahili kwa wale wanaotumia madaraka yao vibaya.

 

Akizungumzia ufumbuzi wa tatizo hilo, Pili Mtambalike alisema, mchakato wa kupata Sera mpya ya Habari ulifanyika mwaka 2000 kwa Serikali kuwashirikisha wadau kikamilifu katika uandaaji uliofanikisha kupatikana kwa Sera ya Habari na Utangazaji ya Mwaka 2003.

 

“Asilimia 99 ya mapendekezo yote yaliyotolewa na wadau yalikubaliwa ambapo mapendekezo matatu ndiyo hayakuingizwa kwenye sera”, alisema Mtambalike.

Alitaja mapendekezo hayo kuwa ni Jinsia na vyombo vya habari ambapo wadau walipendekeza kuwepo kwa  maelekezo ya kisera ambayo vyombo vya habari vitatakeleza ili kupambana na mawazo mgando (gender stereotyping) na kutoa nafasi kwa wanawake ili sauti zao zisikike kwenye vyombo vya habari.  Lengo la kufanya hivyo lilikuwa ni kuwapa  ulingo wa  utekelezaji wa Maazimio ya Beijing (Beijing Platform of Action)

 

Mengine ni kuzuia kuhodhi umiliki mpana wa vyombo vya habari na kuwa na sera ambayo itazuia umiliki wa mtu au kampuni tofauti kuwa na vyombo vingi vya habari yaani magazeti radio, TV na tatu ni umiliki wa vyombo vya habari vya Serikali kuwa wa umma (Magazeti, Radio na Televisheni).

 

Aidha, Pili Mtambalike amesema suala la kujiamini, kupenda kazi na kuwa na shauku ya kujifunza ili kuboresha kazi za taaluma ya uandishi ni muhimu katika kupambana na  unyanyasaji wa jinsia katika sehemu ya kazi.

 

Akiwaasa Waandishi wa Habari wachanga alisema,  kutumia turufu ya kutaka upendeleo au unyonge kunachochea vitendo vya unyanyasaji na uonevu sehemu za kazi hivyo  ni muhimu kuwa waadilifu kazini  kwani uandishi wa habari ni kazi ambayo ina nguvu na ushawishi mkubwa hata kuweza kuponza vhombo wanavyochofanyia kazi au kuingia matatani kama hawatafuata maadili ya taaluma.

 

“Mwandishi wa kike ujiamini kwa sababu unajua kuwa unafanya kazi nzuri na kama utakasolewa uwe tayari kujifunza kazi iwe bora zaidi, unajiamini kwa sababu unajiheshimu na unaheshima kwa unaofanya nao kazi. Huna haja ya kujipendekeza au kujirahisisha kwa ajili ya ajira yako kwa sababu kazi yako inakusemea”.

 

Alibainisha kwamba waandishi wachanga wanao uwezo wa kutoka hapo walipo na kwenda kwengineko ambako watatambua michango yao bila mizengwe ya aina yoyote endapo wanajituma na kufanya kazi kwa ufanisi.

 

Kwa upande wake Mkurugezi wa TBC Taifa (Radio),  Aisha Dachi amewahimiza waandishi wachanga kujifunza,kujiamin na  kuwa  wasikivu na akawashauri kuwa tayari kukutafuta mtu (mentor) atakayewaongoza na kusimamia  maendeleo yao ili wapate ujuzi wa kujimarisha mara kwa mara.

 

“Vijana wa siku hizi muwe tayari kupata maarifa mara kwa mara, kushindwa mwanzoni kusikufanye ujione utashindwa siku zote, tafuta mtu atakayekusimamia au kukuongoza”, aliongeza Dachi.

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na taasasi zisizo za kiserikali liliandaa  kongamano  kupigania maslahi ya wanahabari hususan wanawake wakati Tanzania ikiungana na Mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Mei, 3.

Kaulimbiu ya Mwaka 2021 inasema ‘Habari kwa Manufaa ya Umma’ ambayo inatoa wito wa kuthamini na kutadhmini Habari kwa maanufaa ya umma ikiwa ni pamoja na kuangalia jinsi ambavyo vyombo vya Habari vinaweza kuandaa, kupokea, na kusambaza maudhui ili kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo alisema Serikali kama Wadau Wakuu na Watekelezaji wa Sera na Sheria itachukua hatua za haraka baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa wadau wa Habari juu ya nini kifanyike ili kutokomeza unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana katika vyombo vya habari.

Alishukuru UNESCO , Mashirika yasiyo ya kiserikali, Asasi za Kiraia na Wadau mbalimbali wa Habari kwa kuandaa kongamano akasema Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano na kupokea mapendekezo yakayosaidia kutengeneza mpango mkakati wa kushughulikia vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na wasichana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.