Habari za Punde

Bilioni 1.2 Kujenga Soko la Kimataifa la Kuuzia Dagaa Kipumbwi Wilayani Pangani.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki akimsikiliza kwa umakini Mkuu wa wilaya ya Mkinga Kanali Maulid Surumbu wakati wa ziara yake katika  Kijiji cha Horohoro wilayani humo kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya ambapo kunajengwa mnada wa mifugo wakati alipolitembelea eneo hilo kulia ni Mbunge wa Jimbo la Mkinga (CCM) Dastan.Kitandula.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki kushoto akigawa  vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kilimo cha mwani kwa vikundi vitatu vya wakulima wa zao hilo wilayani Mkinga


Na.Oscar Assenga -Pangani.

SERIKALI inatarajiwa kutumia Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa la kuuzia dagaa Kata ya Kipumbwi Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga ambalo litatumika na wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo, iliyoambatana na ukaguzi wa majengo ya Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika Wilaya za Mkinga na Pangani.
 
Majengo hayo yaliyojengwa kupitia mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH).

Alisema wanunuzi wa dagaa wanaotoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Rwanda na Burundi wataenda kununua dagaa kutoka Kipumbwi hivyo wafanyabiashara wa kata hiyo hawatapata shida ya kutafuta soko la dagaa.

“Niwaambie serikali imesikia na inakusudia kujenga kujenga soko la Kimataifa la kuuza dagaa, msipate shida kuuza dagaa wenu.” Alisema
Waziri Ndaki.

Aidha, Waziri Ndaki alitoa onyo kwa viongozi wa BMU maeneo mbalimbali nchini, ambao wamekuwa wakishiriki vitendo vya uvuvi haramu pamoja na baadhi ya wavuvi kuwa vikundi hivyo vitavunjwa na wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Alifafanua pia baadhi ya BMU zimekuwa zikishindwa kutekeleza wajibu wake na kujikuta wakishirikiana na wavuvi haramu ambapo aliwataka kuacha vitendo hivyo kabla hawajakumbana na mkono wa sheria.

Akiwa wilayani Mkinga kwenye Kijiji cha Zingibari, Waziri Ndaki alisema serikali itaendelea kuwawezesha wakulima wa mwani kwa vifaa pamoja na utaalamu ili waweze kuzalisha kwa tija  zao hilo kwa wingi na ubora
unaohitajika sokoni.

Alitoa kauli hiyo wakati akitoa vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya kilimo cha mwani kwa vikundi vitatu vya wakulima wa zao hilo wilayani Mkinga.

Alisema kuwa kutokana na zao hilo kuwa la kiuchumi kwa wananchi wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi, serikali imeanza kuweka mazingira mazuri ya uwezeshaji na kutafuta masoko ya uhakika ili wakulima
waweze kunufaika kiuchumi.

"Huu msaada wa vifaa kwa ajili ya kilimo utafika katika maeneo yote yenye uzalishaji na msisitizo tumeanza kuweka kwenye elimu ya
namna ya kulima zao la mwani kwa ajili ya tija zaidi." alisema Waziri Ndaki

Kuhusu sekta ya mifugo, Waziri Ndaki alieleza sababu za kuanzishwa minada kwenye mipaka mbalimbali hapa nchini ambapo ikiwa na lengo la kuhakikisha wafugaji kutoka Tanzania wanauza mifugo kwenye minada hiyo
na wanunuzi wanatoka nchi nyingine kwenda kununua ili kudhibiti
utoroshaji.

Waziri Ndaki alisema hayo baada ya kufika katika mnada wa mipakani wa Horohoro kujionea miundombinu mbaimbali inayowekwa kabla ya kuanza rasmi kwa mnada huo ambao anasema utakuwa na matokeo chanya pindi utakapokamilika.

“Licha ya kusaidia kupunguza utoroshaji wa mifugo mnada utasaidia kuongeza kipato kwa wananchi na hivyo kuinua uchumi wao, kwa sababu wakipeleka ng’ombe nje ya nchi wanauza bei ya juu lakini pia tunataka tuwapunguzie wananchi adha ya kuvuka mipaka kwani jambo hili wakati mwingine linasababisha kuuza mifugo yao kwa bei ya
chini” Alisema

Hata hivyo Waziri Ndaki alisema wameamua kuondoa shida hizo kwa kuwa na minada ya mipakani ili wafugaji waweze kuuza mifugo yao maeneo rasmi na serikali iweze kupata mapato yao .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.