Habari za Punde

MHANDISI MASAUNI AIAGIZA UTT AMIS KUWAELEZA WANANCHI FURSA ZA UWEKEZAJI ILI WAJIKWAMUE KIUCHUMI

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa UTT AMIS, Bw. Simon Migangala, akimuongoza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kulia), alipowasili katika Ofisi za Mfuko huo katika ziara ya kikazi ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (katikati) akisikiliza maelezo kuhusu mitambo ya kuhifadhia taarifa za wateja wa Mfuko wa UTT AMIS, alipotembelea taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa UTT AMIS, Bw. Simon Migangala, akizungumza jambo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kulia), alipotembelea taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Viongozi wa Menejimenti ya Mfuko wa UTT AMIS, wakisikiliza kwa makini maagizo ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (hayupo pichani), kuhusu kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kunufaika na Mfuko huo.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) (wa tano kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa UTT AMIS, Bw. Simon Migangala, wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Menejimenti ya Mfuko huo, jijini Dar es Salaam.

(Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam)

Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam.

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza Kampuni ya Uwekezaji ya Pamoja-UTT-AMIS kutoa elimu zaidi ya uwekezaji kwa wananchi wakiwemo wastaafu wanaokabiliwa na changamoto kubwa ya kufanya uwekezaji wa mafao yao ya uzeeni kwenye miradi isiyo na tija na kuwasababishia hasara.

Mheshimiwa Masauni alitoa maagizo hayo alipotembelea Taasisi ya UTT-AMIS inayosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake katika Taasisi zinazosimamiwa na Wizara hiyo, Jijini Dar es Salaam

Alisema kuwa uwekezaji kwenye mifuko inayosimamiwa na UTT-AMIS umekuwa na tija kubwa na kwamba licha ya mfuko huo kufanya vizuri na kutoa faida inayomnufaisha mwekezaji, watu wengi hawana taarifa muhimu kuhusu mfuko huo na kuuagiza uongozi kuongeza kasi ya kujitangaza.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mfuko huo unaoendesha mifuko 6 ya uwekezaji, ukiwemo mfuko wa Umoja, Wekeza, Watoto, Jikimu, Ukwasi na Hati Fungani, Mkurugenzi Mtendaji wa UTT-AMIS, Bw. Simon Migangala, alisema kuwa mfuko wake umefanikiwa kuongeza mtaji kutoka shilingi bilioni 290.7 hadi shilingi bilioni 619.6 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.