Habari za Punde

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ametoa Bilioni 2.6 Ujenzi wa Kituo cha Kuegesha Magari Makubwa Nyakanazi.

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokagua ujenzi wa Kituo cha Kuegesha Magari Makubwa cha Nyakanazi mkoani Kagera, Septemba 18, 2021. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Ibuge na wa pili Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye
Muonekano  wa Kituo cha Kuegesha Magari Makubwa cha Nyakanazi  ambacho Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake September 18, 2021. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kituo cha kimkakati cha maegesho ya magari makubwa katika eneo la Nyakanazi wilayani Biharamulo, Kagera.

 

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 18, 2021) wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Nyakanazi baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho ambao unagharimu sh. bilioni 2.6 na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2021.

 

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa kuwaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera wahakikishe wanasimia vizuri miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ukiwemo na huo wa ujenzi wa kituo cha maegesho ya magari makubwa kwa maendeleo ya wananchi.

 

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo kuhakikisha eneo la Nyakanazi linapimwa na kuanisha matumizi ya kila eneo ikiwemo makazi, Huduma za Jamii, Viwanda, Viwanja vya Michezo na maeneo mbalimbali ya uwekezaji

 

Kwa upande wake, Mhandisi wa TARURA wa wilaya ya Biharamulo, Julius Sumaye ambaye ndiye msimamizi wa ujenzi wa mradi huo amesema unalengo la kuongeza mapato ya halmashauri ili iweze kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu.

 

Amesema halmashauri yao imetenga eneo la ukubwa wa hekta 10 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya uwekezaji ambapo kati yake hekta 3.2 zimetumika katika ujenzi kituo hicho, hekta 2.3 ni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi na hekta 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya biashara.

 

Mhandisi huyo amesema kwa awamu ya kwanza wameanza na ujenzi wa mradi wa kituo cha kuegeshea magari makubwa chenye uwezo wa kuegesha malori 300 kwa wakati mmoja. Mradi huo umefikia asilimia 48 ya utekelezaji wake.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAMOSI, SEPTEMBA 18, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.