Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi Amewaombea Dua Wananchi wa Mkoa wa Mjini Unguja Kwa Mwenyenzi Mungu Kila la Kheri na Malipo Mema ya Swaumu zao Wananchi wa Mkoa wa Mjini.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi,na (kulia kwa mufti ) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar.Mhe.Haroun Ali Suleiman baada ya kumalizika kwa hafla ya futari maalum aliyowaandalia Wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja iliofanyika katika ukumbi wa jengo la Michezani Mall Jijini Zanzibar na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.Mhe.Idrisa Mustafa Kitwana  na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Ndg. Talib Ali, wakiitikia dua.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu kuwajaalia kheri na malipo mema ya swaumu, wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi waliojumuika pamoja nae katika hafla ya Iftari.

Dk. Mwinyi  ameomba dua hiyo leo katika  Iftari aliyoianda kwa ajili ya wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi katika hafla iliofanyika Ukumbi wa Jengo la  Michenzani Mall, jijini Zanzibar, ikiwa ni muendelezo wa utaratibu wake wa kufutari pamoja na wananchi wa Mikoa yote mitano ya Zanzibar .

Amemuomba Mwenyezi Mungu atakabali swaumu za wananchi hao na kuwalipa malipo mema , huku akiwashukuru kwa dhati kwa kuitikia wito wake wa kujumuika na kufutari pamoja.

Aidha, Dk. Mwinyi ameushukuru Uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa maandalizi mazuri yaliofanikisha Iftari hiyo pamoja na zawadi mbali mbali walizomtunukia.

Katika hafla hiyo,  Dk. Mwinyi amepata fursa ya kufutari pamoja na makundi mbali mbali ya wananchi wa Mkoa huo, ikiwemo kundi la  watu wenye Ulemavu, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla.

Nae, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amemshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa takrima aliyofanya kwa wananchi hao  na kumuomba Mwenyezi Mungu  amzidishie kheri nyingi yeye na familia yake.

Aidha, aliwashukuru wananchi wote walioitikia wito wa kiongozi huyo na kujumuika pamoja na katika Iftari hiyo, sambamba na kumtunukia zawadi mbali mbali, ikiwemo mas-hafu, saa ya ukutani (kwa ajili ya mama Mariam) pamoja na marfaa’gh kwa ajili yake na familia yake.

Mapema, akitoa neno la shukurani, Mwinyichande Haruna Mohamed kutoka kundi la watu wenye Ulemavu, alimuombea kheri Rais Dk. Mwinyi na kumuomba Mwenyezi Mungu amuwezesha kutekeleza kwa mafanikio yale aliyolenga kuyafanikisha katika uongozi wake.

Aidha, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huo, amesema wananchi wamefarijika mno kutokana na uongozi wa Dk. Mwinyi kwa kuwasogeza karibu na Serikali yao.

Viongozi mbali mbali wa Serikali, akiwemo Mama Mariam Mwinyi, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Mawaziri, masheikh na wananchi walihudhuria katika hafla hiyo ya Iftari.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.