Habari za Punde

WEMA Itaendelea Kusimamia Michezo Inakuza Mashirikiano na Kutoa Vipaji Kwa Wanafunzi.

Na Maulid Yussuf WEMA ZANZIBAR.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw.Ali Khamis Juma amesema Wizara ya elimu itaendelea kusimamia michezo kwani inakuza mashirikiano kutoa vipaji kwa Wanafunzi.

Amesema hayo wakati wa. ufunguzi wa Kongamano la michezo katika Skuli, kwa  wadau mbalimbali wa Michezo, katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Unguja amesema  michezo huwaleta Wanafunzi karibu na kupelekea kukuza sekta ya elimu  nchini.

Amesema Mwanafunzi kushiriki katika michezo humsaidia sana kuepukana na vitendo viovu  pamoja na kuchangia kukua vyema kiakili pamoja na afya yake.

Amesema  Rais wa awamu ya saba Dk Ali Mohammed Shein aliunda kamati maalum ya kuhakikisha michezo inarudi katika hadhi yake hasa katika Skuli, hivyo kuna umuhimu kwa wadau hao kutoa michango yao ili kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.

Amesema bado Zanzibar inahitaji mabalozi wa michezo kwenye Mataifa mbali mbali Duniani, hivyo ni vyema kushirikiana kuwajenga mabalozi hao kupitia  Skuli.

Aidha amekiri kuwepo kwa matatizo mbalimbali ya kimichezo ndani ya Wizara ambapo tayari ameshaweka muongozo ili uweze kujadiliwa ndani ya Mkutano huo na kupata maendeleo.

Hivyo amesema kongamano hilo litasaidia sana Wizara kuweza kupata muongozo mzuri wa kuimarisha michezo nchini.

Amesema muda umefika kwa kila mtu kujua nafasi yake na wajibu wake ili kuweka mikakati sahihi ya kuhakikisha Zanzibar inakua na vipaji mbalimbali vya michezo kupitia Skuli.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya michezo Wizara ya Elimu Zanzibar bi Sichana Haji Foum amesema michezo ina umuhimu wake na ndio maana Wizara imeanzisha Idara maalum ya michezo kwa lengo la kuzalisha vijana wenye  taaluma na afya imara.

Amesema kongamano hilo litasaidia kupanga mikakati ya kuimarisha michezo katika skuli za maandalizi, msingi, sekondari hadi vyuo.

Nae Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Michezo katika Idara ya Michezo Wizara ya Elimu  na Mafunzo ya Amali, mwalimu Musa Abdurabi amesema lengo la kongamano hilo ni kuelimisha jamii juu ya1 umuhimu wa michezo katika skuli mbalimbali.

Amesema kongamano hilo litasaidia kuibua changamoto za tasnia ya michezo katika Skuli ili kuwa na mfumo bora endelevu na kuzalisha wanamichezo mahiri.

Wakitoa michango yao washiriki wa kongamano hilo wameshauri Serikali kuweka bajeti maalum juu ya masuala ya mochezo pekee ili kuweza kuibua vipaji vya watoto.

Wanafunzi wa somo la michezo nao wameiomba Serikali kujenga Skuli maalumu ya kisasa itakayohusu michezo pekee pamoja na kuweka vifaa vya kutosha ili kuibua vipaji vya Watoto nchini.

Kongamano hilo limefanyika ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 57 ya tamasha la elimu bila malipo ambapo huadhimishwa kila mwaka  septemba 23.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.