Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mwanza
Mwanadamu hupewa jina ili
kumtambulisha ili atofautishwe na watu wengine. Jina hilo linaweza kuwa linamtambulisha
yeye binafsi au cheo chake katika
taasisi hata nafasi yake katika nchi.
Siku ya Jumatano Agosti 08,
2021 itakumbukwa na Watanzania pamoja na dunia kwa ujumla kwa kuwa Machifu wa
Tanzania wamempata Chifu wao Mkuu wa kwanza mwanamke ambaye pia ni Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akichukua nafasi ya
mtanglulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Kwa kukabidhiwa kwake
madaraka hayo, kunamfanya apewe jina ambalo ndilo linalomdhihirisha kuwa yeye
ni Kiongozi Mkuu wa Kitaifa kuwaongoza Machifu wenzake na Watanzania kwa
ujumla.
Ilikuwa majira ya saa sita
kuelekea saa saba mchana katika Viwanja vya Red Cross eneo la Kisesa wilaya ya
Magu mkoa wa Mwanza ndipo Mhe. Rais Samia alipewa jina la Hangaya wakati
alipokuwa anakabidhiwa madaraka ya kuwa Chifu Mkuu nchini.
Jina hilo, Hangaya lina
maana ya nyota angavu ya asubuhi inayoonesha matumaini linasadifu nafasi ya
Mhe. Rais Samia ambayo Watanzania wana matumaini makubwa kwa uongozi wake kwenye
maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Ili kuwa Chifu kamili,
Kiongozi huyo wa Machifu nchini, Chifu Hangaya alifanyiwa ibada ya kimila
iliyokuwa na sala maalumu ya kumuombea siha njema, dhima na dhamana ya kuwa kiongozi
hodari na mahiri kwa taifa analoliongoza.
Sala hiyo iliongozwa na
maneno kuntu ambayo yalishamirisha sherehe hiyo adhimu iliyokuwa imefurika hadhira
iliyohudhuria Tamasha la Utamaduni la siku mbili kuanzia Septemba 7 hadi 8,
2021. Tamasha hilo liliandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) kwa lengo la
kulinda mila na desturi za Mtanzania liliongozwa na kaulimbiu isemayo,
“Turithishe Utamaduni Wetu, Tudumishe Utamaduni Wetu, Amani na Umoja ni Tunu
Zetu.”
Kwa mujibu wa Makamu
Mwenyekiti wa Machifu Tanzania, Chifu Msagata wa Uchifu wa Unyanyembe
Tabora alisema “Sasa una mamlaka ya
kuwaita watu kwa vikao vyako kwa sababu una mamlaka, wewe ni kiongozi shupavu,
imara, mkakamavu, mweledi, uwaongoze watu wako kwa amani.”
Kiongozi huyo mpya amekabidhiwa
vitendea kazi mbele ya jopo la Machifu na Watanzania ikiwa ni alama ya
kusimamia himaya yake ya kiutawala yaani Taifa la Tanzania akisaidiwa na Machifu
hao katika maeneo yao. Miongoni mwa vitendea kazi hivyo ni pamoja na nguo
nyeusi,nguo nyekundu, ngozi ya chui, ushanga ulio na yai la mbuni, kiti cha
utawala, ngao na mkuki pamoja na usinga.
Ili kujua maana ya vifaa
hivyo, mwandishi wa makala haya alichukua wasaa wa kuonana na Chifu Aron
Mikomangwa Nyamilonda wa Uchifu wa Jiji la Mwanza unaojumuisha Halmashuri za
Ilemela na Nyamagana ambaye ni mbobezi wa masuala ya utamaduni wa kabila la Wasukuma
na kueleza kuwa, nguo nyeusi aliyovikwa Chifu Hangaya ni alama ya mawingu meusi
yanayoleta mvua ili wananchi walime na kupata chakula. Chifu anapovaa nguo
hiyo, maana yake Watanzania wanapomuona kiongozi wao wanapata matumaini ya
kupata mafanikio kupitia kiongozi wao chini ya uongozi wake mahiri.
Aliendelea kusema kuwa, nguo
nyekundu aliyovikwa Chifu Hangaya ni alama ya ulinzi, Chifu Hangaya anapaswa
kuilinda nchi yake. Kwa nafasi yake Rais ni mlinzi wa kwanza wa nchi yake na
watu wake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifaa kingine alichokabidhiwa
Chifu Hangaya Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
ngozi ya chui ambayo alivikwa ikiwa ni ishara na alama ya upole na ulinzi wakati
wote. Chifu Mikomangwa alisema “Muogope sana chui akiwa na watoto wake ukimkanyaga
atakumaliza.”
Kwa muktadha wa Rais Mhe.
Samia kukabidhiwa madaraka hayo, yeye ndiye Chifu Mkuu na chini yake wapo
Machifu na Watanzania kwa ujumla wao ambao wanamuombea awe mpole awe na mwangalifu
kwa watu wote wenye nia ovu na Tanzania.
