Habari za Punde

Majengo ya Yazingatie Mahitaji ya Sasa na Baadae -- Mhe. Othman.

 





MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amezitaka taasisi  mbali mbali nchini zinapofikiria kuwa na miradi ya ujenzi wa  majengo ya Serikali kuwa na mtazamo wa  kukidhi mahitaji makubwa ya sasa na baadae.
Mhe. Makamu ameyasema hayo leo huko hoteli ya Verde Mtoni Wilaya ya Magharib ‘A’ Unguja, alipotembelea  maonesho ya  masuala ya Ardhi, Makaazi na maendeleo ya Ujenzi yaliyoandaliwa na Wizara ya Ardhi  na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar.
Amesema majengo mengi  ya serikali yanayojengwa kwa muda mfupi huwa hayakidhi  na kutotosheleza mahitaji halisi  kwa shughuli za serikali kutokana na kuwepo fikra zisizozingatia mahitaji muhimu ya sasa na ya baaadae jambo ambalo ni makosa yanayopaswa kuepukwa yasiendelee kutokea katika shughuli za ujenzi wa majengo ya serikali.
Amesema kwa kuzingatia hali hiyo, ni vyema miradi ya ujenzi inayoanzishwa kuelekeza fikra katika majengo yenye ghorafa nyingi zaidi zitakazoweza kukidhi mahitaji makubwa yaliyopo na yajayo  kwa kipindi kirefu.
Aidha ameshauri kwamba majengo ya serikali yanayoanzishwa pia ni vyema yakazingatia utamaduni halisi wa visiwa vya Zanzibar ili kutunza na kuendeleza kielelezo rasmi cha Utamaduni wa Wazanzibari.
Pia ameishauri Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar,  kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kufikiria, kuwapungunzia mzigo wa kodi na tozo nyingi wananchi na wafanyabiashara wanapofanya miamala ya masuala ya nyumba na ardhi kwa kuwa tozo zilizopo sasa ni kubwa na zinawabebesha mzigo zaidi wananchi.
Katibu Mkuu wizara ya Ujenzi na maendeleo ya Makaazi Nd. Joseph John Kilangi, alimshukuru Mhe. Othman kwa kutembelea maonesho hayo yaliyowapa fursa wananchi kuona kazi mbali mbali zilizoandaliwa na wadau tofauti.
Kabla ya shuhuli hio Mhe.Othman alihudhuria mwaliko wa chakula cha mchana ulioandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi, kwaajili ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Burundi Gen. Evariste Ndayishimiye katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar.

Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
23.10.2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.