Na.
Georgina Misama – MAELEZO
Septemba
03, 2021
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imepunguza tozo
kwa asilimia 30 baada ya kusikia malalamiko ya Watanzania, na kuwasisitiza umuhimu wa tozo hizo katika
kukamilisha miradi mikubwa iliyoachwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na pia
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo vituo 220 vya afya, pamoja na
miradi ya elimu, maji na umeme ambayo inakwenda moja kwa moja kwa
wananchi.
Akizungumza na wakazi
wa jimbo la Kawe Jijini Dar es
salaam leo, wakati akiwa njiani kuelekea
Bagamoyo katika ziara yake ya kurekodi vivutio vya utalii ili kuitangaza
Tanzania, Rais samia alisema kwamba Serikali iliweka tozo ya miamala ya simu
ili kukusanya fedha kwa ajili ya maendeleo na kuwahakikishia kukamilika kwa
miradi hiyo kama ilivyopangwa kwa faida ya watanzania wote.
“Katika bajeti
iliyopita tuliweka tozo kwenye miamala ya simu ambayo imepigiwa kelele kila mahali.
Nimesikia malalamiko yenu, nimekaa na wataalam wangu, tumepunguza asilimia 30
lakini hatutozifuta kabisa tozo hizo kwasababu fedha tutakazopata zitatusaidia
kutekeleza miradi yetu wenyewe, pasipo kuingiliwa, hakuna wa kutujengea
madarasa pasipo sisi wenyewe”, alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia
alisema kwamba fedha zitakaozokusanywa kwa miezi ya Septemba na Oktoba,
zitatumika kujenga vyumba vya madarasa zaidi ya 500 Tanzania nzima ili
kuwaandalia wanafunzi wanaotarajiwa kuingia sekondari mwakani na pia wale
watakaoanza shule ya msingi ikiwemo shule aliyoomba mbunge wa Kawe Mhe.
Josephat Gwajima katika mkutano huo.
“Misaada siku hizi ni
michache sana, lazima tuminyane wenyewe kwa wenyewe ili tujiletea maendeleo,
tuna wimbi kubwa la watoto wanataka madarasa kuingia sekondari na wengine
wataanza darasa la kwanza, niwahakikishie tutakwenda kuikamilisha miradi hiyo
kama ilivyopangwa”, alisisiza Rais Samia.
Kwa upande wake Mbunge
wa Jimbo la Kawe Mhe. Josephat Gwajima alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa
kuwawapatia fedha kiasi cha shilingi
bill.8 ambazo zimetumika kujengea mifereji katika kata ya Mbweni ambayo
ilikuwa inakabiliwa na mafuriko, lakini pia kwa kupokea shilingi Bil.14 kwa ajili
ya ujenzi wa barabara za ndani 115
katika jimbo hilo.
“Tunakushukuru Mhe.
Rais kwa mambo makubwa uliyotufanyia, ulituahidi kutupa bill.8 ili zitusaidie
kujenga mifereji katika kata ya Mbweni ambayo ilikuwa na changamoto ya
mafuriko. Tayari fedha hizo tumeshapokea na kazi ya kujenga mifereji inaendelea,
aidha, tunakushukuru kwa kutupatia bill.14 kupitia mkono wa TARURA ili kujenga
barabara hizo”, alisema Mhe. Gwajima.
Aliongeza kuwa hivi
sasa wapo kwenye kukamilisha mradi wa maji ambapo unatarajiwa kukamilika
ifikapo Oktoba 15 mwaka huu kwenye vijiji
vya Nakasangwe na Kisanga vinavyokabiliwa na changamoto hiyo.
Mhe. Gwajima pia
alimuomba Rais Samia kuwajengea shule wakazi wa Wazo ambao hivi sasa wanalazimika kuvuka
barabara ili kwenda kwenye shule za Kunduchi na kusababisha kugongwa na magari
wakati wakivuka barabara kubwa ya Bagamoyo, ambapo changamoto hiyo ilitatuliwa
hapo hapo na Mhe. Rais.
No comments:
Post a Comment