Vile vile katika hafla hiyo
Chifu Hangaya Samia alivikwa ushanga wenye yai la mbuni, ndege huyo ni
mwangalifu sana katika kulinda mayai na watoto wake. Hivyo, Watanzania ndiyo
mayai na vifaranga wa Chifu Hangaya Samia ambaye anawajibu wa kuwalea,
kuwatunza na kuwalinda Watanzania.
Hali kadhalika Mhe. Rais
amekabidhiwa kiti chenye mguu mmoja ambacho ni alama ya utawala mmoja ambacho
hakikaliwi na mtu mwingine zaidi yake. Mikomangwa alisema Hangaya anapokaa
katika kiti chake cha kiutawala, hukaa na Watanzania ili kujenga na kuendeleza
nchi na watu wake.
Pia, amekabidhiwa ngao na
mkuki akiwa kiongozi na Mkuu wa Mchifu nchini ili aweze kulinda nchi yake na
watu wake kupitia majeshi ya Ulinzi na Usalama ambapo yeye ni Amiri Jeshi Mkuu.
Mwisho ila siyo kwa umuhimu,
alikabidhiwa usinga unaotokana na singa za mikia ya nyumbu ambao tafsiri yake
ni watu. Usinga kwa muonekano na uhalisia wake una manyoya mengi, haya
yanawakilisha uwingi wa watu alionao Chifu Hangaya ambao ni Watanzania.
Amekabidhiwa ili awalinde kwa amani.
Hakika Chifu Hangaya Samia
Suluhu Hassan ameanza kazi yake ya Uchifu mara moja ambapo alisema Tanzania ipo
kwenye mchakato wa kuandaa Sera mpya ya Utamaduni itakayoendana na mazingira ya
sasa ya dunia lakini itakayolinda maadili Mtanzania.
Hivyo, mara baada ya
kukabidhiwa madaraka hayo aliagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo ambayo ndiyo yenye dhamana na Utamaduni kupata maoni kutoka kwa Watemi
na Machifu.
“Na niagize Wizara, katika
maadalizi ya mchakato wa Sera hii, lazima tupate maoni kutoka kwa Watemi na
Machifu wetu, maoni yao yaingizwe kweye Sera hii ili tuendeleze utamanuni wetu.
Na ni imani yangu kuwa hatua hizi zitasaidia kulinda, kuenzi na kukuza
utamaduni wetu” alisisitiza Rais Mhe. Samia.
Ujio wa Machifu wengi katika
hafla hiyo ya kukabidhiwa madaraka hayo kwa Chifu wao Mkuu Hangaya Samia Suluhu
Hassan ni udhihirisho na imani ya Watanzania wote kusimama imara na kuhakikisha
kaulimbiu ya uongozi wake ya “Kazi Iendelee” inakuwa mwanzo mpya wa kuhakikisha
utamaduni wa Mtanzania utaendelea kujulikana kote kupitia filamu ya “Royal
Tour” inayoandaliwa kuitangaza Tanzania duniani.
Katibu
Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya Filamu ya “Royal Tour”, Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa
filamu hiyo ni fursa adhimu ambayo itasaidia kutangaza rasilimali za Tanzania
huku akinukuu maneno ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alisema “Baada ya
kukamilika kwa filamu hii itakayotangaza utalii, biashara na fursa za uwekezaji
nchini kupitia kipindi maarufu cha Royal Tour, dunia itafahamu kuwa madini ya
Tanzanite yanachimbwa Tanzania pekee.”
Maneno
hayo yalisemwa na Rais Septemba 5, 2021 akiwa mkoani Manyara wakati akizungumza
na wananchi wa Mirerani na kuongeza kuwa ni faraja na ushahidi dhahiri kuwa eneo
hilo ni mahali pekee yanakochimbwa madini ya Tanzanite duniani.
Sasa
ni wakati wa kuutangaza utamaduni wa Mtanzania duniani ili kuakisi maneno ya
Mwasisi wa Taifa la Tanzania, Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere ambaye
aliwahi kusema “Utamaduni ni kiini ama roho ya taifa lolote, taifa lisilo na
utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu usio na roho.”
Kupitia
Tamasha la Utamaduni la Kisesa Mwanza, Rais Mhe. Samia ametoa mwanga na hamasa kwa
makabila yote nchini kuanzisha matamasha katika maeneo yao ili kutambulisha
mila na desturi zilizopo katika maeneo yao na kutangaza fursa za kiutamaduni na
utalii hatua itakayosaidia kukuza uchumi katika mikoa yote na kila pembe ya
Tanzania.
Matamasha
hayo yamekwisha anza kufanyika katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Manyara, Dodoma
na Mbeya. Sasa ni zamu yenu mikoa mingine kuwa na matamasha yanayowapa fursa ya
kutangaza utamaduni wenu na kuwapa fursa Watanzania kufanya utalii wa ndani
katika mikoa yenu ili kuweza kujifunza mila, desturi, historia na tamaduni za
makabila mbalimbali yaliyopo nchini. “Hakika Kazi Iendelee.”
Mwisho
No comments:
Post a Comment