RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema wakati
umefika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyakazi kwa karibu na wananchi, ili
waweze kutambua umuhimu wa kuwepo Jumuiya hiyo.
Dk. Mwinyi amesema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar, alipozungumza na Ujumbe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Dk. Peter M. Mathuki, uliofika kwa ajili ya kusalimiana.
Amesema azma ya Jumuiya hiyo kufanya baadhi ya vikao vyake vya Bunge pamoja na Mahakama hapa Zanzibar, itawafanya wananchi wawe na uelewa wa kuwepo kwa Jumuiya hiyo pamoja na kujenga imani nayo.
Aidha, alisema hatua ya Ujumbe huo kukutana na viongozi wa sekta binafsi hapa Zanzibar ni jambo jema, hususan katika uimarishaji wa biashara kwa kuzingatia kuwa wadau kutoka sekta binafsi ndio wanaofanya biashara.
Aidha, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuendeleza biashara pamoja na kuondokana na vikwazo mbali mbali vilivyopo .
Rais Dk. Mwinyi, alisema kuna umuhimu wa kuitumia ipasavyo bahari ili kuimarisha uchumi wa Taifa na kubainisha Zanzibar kuwa na sera ya Uchumi wa Buluu.
“Katika uchumi wa Buluu kuna sekta kadhaa, ikiwemo Utalii, Uvuvi, mafuta na gesi, miundombinu ya bandari pamoja na usafirishaji wa baharaini, lengo ni kuupa nguvu Uchumi huo, pamoja na kuwepo bahari bado haijatumika vilivyo, hivyo ni vyema tukaweka nguvu katika kuimarisha uchumi”, alisema.
Alisema Viongozi hao wakiwa wadau wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanapaswa kufikisha ujumbe kwa nchi wanachama kuwa Zanzibar iko tayari kupokea wawekezaji.
Akizungumzia Kamisheni ya Kiswahili, alisema amefurahishwa na juhudi zinazoendelea katika kuimarisha Kamisheni hiyo katika uimarishaji majengo pamoja na upatikanaji wa huduma, hatua itakayosaidia sana kuiendeleza lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na Bara zima la Afrika.
Aidha, alisema wakati umefika wa kuhakikisha ubora wa viwango wa bidhaa zinazozalishwa kutoka miongoni mwa nchi wanachama, zinasajiliwa na kutumika katika nchi zote wanachama wa Jumuiya hiyo.
Vile vile alipongeza uwepo wa miradi kadhaa ya pamoja ya maendeleo, ikiwemo ha miundombinu ya barabara katika nchi wanachama, na kutumia nafasi hiyo kuishauri Jumuiya kuipatia fursa Zanzibar katika miongoni mwa miradi itakayoanzishwa, ikiwa ni hatua ya kukuza ushirikiano.
Nae, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dk. Peter M. Mathuki, alisema hali ndani ya Jumuiya hiyo hivi sasa ni shwari, lengo likiwa ni kuipeleka karibu na wananchi.
Alisema ni lengo la Jumuiya hiyo kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika mawasiliano, na kuipongeza Serikali kwa kuipatia eneo kwa ajili ya Ofisi, wakati ambapo Uongozi wa jumuiya hiyo unaendelea na mchakato wa kutafuta fedha ili kuwa na eneo la kutosha.
Aidha, alisema miongoni mwa shughuli zilizofanywaa na Viongozi wa Jumuiya hiyo tangu wawasili Zanzibar ni pamoja na kukutana na viongozi wa sekta binafsi, lengo likiwa ni kuangalia namna bora ya kuwasaidia kuingia katika Uchumi wa Buluu.
Alisema Jumuiya inalenga kuwa na Kamati maalum itakayokuwa na jukumu la kuondoa vikwazo na kuwawezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao katika masoko mbali mbali yalioko katika nchi wanachama.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment