Habari za Punde

China Yaipatia Tanzania Msaada wa Shilingi Bilioni 35.37 Kwa Ajili ya Kutekeleza MIradi ya Maendeleo.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa China, Mhe.  Wan Ke (kushoto), wakisaini Mkataba wa msaada wa kiasi cha shilingi bilioni 35.37 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, Jijini Dar es Salaam.

Na. Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

Serikali ya China imeipatia Tanzania msaada wa yuan za China milioni 100 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 35.37 utakaotumika kutekeleza miradi itakayokubaliwa ama kuridhiwa na pande zote mbili.

 

Mkataba wa makubaliano ya msaada huo umesainiwa Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Wan Ke, kwa niaba ya Serikali ya China.

 

Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa Mkataba huo, Bw. Tutuba alipendekeza msaada huo utumike kupanua ujenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kupandisha hadhi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuwa Chuo Kikuu, kutekelea mradi wa uhifadhi wa Miamba katika eneo la Ngorongoro (Geopark), na miradi mingine itakayoafikiwa na Serikali zote mbili.

 

Aidha, aliishukuru China kwa misaada na mikopo yenye masharti nafuu inayoipatia Tanzania kuanzia mwaka 2010 na kutumika kujenga miundombinu ya Reli, Elimu, Afya, Tehama, Nishati, Maji, Sekta ya Viwanda, Kilimo, Usalama, na Misaada ya Kitaalam, iliyofikia dola za Marekani bilioni 1.8 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 4.15.

 

 

“Nachukua fursa hii kukuhakikishia kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha kwamba miradi itakayotekelezwa kwa fedha za msaada huu inakamilika kwa wakati ili kufikia malengo yaliyokusudiwa” aliongeza Bw. Tutuba

 

Kwa upande wake Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Wan Ke, alisema kuwa msaada huo ni matokeo ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Bw. Wang Yi, aliyoifanya mwezi Januari mwaka huu na ni mwendelezo wa ushirikiano mwema kati ya China na Tanzania uliodumu kwa zaidi ya miaka 57 sasa.

 

 “Tangu wakati huo China imeisaidia Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo ujenzi wa reli ya TAZARA, Uwanja wa Michezo wa Benjamin Mkapa, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNCC), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, na Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam” alisema Mhe. Balozi Wan Ke.

 

 

Alibainisha miradi mingine iliyofadhiliwa na China kuwa ni upanuzi wa Chuo cha Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro, Ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam ambapo miradi hiyo yote imekabidhiwa Serikali ya Tanzania.

 


“Vile vile tumewaleta madaktari wa kujitolea wapato 25 ambao wamekuwa wakijihusisha na utoaji wa tiba ya moyo na kupambana na malaria maeneo mbalimbali nchini na hivi sasa pia China imefadhili ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi mkoani Kagera ambacho ujenzi wake ukikamilika kitakuwa chuo kikubwa kuwahi kujengwa hapa nchini.

 

Aidha, Mhe. Wan Ke, alisema kuwa China imeipatia Tanzania msaada wenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.3 kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid 19 kwa ajili ya kununulia barakoa, vitakasa mikono,  vifaa tiba na dawa na kwamba nchi yake  imetia saini kushiriki kwenye mpango wa kuahirisha ulipaji wa madeni (DSSI) ili kuruhusu Serikali kuelekeza fedha hizo kwenye maeneo mengine katika kupambana na maradhi hayo yanayoendelea kuitikisa dunia.

 

Akizungumzia kuhusu uwekezaji wa China hapa nchini, Mhe. Balozi Wan Ke, alisema kuwa licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa Covd-19 na kuathiri uchumi wa nchi zote mbili, katika mwaka 2020, biashara na uwekezaji ulifikia dola milioni 4.58 sawa na ongezeko la asilimia 9.9.

 

“Uwekezaji wa mitaji wa China nchini Tanzania umefikia dola za Marekani milioni 159.71 ikiwa ni ongezeko la asilimia 62.37 na kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu kiwango cha biashara kimekua kwa asilimia 59.71 ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka uliopita 2020 huku bidhaa kubwa zinazoingia katika soko la China hivi sasa ni muhogo, mvinyo, na maharage ya soya” alisema Mhe. Ke.

 

Mhe. Balozi Wan Ke, alisema kuwa anaimani na uongozi wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameahidi kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini pamoja na kulinda uwekezaji ili kuwaongezea kujiamini zaidi na kwamba uamuzi huo unaungwa mkono na kampuni za China zilizowekeza hapa nchini na utawavuta wawekezaji wengi zaidi kutoka China kuja kuwekeza mitaji na teknolojia hapa nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia), na Balozi wa China, Mhe.  Wan Ke (kushoto) wakibadilishana hati za mkataba wa kiasi cha shilingi bilioni 35.37 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba na Balozi wa China, Mhe.  Wan Ke,  wakionesha mkataba wa msaada wa shilingi bilioni 35.37 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayokubaliwa na pande zote mbili, hafla iliyofanyika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa China, Mhe.  Wan Ke, wakipongezana baada ya kukamilika kwa halfa ya utiaji saini  Mkataba wa msaada wa shilingi bilioni 35.37, kati ya Tanzania na China, katika ukumbi wa Benki Kuu, Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa China, Mhe.  Wan Ke, wakiteta jambo wakati wa halfa ya utiaji saini msaada wa shilingi bilioni 35.37 kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China, Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China, Mhe.  Wan Ke, akizungumza wakati wa halfa ya utiaji saini mkataba wa msaada wa kiasi cha shilingi bilioni 35.37 kwa ajili ya miradi mbalimbali, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (hayupo pichani), wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa msaada wa shilingi bilioni 35.37 kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China, Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Naibu Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Bw. Melkizedeck Mbise, Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Wizara ya Fedha na Mipango Wakili Msomi Elias Kimath na Kaimu Kamishna Msaidizi Idara ya Mipango ya Kitaifa Bw. Royal Lyanga.

Ujumbe kutoka Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba (wa pili kushoto walioketi), wakiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Serikali ya China ukiongozwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Wan Ke (wa pili kushoto), baada ya hafla ya utiaji saini kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam.

 

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango – Dar es Salaam)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.