Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Mwakilishi Mkaazi wa WHO Nchini Tanzania.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afri Duniani Nchini Tanzania (WHO) Dr.Tigest Ketsela Mengestu, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika leo 3/6/2021 katika ukumbi wa Ikulu akiwa na Ofisa wa WHO Zanzibar Dr.Ghirmay Redae Andemichael

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali iko tayari kupokea msaada wa chanjo COVID -19 pamoja na misaada mbali mbali ya kitabibu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

Dk. Mwinyi amesema hayo Ieo Ikulu Jijini Zanzibar , alipokutana na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani, anaefanyia shughuli zake nchini Tanzania Dr. Tigest Ketsela Mengestu, aliefika kujitambulisha.

Amesema sekta ya Afya nchini ina mahitaji makubwa ili iweze kufanikisha lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo azma ya WHO kuendelea kuisadia Zanzibar katika nyanja mbali mbali, ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa madaktari na wafanyakazi wa Afya pamoja na uimarishaji wa miundombinu ni jambo muhimu.

Alisema katika hatua ya kuimarisha utoaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi, kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo Bima ya Afya nchini.

Aidha, alisema kuna haja ya kuimarisha miundo mbinu ya huduma za Afya, hususa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambayo hivi sasa haikidhi mahitaji ya wakati katika utoaji wa huduma kutokana ongezeko la watu pamoja na ufinyu wa nafasi.

Alisema Hospitali hiyo yenye majengo ya kale, ina ufinyu mkubwa wa nafasi,  ikiwemo uchache wa vyumba vya upasuaji hususan kwa  magonjwa makubwa kama vile  moyo  pamoja  na kuwa na wodi chache za kulaza wagonjwa.

Alisema hali hiyo imeifanya Serikali kuweka malengo ya kujenga Hospitali kubwa na ya kisasa katika eneo la Binguni, Mkoa wa Kusini Unguja.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alilishukuru shirika hilo kwa mashirikiano pamoja na misaada mbali mbali inayotoa kwa Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za Afya nchini.

Mapema, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO)  nchini Tanzania Dr. Tigest Ketsela Mengestu, alisema WHO iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala la kuimarisha sekta ya Afya nchini, hususan katika  utoaji wa mafunzo kwa madaktari na wafanyakazi wa sekta hiyo.

Alisema Shirika hilo linalenga kuendelea kuisaidia Zanzibar katika kuwajengea uwezo  wataalamu wa Afya ili waweze kutoa elimu hiyo kwa wananchi katika kukabiliana na   magonjwa mbali mbali kama vile kipindupindu, ukosefu wa lishe, mafua makali pamoja na COVID -19.

Aidha, akaiomba Serikali kubainisha aina ya chanjo ya COVID-19 inayohitajika, sambamba na kuhakikisha mchakato wa kuwapatia chanjo Mahujaji  wa Zanzibar unakamilika kwa wakati, ikizingatiwa muda mdogo uliobaki kabla ya kufanyika kwa ibada hiyo.

Dr. Mengestu alimhakikisha Rais Dk. Mwinyi kuwa WHO itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya Afya nchini, ikiwa ni hatua ya kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu, ulioasisiwa tangu miaka ya 1960.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.