Na.Kassim Abdi. OMPR.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuthamini na kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na wafanyabiashara wazalendo katika kutoa huduma za jamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati akipokea msaada wa vifaa mbali mbali vilivyotolewa na mfanyabiashara mzalendo Said nassir nassor Bopar katika viwanja vya Ukumbi wa Sheik Idriss Abduwakili Kikwajuni.
Alisema msaada wa Mashine Kumi (10) zilizotolewa na mfanyabiashara huyo kwa mamlaka ya maji Zanzibar inadhihirisha wazi uzalendo aliokuwa nao Bw. Bopari katika kutatua shida mbali mbali zinzowakabili wananchi wa Zanzibar.
Kupitia hafla hiyo ya Makabidhiano Mhe. Hemed alitoa wito kwa wafanyabiashara wengine kuiga mfano wa Bw.Bopar kwa kujitokeza kusaidia katika masuala ya huduma za jamii.
Kuhusu vifaa vilivyotolewa kwa Wizara ya Afya, Ustawi wa jamii,Wazee jinsia na watoto Makamu wa Pili wa Rais aliuomba uongozi wa Wizara ya Afya kuvitumia vifaa hivyo kwa uwangalifu kwa kuzingatia matumizi sahihi kwa walengwa waliokusudia.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Makamu wa Pili wa Rais mfanyabiashara Said Nassir Bopar alisema kukabidhi kwa vifaa hivyo kunatokana na ahadi yake alioitoa mbele ya Mhe. Hemed wiki mbili zilizopita ambapo mashine hizo zinalenga kwenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Akitoa Shukrani baada ya kukabidhiwa mashine za maji Waziri wa Maji na Nishati Mhe. Suleiman Masoud Makame aliahidi kuwa wizara anayoisimamia kupitia mamlaka ya maji Zanzibar itazitumia mashine hizo kama ilivyokusudiwa ili kutatua tatizo la upatikanaji wa maji hasa katika maeneo yaliokuwa yakikabiliwa na shida ya maji kwa muda mrefu.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mashine Kumi za maji, Magodoro hamsini, Viti vya kubebea wagonjwa hamsini, Biskuti Mia Tatu, Dawa za Meno, Mchele Kg 3000 kwa ajili ya wagonjwa,Vitakasa Mikono pamoja na vifaa vyenginevyo.
No comments:
Post a Comment