Habari za Punde

SMZ Inathamini Uhusiano Mkubwa Unaoipata Kutika Mashirika ya Umoja wa Mataifa UN. -Dk. Hussein Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Maadhimisho ya Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa ( UN ) maadhimisho hayo yamefanyika Zanzibar katika Ukumbi wa Sheikh.Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana ushirikiano mkubwa inaoupata kutoka katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) yaliopo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 76 ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa, sherehe zilizofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil, Kiwajuni Jijini Zanzibar.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kazi kubwa inafanywa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyopo Zanzibar na imekuwa kiungo muhimu katika kufanikisha shughuli mbali mbali za kimaendeleo.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kupitia programu mbali mbali zinazoendeshwa na Mashirika ya UN hapa Zanzibar hasa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia na hivi sasa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza na inaedelea kunufaika sana na ushirikiano inaoupata kutoka mashirika yote ya Umoja wa Mataifa.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kupata mafanikio katika sekta ya elimu, afya, uhifadhi wa mazingira, kupunguza umasikini na idadi ya vifo vya akina mama na watoto, kuendeleza kilimo, uvuvi na ufugaji, kuwajengea uwezo wafanyakazi, uwezeshaji kiuchumi, kukuza ajira kwa vijana, kuimarisha demokrasia na utawala bora, kudumisha amani na usalama pamoja na maendeleo mengineyo.

Rais Dk. Miwnyi alitumia fursa hiyo kuyakaribisha Mashirika ya UN kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kuendeleza dira ya uchumi wa Buluu, ikiwa ni pamoja na kuendeleeza ushirikiano uliopo katika kuendeleza uvuvi pamoja na wavuvi, kilimo cha mwani na kuliongezea thamani zao hilo.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mipango ya maendeleo iliyopangwa hapa Zanzibar katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA III), na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yote imezingatia mipango mikuu ya mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kufurahishwa na kauli mbiu ya Maadhimisho ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu 2021 ambayo ni “Kujijenga upya vizuri zaidi kwa kuweka mifumo bora ya afya” (Building back Better with Health System) na kueleza kwamba kaulimbiu hiyo ina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa dunia sambamba na umuhimu wa pekee kwa maendeleo ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa idadi ya vifo na maambukizi ya maradhi ya UVIKO-19, kwa upande wa Zanzibar haikuwa kubwa kama ilivyotokea katika nchi mbali mbali, lakini athari za kiuchumi ni kubwa zaidi kuliko ilivyotokea katika baadhi ya nchi zilizokuwa na idadi kubwa ya vifo na maambukizi.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi sote, tunathamni sana sherehe hizi za maadhimisho kwani zinatupa fursa ya kufahamu na kutafakari historia ya Umoja wa Mataifa, mashirika yake, kazi na majukumu yake pamoja na michango yake kwa maendeleo ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla pamoja na mataifa yote duniani”,alisema Rais Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza vijana wabunifu na kusisitiza haja kwa viongozi wa Serikalini kuwaunga mkono vijana hao ili waweze kufanikiwa zaidi katika ubunifu wao huku akieleza azma ya Serikali ya kuweka eneo maalum kwa ajili ya ubunifu pamoja na kujenga viwanda vidogo vidogo kwa azma ya uchumi wa Zanzibar uweze kuongozwa na teknolojia.

Mapema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui alizipongeza juhudi zinazochukuliwa na UN yakiwemo Mashirika yake katika kuiunga mkono Zanzibar hasa katika sekta ya afya na kueleza jinsi mashirikiano ya pamoja yaliyooneshwa na UN katika kupambana na UVIKO-19 hapa Zanzibar.

Nae Mratibu Mkaazi wa Umoja wa  Mataifa Tanzania  Zlatan Milisic alieleza hatua mbali mbali zinazochukuliwa na UN kupitia mashirika yake hapa nchini katika kuiunga mkono Tanzania huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Tanzania katika kuendeleza uchumi wake hasa kupitia sekta ya Utalii ambapo pia, alitumia fursa hiyo kuahidi na kusisitiza kwamba UN itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza shughuli zake za maendeleo.

Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.