Na.Beatrice Sanga-MAELEZO.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari Maelezo imejipanga kupinga ukatili wa kijinsia ndani na nje ya vyumba vya habari kwa kuhakikisha kuwa Tasnia ya Habari inakuwa na sauti moja katika kutetea na kuwawezesha wanawake kwenye vyombo vya habari.
Hayo
yamesemwa jana katika mkutano wa siku
nne wa kupanga mradi wa kuimarisha nafasi ya vyombo vya habari katika
kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ulioandaliwa na Shirika la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na
Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto na Wadau mbalimbali wa kupigania haki za
Waandishi wa Habari Wanawake unaoendelea mkoani Morogoro.
Akizungumza
katika kikao hicho Afisa Habari Mkuu na Mwakilishi kutoka Idara ya HABARI
MAELEZO Bi Ingiahedi Mduma alipokuwa akielezea nafasi ya Wizara katika
kukabiliana na ukatili wa ndani na nje ya chumba cha habari, alisema kuwa
Serikali kupitia Idara hiyo imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali ya ukatili
wa kijinsia wanaofanyiwa wanawake ndani na nje ya chumba cha habari na kuweka
wazi mikakati mbalimbali ya Wizara ambayo itawezesha kukabiliana na tatizo
hilo.
Bi Mduma Amesema kuwa, Serikali imejipanga
kukomesha ukatili wa kijinsia katika vyombo vya habari kwa kutoa ushauri na
kuwatambua waandishi wa habari wanawake kwa kuwajengea uwezo wa kujiamini na
kujitambua ili waweze kukabiliana na waajiri wao na kuepukana na vitendo vya
unyanyasaji wa kijinsia
“Kumekuwa na malalamiko kuwa baadhi ya wasimamisi/wahariri
wanatabia ya kuwalaghai wasichana ili wafanye nao mapenzi kwa kuwadanganya kuwa
watawaajiri. Tabia hii inaenda kinyume na maadili ya taaluma ya uandishi wa
Habari, Hatua thabiti
zitachukuliwa pale itakapobainika na kuthibitika kuwa kumetendeka unyanyasaji
wa kijinsia ndani na Nje ya vyumba vya habari”,Amesema Mduma
Aidha ameongeza kuwa Serikali Inaendelea kuboresha mazingira katika
sekta ya habari ili kuwawezesha waandishi kutekeleza majukumu yao bila hofu, na
kwa kujiamini huku wakizingatia sheria, kanuni, maadili na weledi ili wananchi
waweze kupata habari sahihi kwa ajili ya manufaa ya Taifa na maendeleo yao.
Mkutano
huo umekuja kufuatia maazimio ya Mkutano wa siku ya uhuru wa vyombo vya Habari
Duniani ambao kitaifa ulifanyika Jijini Arusha Mei 3,2021.
No comments:
Post a Comment