. Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiwapa chakula Samaki wanaofugwa
katika sehemu ya vizimba vya Kampuni ya TanGreen vilivyowekwa ndani ya ziwa
Victoria. Ulega alifanya ziara katika eneo la Kampuni hiyo ya Kichina ambayo inajishughulisha na ufugaji wa samaki
kwa kutumika vizimba.
Naibu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akiongea na Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, Mhandisi Robert Ruhumbi (katikati) alipomtembelea ofisini kwake
Septemba 27, 2021. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid
Tamatamah.
Na Mbaraka Kambona, Mwanza
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga
kufanya mpango wa matumizi bora ya ziwa Victoria ambao utaainisha maeneo ambayo
yatatumika kufanya ufugaji wa vizimba
ili kutoa nafasi pia kwa shughuli za uvuvi wa asili kuendelea bila kuwa
na muingiliano.
Ulega aliyasema hayo Septemba 27, 2021 alipotembelea eneo la
Kampuni ya Kichina ya Tangreen
iliyowekeza katika mradi wa ufugaji wa Samaki kwa kutumika vizimba kandokando
ya ziwa Victoria, jijini Mwanza.
Alisema kuwa serikali imedhamiria kufanya hivyo ili
kupunguza muingiliano wa shughuli za ufugaji wa Samaki na Uvuvi wa asili ili
shughuli zote zifanyike kwa ufanisi na kuleta tija katika uchumi wa buluu.
"Mpango wa Serikali ni kuhakikisha ufugaji wa vizimba
unafanyika katika maeneo maalum na sio kila mahala, tuwe na maeneo mahsusi ya
kazi hii ili kutoa nafasi pia wavuvi wa asili
waweze kuendelea na shughuli zao," alisema Ulega
Waziri Ulega alisema kuwa mpango huo pia utavutia wawekezaji
wengi kuwekeza katika ziwa Victoria, na wao kama Serikali wanawakaribisha
wawekezaji kama TanGreen kuja kuwekeza nchini.
"Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira
mazuri ya uwekezaji, na hivi karibuni tumemuona akifanya jitihada kubwa kwa
kuitangaza nchi yetu katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kufungua milango
ya uwekezaji, na moja ya maeneo ya uwekezaji aliyokuwa akiyatangaza ni katika
uchumi wa buluu," alisema Ulega
Aliongeza kuwa TanGreen imejikita katika kukuza uchumi wa
buluu kwa kufuga Samaki wa vizimba na wanatarajia kuvuna Tani Elfu kumi (10,
0000) kwa mwaka, huku akisema kuwa kwa sasa nchini samaki wanaovuliwa kutoka
kwenye mabwawa ni Tani Elfu Ishirini na
Mbili (22,000) hivyo TanGreen wanakwenda kuzalisha nusu ya kile kinachozalishwa
sasa nchini.
Aidha, alimuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salim Mkali
kuhakikisha muwekezaji huyo analindwa,
na kama kutakuwa na wadokozi wenye nia ya kuirudisha nyuma kampuni hiyo wawachukulie hatua kali.
Ulega aliendelea kusema kuwa bado kunahitajio kubwa la
Samaki nchini, kiasi kinachohitaji kwa mwaka ni Tani Laki Saba (700, 000)
wakati uwezo uliopo kwa sasa Ni kuzalisha Tani Laki Nne (400, 000) hivyo
kufanya pungufu ya Tani Laki Tatu (300,000)
huku akisema ufugaji wa vizimba ukifanyika vizuri utasaidia kupunguza
changamoto hiyo nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Ruhumbi alisema
kuwa wamejipanga kuufanya Mkoa huo kuwa mzalishaji mkubwa wa Samaki wa kufugwa
katika mabwawa.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid
Tamatamah alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea
kuhamasisha uwekezaji wa mitaji na wamehamasisha mabenki kama Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na
imeshaanza kutoa mikopo, huku akisema wanaendelea kuwashawishi wawekeza wakubwa
wa mitaji kuwekeza katika ufugaji wa samaki na kukuza uchumi wa buluu.
"Hivyo unaweza kuona kuwa ushawishi tulioufanya ndio
umepelekea wawekezaji wakubwa kama TanGreen kujitokeza na kwa kweli imeleta
tija kwa sababu miaka mitatu iliyopita kulikuwa na vizimba 18, lakini kwa sasa
tunavizimba 473 na asilimia 77 ya vizimba vyote
vipo hapa ziwa Victoria," alisema Dkt. Tamatamah
Awali, Daktari wa Samaki wa Kampuni ya TanGreen, Dkt. Mugure
Katwiga Mariwanda akisoma taarifa fupi ya Kiwanda hicho alisema kuwa moja ya
lengo la Kampuni hiyo ni kukuza na
kutangaza teknolojia ya ufugaji ikiwemo
kufungua fursa ya ajira kwa vijana.
"Mhe. Naibu Waziri, pamoja na jitihada tunazoendelea
nazo lakini tunakumbana na changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa vifaranga vya
Samaki ndani ya nchi, baadhi ya wavuvi kuingia ndani ya mradi kuiba au kuharibu
miundombinu," alisema Dkt. Katwiga Mariwanda
Aliongeza kwa kuiomba Serikali itoe vibali vya kuingiza
vifaranga vya samaki kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji yaliyopo huku
akiiomba Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii ya wavuvi juu ya uwekezaji wa
vizimba ili waache kufanya shughuli za uvuvi katika mradi huo.
No comments:
Post a Comment