Na. Mwashungi Tahir Maelezo 30-6-2021.
WAZIRI wa Nchi Afisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Mhe.Mudrik Ramadhani Soraga amesema Idara ya Uwezeshaji kiuchumi ina lengo la kuwapatia elimu na mafunzo wajasiriamali ili waweze kujiongeza katika maisha yao.
Ameyasema hayo huko katika ukumbi wa Golden Tulip Malindi wakati akifunga shindano la mpango wa biashara kwa wajasiriamali na kuwataka elimu waliyokuwa nayo waiendeleze.
Amesema lengo lakupatiwa elimu na mafunzo wajasiriamali hao ni kuwashajihisha kuingia katika ujasiri pamoja na kuwasaidia kwa kuwawezesha kupata mitaji ili kujiendeleza katika shughuli zao za maisha.
Aidha amesema lengo ni kukuza ubunifu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati katika sekta ya Teknohama IT , Utalii na usarifu wa mazao pamoja na mafunzo ya uwokaji ili kuweza kutatua changamoto za ajira na kuongeza kasi ya mafanikio Zanzibar.
Pia amesema kutokana na ukosefu wa ajira kwa vijana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka kituo cha kulea wajasiriamali na kuchukua juhudi katika kubuni nyenzo za miradi tofauti ya kuwawezesha vijana ili waweze kuibua fursa zilizopo katika sekta mbali mbali kwa kuondokana na changamoto za ajira.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu Uwezeshaji na kiuchumi Ameir Haji Sheha amewataka wajasiriamali kukuza vipaji vyao ili waweze kujiwezesha kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi.
Nao wajasiriamali wa mafunzo hayo wameishukuru Serikali kwa jitihada wanazozichukua katika kuwawezesha kwa kujiinua kiuchumi ambapo mshindi wa kwanza katika shindano hilo ni Nassor Abdullah Nassor katika mradi wa kugundua gesi Rock tech service kati ya washindi kumi.
No comments:
Post a Comment