Habari za Punde

Misikiti Ina Kazi Zaidi ya Ibada ni Vyema Waumini wa Dini ya Kiislam Wakiitumia Kama Alivyokuwa Bwana Mtume Muhammad (SAW)

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kuashiria kuufungua Masjid Shifaa Muembetanga (zamani ukijulikana kwa jina la Msikiti Maiti) (kulia kwa Rais) Mfadhili wa ujenzi wa Msjid Shifaaa Dk.Mohamed Saeed  Mahfoudh, Waziri wa Katiba,Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar.Mhe.Haroun Ali Suleiman na (kushoto kwa Rais) Imamu Mkuu wa Masjid Shifaa Sheik. Mwalim Abubakar Said (Mwalimu Abuu) Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Khalid Ali Mfaume na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba mbali ya ibada ni vyema misikiti ikatumiwa katika masuala yanayohusu jamii.

Alhaj Dk Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akitoa nasaha zake katika ufunguzi wa Masjid Shifaa,  Mwembetanga, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini na Serikali pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu.

Alhaj Dk. Mwinyi ambaye mapema aliungana  wa Waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa katika msikiti huo, alisema kuwa misikiti ina kazi zaidi ya ibada hivyo ni vyema Waumini wa dini ya Kiislamu wakaitumia kama alivyokuwa akifanya kiongozi wa Waislamu Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) katika uhai wake.

Alisema kuwa katika jamii kuna matatizo mengi ambayo yanapaswa kujadiliwa na kufanyiwa kazi misikitini ikiwa ni pamoja na kuangalia utaratibu wa kuwasaidia wajane, wazee, watu wenye mahitaji maalum, kupambana na wizi, kupiga vita matumizi ya dawa za kulevyapamoja na udhalilishaji ambayo yapo katika jamii.

Aliongeza kuwa matatizo kadhaa katika jamii yakiwemo wizi na matumizi ya dawa za kulevya na udhalilishaji jamii imekuwa ikivitegemea sana vyombo vya usalama peke yake katika kupambana na majanga hayo jambo ambalo iwapo misikiti ikitimiwa vyema inaweza kutoa msaada mkubwa.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa misikiti inaweza kutumiwa zaidi ya ibada ya sala na badala yake ikawa ndio sehemu ya mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kufundisha  darsa pamoja na mafunzo mengine ya dini hiyo.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi amewataka Waumini wa dini ya Kiislamu kudumisha utamaduni wa matengenezo ya misikiti kwani misikiti baada ya kufunguliwa utamaduni wa kuifanyia matengenezo huwa haufanyiki na kusababisha kuanza kuharibika mapema.

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi amewasisitiza watakaousimamia msikiti huo ni vyema wakafuata utaratibu wa kufanya matengenezo kwa msikiti huo ili uweze kutumika kwa muda mrefu.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema vitega uchumi vya misikiti pamoja na sadaka zinazotolewa na Waumini zikaendelea kutumika katika kusaidia kuendesha misikiti ikiwa ni pamoja na kuifanyia matengenezo.

Katika nasaha zake hizo kwa Waumini wa dini ya Kiislamu Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa shukurani zake kwa mfadhili wa msikiti huo pamoja na kutoa shukurani kwa mwaliko huo alioupata wa kufungua msikiti huo ambapo hapo awali kabla ya kujengwa upya ulijulikana kwa jina la ‘Msikiti Maiti’.

Nae Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Katiba, Sheria , Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alimpongeza Alhaj Dk. Mwinyi kwa kuwa na utaratibu mzuri wa kuungana na waumini katika mambo ya kheri zikiwemo sala za Ijumaa na Taraweh.

Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume alieleza faida anazozipata mtu mwenye kujenga msikiti ikiwa ni pamoja na kujengewa nyumba na MwenyeziMungu Peponi.

Pia, Sheikh Khalid alieleza faida ya kutoa sadaka hali ambayo inampelekea mtoaji kufutwa madhambi yake na Mwenyezi Mungu huku akisisitiza kwamba mali ya anayetoa sadaka haipotei na badala yake huongezeka.

Sheikh Khalid alieleza haja ya kuisimamia na kuitunza misikiti kwa kuiifanyia usafi, kutoa taaluma huku akitumia fursa hiyo kuwataka waumini kuzidisha mapenzi baina yao, kusameheana sambamba na kuongeza juhudi katika kuondokana na fitna.

Akitoa maelezo mafupi mfadhili wa msikiti huo Dk. Mahfoudh alieleza hatua zilizochukuliwa katika kuujenga upya msikiti huo kwa mashirikiano ya mafundi na mainjinia huku akiwasihi waumini kuwa kitu kimoja katika kuuendeleza msikiti huo.

Mapema akisoma hotuba ya Sala ya Ijumaa, Sheikh Abdulqadir Said Abdalla alieleza haja kwa waumini kulitumia vyema kumi hili la mwisho la mwezi wa Ramadhan kwa kufanya ibada.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.