Habari za Punde

Mhe Hemed aitaka jamii kutokwepa jukumu la kuwalea wazee

Mratibu wa Miradi Jumuiya ya wazee wastaafu Ghanima Othman Juma akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati alipotembelea Jumuiya za wazee katika kilele cha Maadhimisho siku ya wazee Duniani kilichofanyika katika viwanja vya skuli ya Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mhe. Hemed akizungumza na wazee pamoja na wananchi waliohudhuria katika kilele cha maadhimisho siku ya wazee duniani kilichofanyika katika viwanja vya skuli ya Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  akizungumza na waumini wa mskiti wa Ijuma Mahonda mara baada ya kukamilika kwa ibada ya sala ya Ijumaa ambapo aliwaeleza waumini hao kuwa serikali ya Rais Dk. Mwinyi itawatumikia wananchi wake bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Na Kassim Abdi, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla ameitaka jamii kutokwepa jukumu la kuwalea wazee katika kuwapatia matunzo na huduma za msingi.

Mhe. Hemed ametoa wito huo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wazee duniani kilichofanyika  katika Uwanja wa Skuli ya Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema wazee wanahitaji mapenzi na huruma kutoka kwa Watoto wao na jamii inayowazunguka hivyo kuna haja kwa familia na jamii kwa ujumla kuhakikisha wazee wanapata mapenzi hayo wakiwa katika familia zao.

Alieleza kuwa, kuwalea wazee ndani ya nyumba ni jambo linaloleta barka na fanaka sambamba na kutoa mafunzo mema kwa Watoto katika kuwalea wazee wao.

“Tufahamu kwamba vitabu vitakatifu vinaeleza umuhimu na baraka ya kuwatunza wazee, Na tufahamu kuwa ukimtendea maovu mzee wako Mwenyezi Mungu anakuja kukulipa maovu na wewe” Alieleza Mhe. Hemed

Makamu wa Pili wa Rais aliesema katika kuunga mkono suala hilo Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi imeendelza dhamira na shabaha ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka mikakati ya kuwaendeleza wazee ambayo inaendelea kuimarishwa na kwa kuendelea kuwatunza wazee wasiokuwa na jamaa wala rasilimali katika makazi maalum ikiwemo Sebleni, Welezo na Limbani.

Mhe. Hemed Alifafanua Serikali imeendeleza matunda hayo kwa kuweka sera na mipnago mbali mbali za kuimarisha Ustawi na maendeleo ya wazee nchini ikiwemo kufanya mapitio ya muongozo wa pensheni jamii na kutengeneza kanuni na sheria ya wazee iliyozinduiwa mwaka 2020.

Alieleza, Mpango wa Penchini jamii umeweza kuwasiadia kiuchumi baadhi ya wazee walio wengi kwa kuzitumia fedha hizo katika shughuli ndogo ndogo za uzalishaji mali na kujiongezea kipato.

Alisema wazee waliopo katika vituo hivyo Serikali inaendelea kuwapatia huduma zote za msingi wanazostahiki ikiwemo kuwasimamia, chakula, malazi ,mavazi matibabu pamoja na posho.

Mhe. Hemed alisema Serikali inatambua umuhimu na mchango mkubwa uliotolewa na wazee katika maendeleo ya nchi na kupelekea kuanzisha program maalum ya kuwapatia pensheni wazee wote waliofikia uimri wa miaka 70 na kuendelea ikiwa ni utekelezaji wa sera na hifadhi ya jamii.

Alieleza kwamba, Idara yenye dhamana na wazee imehakikisha inaendelea kuwasajili wazee wote waliofikia umri wa miaka sabiini na wananufaika na pensheni hiyo,ili iendelee kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuimarisha huduma za wazee ikiwemo afya na usafiri , na kueleza kuwa kwa hatua ya awali jumla ya wazee Elfu mbili mia nne na arubaini na nane (2,448) wameshapatiwa vitambulisho maalum vya kuwasaidia kupata huduma hizo kwa urahisi.

Akigusia suala la malezi Mhe. Hemed aliwataka wazee kuendelea kulinda mila, silka na desturi ya wazanzibar katika malezi, ili kupunguza vitendo vya udhalilishaji katika jamii zetu.

Pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa mwenyekiti mwenza wa Kamati ya sensa ya watu na makaazi Taifa aliwaomba wazee hao kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa kupitia sensa inayotarajiwa kuanza Mwezi Agosti Mwaka Kesho.

Akisoma risala kwa niaba ya wazee Maulid Nafasi Juma alisema wazee wa Zanzibar wanampongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza Jitihaza zilizoanzishwa  na Serikali ya awamu na sab ana kuahidi kuendelea kumuunga mkono Mhe. Rais katika kupambana na vitendo viovu ikiwemo kupiga vita suala la ubadhilifu wa mali za umma.

Alisema Pamoja na mipangoz mizuri ya serikali lakini bado wazee wanakabiliwa na baaadhi ya changamoto ikiwemo wazee kubebeshwa tuhuma za uchawi ndani ya jamii, uchakavu wa majengo wanayoishi wazee, Pamoja na kuanywa nyuma katika utekelezaji wa baadhi ya mipango ya kisekta.

Aidha, katika risala hiyo, wazee waliishauri serikali kushusha umri wa wazee katika kuopkea pencheni jamii ili iweze kutoa fursa  kwa wazee wengi Zaidi waweze kupata penchini hiyo Pamoja na kuanzishwa kwa dirisha maalum katika vituo vya Afya kwa ajili ya kuwahudumia wazee.

Nae, Mkurugenzi wa Shirika la kuwahudumia wazee Duniani nchini Tanzania  (Help Age International) Smart Daniel Alipongeza serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuanzisha program maalum ya pencheni jaamii jambo ambo limepelekea baadhi ya nchi katika bara la Afrika kuiga jambo hilo ikiwemo nchi ya Kenya na Uganda kwa upande Nchi za Afrika Mashariki.

Alieleza, kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuwashirikisha wazee katika kuchangia pato la taifa hasa katika matumizi ya kidigitali.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “MATUMIZI SAHIHI YA KIDIGITALI KWA USTAWI WA RIKA ZOTE”.

Wakati wa Mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla aalijumuika na Waumini wa Mskiti wa Ijumaa Mahonda, katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Akitoa salamu zake kwa waumini hao Mhe. Hemed amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi imejipanga kuwapatia maendeleo wananchi wake bila ya ubaguzi wa aina yoyote na aliwaomba kuendelea kutoa mashirkiano yao katika kuiletea maendeleo Zanzibar.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.