Habari za Punde

Zanzibar Yaadhimisha Siku ya Kupinga Matumizi ya Tumbaku Duniani.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto Mhe.Nassor Ahmed Mazrui akizungumza katika hafla Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita matumizi ya Tumbaku kwa hiari, wakati akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali Zanzibar katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazi mmoja Jijini Zanzibar. 
Kaimu Meneja Kitengo cha Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Omar Abdalla Ali akitoa maelezo ya Madhimisho ya Siku ya Tumbaku hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.

Na Khadija Khamis –Maelezo . 31/05/2021.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Mhe, Nassor Ahmed Mazrui ameitaka jamii kuachana na matumizi ya tumbaku na sigara kwani  huathiri afya kwa mtumiaji na ni kichocheo kikubwa cha maradhi yasioambukiza .

Aliyasema hayo  katika Ukumbi wa Wizara ya Afya  Mnazi Mmoja wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbali mbali  vya habari ikiwa ni Maadhimisho ya Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku Duniani  .

Alisema matumizi ya tumbaku ikiwemo uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya ya mtumiaji pamoja na wanaomzunguka  linasababisha athari ya tumbaku kuwa na sumu zaidi ya aina 1,000.

Waziri Mazrui alisema sumu ya athari ya tumbaku husafirishwa kwa njia ya mzunguko wa damu na hatimae kusababisha athari mwilini na kudhuru afya ya binadamu ikiwemo watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano

“Zaidi ya watoto 60,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki dunia kutokana na kuvuta moshi kwa wavutao sigara na kubainika kwamba kati yawatoto saba kati ya wavutaji sigara kumi huanza uraibu wakiwa watoto na kuendelea kuvuta sigara kwa muda mrefu wa maisha yao”, alifahamisha Waziri huyo.

Alieleza kuwa baadhi ya madhara ya utumiaji wa tumbaku na sigara  ni ugonjwa ya mapafu kwa kupasuka kwa vibofu vya hewa safi, saratani ya koromeo na kuziba njia ya hewa na hatimae kushindwa kupumua .

Waziri huyo alisema ongezeko kubwa la maradhi ya saratani kwa upande wa Zanzibar linatokana na matumizi ya tumbaku na kuleta athari mbali mbali ikiwemo kuongezeka kwa maradhi yasioambukiza ikiwemo matatizo ya moyo ugonjwa ya mfumo wa hewa na maradhi mengineyo.

“Zaidi ya asilimia 7.3 kwa  watu wa Zanzibar hutumia tumbaku za aina mbalimbali  kama sigara, mvuato na kadhalika kati ya hao asilimia 14.6ni wanaume na 0.7 ni wanawake”, alifahamisha Waziri Mazrui.

Nae Kaimu Meneja wa Maradhi Yasiombukiza kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Omar Abdalla Ali alisema maradhi yanayoongoza kwa vifo na wagonjwa wengi ni shindikizo la damu  ambalo husababisha kupata kiharusi .

Aliyataja maradhi yasiyoambukiza ambayo yaathiri jamii ni pamoja na figo kushindwa kufanya kazi, moyo kushindwa kufanya kazi, saratani ya matiti saratani ya shingo ya kizazi saratani ya kifuko cha mkojo pamoja na tenzi dume .

Alifahamisha kuwa matumizi ya tumbaku na sigara ni moja ya kichocheo cha kupelekea saratani ambayo ina sumu mbaya sana ambapo  ujumbe wa maadhimisho ya mwaka huu “JITOE KATIKA MATUMIZI YA TUMBAKU” .


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.