RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Jezi na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa kwa ajili ya kukimbilia katika Zanzibar Marathon yanayotarajiwa kufanyika mwezi ujao katika Uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar na (kushoto kwake) Maneja Masoko wa Kampuni ya Just Fit Ndg. Jabir Ali Jabir,baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa Jezi na Balozi wa Zanzibar International Marathon Bi. Salama Jabir kwa ajili ya kukimbilia katika Zanzibar Marathon yanayotarajiwa kufanyika mwezi ujao katika Uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar,baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kufanyika
kwa Tamasha la Mashindano ya Kimataifa ya Marathon (Zanzibar International Marathon –
ZIM ) hapa nchini, kutaonyesha utayari wa Serikali katika kuvutia Wawekezaji,
hususan kupitia sekta ya Utalii.
Dk. Mwinyi amesema hyo leo Ikulu Jijini Zanzibar, alipozungumza na Viongozi, Wadhamini, Mabalozi na Wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya Tamasha la Mashindano ya Kimataifa ya Marathon (ZIM) yalio chini ya Uratibu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar.
Amesema pamoja na tamasha hilo kuitangaza Zanzibar pia litaleta sura ya kuwahamasisha watu mbali mbali kuja kuona vivutio vya Utalii vilivyopo nchini na kuwekeza katika shughuli mbali mbali za kibiashara.
Alisema mchezo wa Marathon ni miongoni mwa mambo yenye kusisimua Utalii, hivyo akaahidi Serikali kuunga mkono hatua zote za maandalizi ya mashindnao hayo hadi kukamilika kwake.
Aliwashukuru waandaaji wa mashindano hayo na kubainisha furaha aliyonayo kutokana na wazo linalolenga kuutangaza Utalii wa Zanzibar, wakati huu Dunia ikikabiliwa na janga na maradhi ya Covid 19.
Dk. Mwinyi aliwapongeza Mabalozi na Wadhamini wa Tamasha hilo kwa utayari wao wa kufanikisha tamasha hilo, huku akiahidi Serikali kufanya juhudi ya kuzihamasisha Asasi za Kiserikali nchini kusaidia kuchangia mashindano hayo.
Alisema kufanyika kwa Tamasha hilo kutaleta chachu ya kurejesha matamasha mbali mbali ambayo kwa sababu moja au nyengine yamesimama, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi, hususan kupitia sekta ya Utalii.
Alisema tamasha hilo litasaidia kukuza vipaji vya michezo kwa vijana wa Zanzibar pamoja na kustawisha afya zao, hivyo ni wajibu wa Serikali kuunga mkono juhudi hizo.
Alieleza kuwa suala la kuwasaidia wazee ni jambo jema, kwa kuzingatia kuwa hilo ni jukumu la msingi la serikali, hivyo pale zinapotoa taasisi zenye nia ya kuisaidia jamii, hatua hiyo haina budi kuungwa mkono.
Nae, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Lela Mohamed Mussa alisema Tamasha hilo litafanyika Julai 18, 2021 katika Uwanja wa Amani na kuhusisha mbio za masafa tofauti (km 21, km 10 pamoja na km tano ) ambapo washiriki watapita katika maeneo mbali mbali ya Jiji la Zanzibar.
Aidha, alisema mashindano hayo yatahusisha watoto na wazee watakaokimbia masafa ya mita 700, ambapo washindi watatunukiwa zawadi.
Akigusia suala la usajili wa mashindano hayo, Lela alisema wageni watalazimika kulipia ada ya Dola 50, malipo ya shilingi 30,000 kwa Watanzania, shilingi 20,000/ kwa Vijana na Wanafunzi wa Vyuo pamoja na shilingi 15,000/ kwa watoto, sambamba na washindi kutunukiwa Medali.
Aidha, Waziri Lela alimuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi kuwa miongoni mwa washiriki wa mashindano hayo kwa lengo la kuhamasisha michezo sambamba na kustawisha Utalii.
Mapema, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hassan Zanga, alisema ZIM imeamua kurejesha mashindano hayo kwa lengo la kuhamasisha michezo yote, ikiwemo Marathon pamoja na Utalii kupitia sekta ya Uchumi wa Buluu.
Aidha, Afisa Habari wa Kamati hiyo (ZIM) alisema wazo la kufufua mchezo huo linalenga kuunga mkono kauli za Rais Dk. Mwinyi alizozitoa wakati wa Kamapeni ya Uchaguzi Mkuu (2020) ya kuendeleza michezo pamoja na muongozo alioutoa kwa wananchi kuwa michezo isiishie katika kukuza vipaji vya vijana pekee bali iwe suala la kibiashara.
Alisema mashindano hayo yatakayowashirkisha wanamichezo kutoka ndani na nje na nchi yanalengo la kurejesha mchezo huo pamoja na kutoa msukumo wa kuimarisha uchumi ambao umeathirika kutokana na maradhi ya Covid 19.
Alisema changamoto kubwa inayoikabili Kamati hiyo ni suala la udhamini, ambapo kabla ZIM ililenga kupata wadhamini kutoka taasisi ziliopo Zanzibar kwa asilimia mia moja, jambo ambalo lilishindikana hivyo kulazimika kuvuka upande wa pili wa Muungano.
Aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kuunga mkono juhudi za Kamati hiyo ili kufanikisha Tamasha hilo ambapo hatimae linalenga Zanzibar kuwa kituo kikubwa cha Utalii.
Nao, Mabalozi wa Kamati hiyo (ZIM) Maulid Kitenge, Hilary Matuta (Zembwela) pamoja na Salama Jabir, walimuomba Rais Dk. Mwinyi kuzihamasisha Kampuni na taasisi ziliopo Zanzibar kudhamini mashindano hayo.
“Mashindao hayo ni shughuli za kiuchumi na kiafya, yanatoa fursa ya kuitangaza Zanzibar kwa upana kwani yatahusisha washiriki kutoka maeneo mbali mbali Duniani”, alisema Zembwela.
Aidha Wawakilishi wa Kampuni zinazodhamini mashindano hayo; Benki ya NMB, VODACOM pamoja na Kampuni Justfit inayojishughulisha na shughuli za michezo, wamesema wameamua kuunga mkono wazo la kufufua mchezo huo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza uchumi kupitia sekta ya Utalii.
“Tumejiandaa kufanikisha mandalizi hayo kwa kurahisisha mifumo ya malipo kwa washiriki wa mashindao kwa kujisajili kidigitali hivyo kutoa fursa kwa wageni kujisajili wakiwa nchini kwao”, alisema Abdalla Duchi kutoka NMB Zanzibar.
Mwakilishi wa Kampuni ya Justfit Jabir Ali Jabir alisema Kampuni hiyo inayojishughulisha na uagiziaji na uuzaji wa vifaa mbalimbali vya michezo inalengo la kuwekeza hapa Zanzibar baada ya kubaini kuwepo kwa fursa za uwekezaji, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mashindano ya Kimataifa ya Marathon yalifanyika baina ya mwaka 1997 hadi 2002 katikia Mikoa mbali mbali ya Zanzibar na kuyashirikisha matafa mbali mbali Duniani kabla ya kusimama hadi leo kutokana na sababu tofauti
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment