Habari za Punde

Jitihada za Baraza la Kiswahili la Taifa Zinavyowezesha Kubidhaisha Lugha ya Kiswahili

Na Jovina Bujulu-BAKITA

Kiswahili ni miongoni mwa lugha kumi zinazotumiwa na watu wengi duniani. Chimbuko la lugha hii ni Tanzania na inakadiriwa kutumiwa na watu zaidi ya milioni 200.                        

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), ndicho chombo chenye dhamana ya kuendeleza, kusimamia na kuratibu shughuli za wadau wote wanaokuza Kiswahili nchini Tanzania na pia Baraza hili ni mdau muhimu wa maendeleo ya Kiswahili kimataifa.

Miongoni mwa majukumu ya BAKITA ni kuhimiza matumizi fasaha ya Kiswahili na kuzuia upotoshaji wake, kushirikiana na mashirika ya kitaifa, asasi, au vikundi na watu binafsi katika kuendeleza lugha hii, kushauri pamoja na kusimamia shughuli za ukuzaji wa Kiswahili na ubidhaishaji wake.

Tangu kuanzishwa kwa BAKITA mwaka 1967, Baraza limeendelea kufanya juhudi mbalimbali ambazo zimewezesha kuipaisha lugha hii kitaifa, kikanda na kimataifa. Aidha, juhudi hizo zimewezesha Kiswahili kuwa lugha ya mawasiliano mapana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuwa moja ya lugha rasmi na lugha ya kazi katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU).

Fauka ya hayo, Kiswahili kimekubalika kutumika katika mashirika mbalimbali ya Kimataifa kama vile Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na pia kinafundishwa katika vyuo mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na kutangazwa katika idhaa mbalimbali za redio za kimataifa kama vile, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW Swahili) na redio Sauti ya Amerika (VoA), Redio Japan, Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

 

Hivi karibuni  BAKITA limepokea vifaa vya kisasa vya kufundishia ukalimani ambavyo vimenunuliwa na Serikali kwa kiasi cha shilingi mil. 187.5. Vifaa hivyo vitaliwezesha BAKITA kutoa mafunzo ya msasa na kuwasajili wakalimani watakaotumiwa vifaa hivyo katika mikutano mbalimbali kitaifa na kimataifa.

 

Akizindua vifaa hivyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Bashungwa alisema kupatikana kwa vifaa hivyo kumetimiza malengo ambayo Serikali ilijiwekea katika kukuza lugha ya Kiswahili kwani lugha hiyo inawaunganisha Watanzania na watu wa mataifa mengine kuwa wamoja katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa.

 

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa vifaa hivyo iliofanyika Jijini Dar es Salaam katika Ofisi za BAKITA Mhe. Bashungwa alisema kuwa Kiswahili hivi sasa kinazidi kuenea kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kwani kinatumia katika vyombo mbalimbali vya habari duniani, kufundishwa katika shule, vyuo na taasisi nyingine za elimu za kimataifa na hata kwa mtu mmoja mmoja katika mataifa mengi duniani.

 

“Chimbuko la Kiswahili ni hapa kwetu Tanzania, tuna wajibu mkubwa wa kukiendeleza zaidi kwa kuwasaidia wengine wanaokitafuta kwa kuwapatia rasilimali mbalimbali zitakazo wawezesha kukielewa na kukitumia kwa usanifu na ufasaha zaidi. Moja ya rasilimali hizo muhimu ni utaalamu huu wa ukalimani,” amesema Bashungwa.

 

Aidha, Mhe. Bashungwa alisema kuwa Serikali inasimamia vema azma ya kukuza lugha hii ili iendelee kuwa kuwa lulu ya mawasiliano duniani, na  alifanya kikao na watendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa Jijini Dar es Salam ambapo pamoja na mambo mengine aliagiza kuboresha Mkakati wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili wa Miaka 10 unaoanzia mwaka 2021-2031 na mara baada ya hapo uzinduliwe na uanze kutekelezwa.

Katika kufanya maboresho ya mkakati huo, Waziri Bashungwa aliwaagiza BAKITA kuongeza ufunguzi wa vituo maalumu vya kufundishia lugha ya Kiswahili na Utamaduni wa Mtanzania katika nchi mbalimbali duniani.

Naye Kaimu Katibu wa BAKITA, Consolata Mushi amesema kutokana na kuongezeka kwa mawanda ya matumizi ya lugha ya Kiswahili, Baraza limeweka mipango mipya ya kukidhi ongezeko hilo ili kuwezesha nchi na wataalamu wake kunufaika na fursa za Kiswahili zinazojitokeza duniani.

“Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuendeleza kanzidata ya wataalamu wa Kiswahili, kutoa mafunzo ya kunoa stadi kwa wataalamu mbalimbali hususani wafasiri na wakalimani, waandishi na wahariri, walimu pamoja na wakalimani”, amesema Mushi.

Mipango mingine ni kuandaa Mkakati wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili nchini na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia 2021 hadi 2031. Utekelezaji wa Mkakati huu utahusisha wadau mbalimbali kutoka Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Sekta binafsi. Lengo ni kukuza kukuza Kuswahili ili kitumike kama chachu na bidhaa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ndani na nje ya nchi.

Malengo mengine ya mkakati huo ni kuimarisha matumizi ya teknolojia katika kufundisha Kiswahili kwa njia ya mtandao, kuimarisha ushirikiano na mashirika, taasisi mbalimbali na nchi nyingine katika kusambaza na kubidhaisha Kiswahili pamoja na kuanzisha programu ya kujifunza Kiswahili kwa ajili ya watalii wanaoingia nchini kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali.

Aidha, Mkakati huo utahusu kuendeleza kanzidata ya Baraza ya wataalamu wa Kiswahili ambapo kwa sasa idadi yao ni 1,325. Uingizaji wa wataalamu hao ulifanywa kwa kutumia programu maalumu ya kikompyuta iliyoundwa na Baraza.

Miongoni wa taarifa nyingine zinazoingizwa katika programu hiyo ni aina ya lugha nyingine ambazo mhusika anazimudu vizuri, maeneo ya ubobezi katika taaluma ya Kiswahili, pamoja na ujuzi mwingine alionao mtaalamu kama vile kutumia programu za kompyuta zinazoweza kumsaidia katika ufundishaji na utafiti wa Kiswahili.

“Kuwepo kwa mfumo huo, kutasaidia nchi kutambua idadi ya wataalamu wa Kiswahili waliopo na maeneo yao ya ubobezi. Hatua hii ni njia muafaka ya kutumia fursa za lugha ya Kiswahili zilizopo ndani na nje ya nchi”, ameongeza Mushi.

Mbinu nyingine zinazotumiwa na Baraza katika kubidhaisha Kiswahili ni kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Kiswahili ambapo mpaka sasa takribani wataalamu 1,097 kutoka mikoa 12 wamekwishapatiwa mafunzo hayo ambao walifundishwa mbinu mpya za kufundisha na kutumia vifaa mbalimbali vya ufundishaji ikiwa ni pamoja na vile vinavyotumia teknolojia ya kompyuta.

Baraza pia limekuwa likitumia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kukuza na kusambaza Kiswahili. Hii inatokana na kwamba vyombo hivyo vinawafikia wananchi walio wengi. BAKITA limekuwa likiendesha vipindi mbalimbali katika redio, televisheni, magazeti na mitandao ya jamii kuelimisha umma matumizi sahihi, sanifu na fasaha ya Kiswahili.

Akizungumzia umuhimu wa Mkakati wa ubidhaishaji wa Kiswahili, Mushi alisema kuwa utasaidia kukua na kuendelea kwa Kiswahili ndani na nje ya nchi, kutumika kwa Kiswahili sanifu na fasaha, kuwepo kwa takwimu za wataalamu wa Kiswahili walionolewa vyema katika tafsiri, ukalimani, ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa ushirikiano miongoni mwa wadau mbalimbali hususani sekta za umma na binafsi katika ukuzaji na uendelezaji wa Kiswahili. Utekelezaji wa masuala hayo utaleta matokeo chanya katika kutanua wigo wa matumizi ya Kiswahili na ubidhaishaji wake.

 

MWISHO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.