Habari za Punde

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Yapokea Taarifa ya Utekelezaji wa Sheria ya Ajira kwa Wageni Nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa sheria ya ajira kwa wageni katika ukumbi wa Bunge, Oktoba 26, 2021 Jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheri Mhe. Najma Giga akizungumza katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria katika ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.
Kamishina wa Kazi Brig.Gen. Francis Mbindi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa sheria ya ajira kwa wageni mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria katika Ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifuatilia kikao cha kamati hiyo katika Ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.


Na: Mwandishi Wetu - DODOMA.

SERIKALI imesema kufuatia uwepo wa Sheria za wageni nchini na wawekezaji kumesaidia kuwepo mfumo wa uratibu na mamlaka ya kusimamia shughuli za sekta hiyo ili kuleta ustawi wa watanzania na Taifa kwa ujumla.

Hayo yalisemwa Oktoba 26, 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.  Jenista Mhagama wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipokutana na kupokea taarifa ya utekelezaji wa sheria ya ajira kwa wageni nchini katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.

 

Waziri Mhagama amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia Sheria za Kazi na miongoni mwa sheria hizo ni Sheria ya kuratibu ajira za wageni Na 1. ya mwaka 2015 ambapo sheria hiyo imeweka masharti kwa wageni wanaokuja kufanya kazi nchini.

 

“Uwepo wa Sheria ya kuratibu ajira za wageni nchini Na. 1 ya mwaka 2015 ilipelekea kuanzishwa kwa mamlaka ya utoaji wa vibali vya ajira kwa wageni, hivyo kwa kuzingatia matakwa ya sheria hii wawekezaji na waajiri wanaokusudia kuajiri wageni nchini wanapaswa kuwasilisha maombi kwa Kamishna wa Kazi na hati maalum ya kibali cha ajira itatolewa kwa mgeni husika,” alisema Waziri Mhagama

 

Mheshimiwa Mhagama aliongeza kuwa kutokana na uwezekaji mzuri unaoendelea nchini, Serikali imewataka wawekezaji ama makampuni yaliyoajiri wageni kuweka utaratibu wa urithishaji wa ujuzi kwa wazawa ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao pindi wageni hao wanapokuwa wamemaliza muda wao wa kufanya kazi nchini.

 

Naye Naibu waziri Ofisi ya waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi alisema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa kuomba vibali kielektroniki kulikuwa na mlolongo mrefu hali iliyosababisha uwepo wa vishoka na viashiria vya rushwa hivyo uombaji kupitia mfumo huo wa vibali vya kielekroniki kutavutia wawekezaji zaidi.

 

Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa sheria ya ajira kwa wageni mbele ya kamati hiyo Kamishina wa Kazi Brig. Gen. Francis Mbindi amesema Mfumo wa kushughulikia vibali vya kazi kwa njia ya kieletroniki umeongeza makusanyo ya maduhuli ya serikali.

 

“Jumla ya bilioni 17 zimekusanywa kama ada ya vibali vya kazi kuanzia Mwezi Januari hadi kufikia Mwezi Seoptemba mwaka huu  ikilinganishwa na kiasi cha billioni tatu zilizokusanywa kuanzia Mwezi Julai  hadi Septemba 2020  kupitia mfumo wa zamani wa kushughulikia vibali vya kazi,” alibainisha Brig.Gen. Mbindi. 

 

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na sheria Mhe. Edward Ole Lekaita amepongeza mabadiliko yaliyofanywa na serikali ambayo yameleta matokeo chanya na kuendela kulinda ajira za wazawa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.